![]() |
| Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon |
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amemfuta
kazi mkuu wa Ujumbe wa kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya
skendo nyingine ya udhalilishaji wa kingono kuvikumba vikosi vya ulinzi wa
amani nchini humo.
Ban amesema kuwa amemtaka Babacar Gaye kuachia ngazi, na
kwamba mwanadiplomasia huyo kutoka Senegal amewasilisha barua yake ya
kujiuzulu.
Hatua hiyo imekuja baada ya shirika la Amnesty
International kumtuhumu askari mmoja wa kulinda amani kuwa alimbaka binti wa
miaka 12. Aidha, vikosi hivyo vya Umoja wa Mataifa vilimpiga risasi na kumuua
kijana mmoja pamoja na baba yake wakati wa operesheni ya hivi karibuni kumsaka
kiongozi wa zamani wa waasi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui, limesema
shirika hilo.
Jinai hilo iliyofanyika Agosti 2 na 3 ilisababisha pia
kuuawa kwa mlinda amani kutoka Cameroon na watu wengine wanne.
Madai kama hayo ya kuwadhalilisha watoto yaliwahi
kutolewa dhidi ya askari wengine wa UN nchini humo.
“Umoja wa Mataifa inapopeleka walinda amani, tunafanya
hivyo ili kuwalinda watu walio katika hali mbaya kabisa duniani,” alisema Ban
na kuongeza, “Sitavumilia kitendo chochote cha watu wanaobadilisha uaminifu
kuwa hofu.”
![]() |
| Babacar Gaye, mkuu wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. |
Aidha, kuna tuhuma za dhulma za ngono zinazodaiwa
kufanywa na askari wa Ufaransa, huku ripoti mbalimbali zikisema kuwa
waliwadhalilisha watoto kingono katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa
kubadilishana na chakula. Ufaransa inasema kuwa inayafanyia uchunguzi madai
hayo.
“Siwezi kuelezea jinsi nilivyofazaishwa, kukasirishwa na
kuaibishwa na taarifa za hivi karibuni kuhusu miaka ya dhulma za kingono
zilizofanywa na vikosi vya UN… inatosha,” alisema Ban.
Jamhuri ya Afrika ya Kati iliingia katika machafuko
tangu Desemba 2013 baada ya makundi ya Kikristo yenye silaha kuanzisha
mashambulizi dhidi ya kundi la Seleka lenye Waislamu wengi ambalo liliiangusha
serikali mwezi Machi mwaka huo.
Tangu Januari 2014, nchi hiyo imekuwa ikiongozwa na
serikali ya mpito. Uchaguzi wa Urais na Ubunge umepangwa kufanyika Oktoba 18.


0 comments:
Post a Comment