![]() |
| Imam Youssoupha Sarr |
Kiongozi mmoja wa Kiislamu nchini Senegal ametoa wito wa
kufanyika ‘Jihad ya Kijani’ dhidi ya uchafuzi wa hali ya hewa, akilitaka bunge
la nchi hiyo na jamii nzima ya Kiislamu kujiingiza katika kile anachokiita kama
jukumu la wazi la Kiislamu la kulinda mazingira.
Akiashiria misingi ya Uislamu kuhusu mazingira, Imam
Youssoupha Sarr, amesema katika mahojiano na kituo cha al-Jazeera kuwa hawezi
kuamini kwamba watu katika taifa lake la Kiislamu wamezoea kuishi katika
mazingira yaliyochafuliwa na mifuko ya plastiki na aina nyingine za uchafu.
“Uislamu uko wazi [kuhusu suala la mazingira],” Sarr alisema na
kuongeza, “Aina yoyote ya uchafuzi au
uharibifu wa mazingira ni dhambi na umeharamishwa moja kwa moja. Watu wanatakiwa
kukumbushwa kuhusu jambo hili.”
Kiongozi huyo amesema kuwa anaamini kuwa Mwenyezi Mungu amewajaalia
wanadamu mazingira maridhawa, na hivyo ni wajibu kwa jamii ya wanadamu
kuyalinda kwa gharama yoyote.
![]() |
| Ufukwe nchini Senegal uliochafuliwa kwa chupa za plastiki na uchafu mwingine. |
Wito wa Sarr wa kutaka zichukuliwe hatua za dhati dhidi
ya uchafuzi umeripotiwa kuliamsha bunge la nchi hiyo. Hivi karibuni nchi hiyo
ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchi nzima.
Sambamba na marufuku hiyo, wale wanaopatikana na hatia
ya kuchafua barabara au mazingira kwa kutupa mifuko ya plastiki wanaweza kupewa
adhabu ya kifungo cha miezi sita na kulipa faini kubwa.
Hata hivyo, wananchi wameendelea kutumia mifuko hiyo na
wamelikosoa bunge kwa kupiga marufuku matumizi hayo bila kuwapatia njia
mbadala.
Hayo yanatokea katika kipindi ambacho taifa hilo limekuwa
likipambana kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa miaka mingi, na mbali na athari
ya mabadiliko ya tabianchi, taifa hilo linaathiriwa na uchafuzi wa mazingira
unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.
Viwanda vikubwa vya nchi hiyo kama vile viwanda vya
usindikaji wa samaki, viwanda vya nguo, rangi na usindikaji wa chakula hutupa
taka zake baharini au katika maeneo ya wazi.
Aidha, ardhi yenye rutuba katika nchi hiyo imeanza kuwa
hatarini. Kutokana na shughuli za kilimo zisizofaa, nchi hiyo inakabiliwa na
hatari ya kupoteza ardhi yake ya kijani.


0 comments:
Post a Comment