
Wakati kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu msimamo
halisi wa kisiasa wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk. Willibroad Slaa, mwenyewe ameibuka na kusema ataweka kila kitu
hadharani muda wowote kuanzia sasa.
Katika siku za karibuni, Dk. Slaa amekuwa gumzo kutokana
na kutoonekana katika shughuli mbalimbali za chama hicho pamoja na mikutano
muhimu inayoitishwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Dk. Slaa
alisema kuna mambo mengi yanayozungumzwa juu yake ambayo hayana ukweli wowote
na kwamba hivi karibuni atazungumza na kuweka hadharani kila kitu.
Hata hivyo, Dk. Slaa hakusema ni mambo gani yasiyo ya kweli
yanayozungumzwa juu yake na wala hakuwa tayari kuweka wazi siku atakayoweka
hadharani yale aliyoyahifadhi moyoni mwake.
Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa atashiriki uzinduzi wa
kampeni za uchaguzi mkuu ujao, Dk. Slaa alisema hakuna ukweli wowote kuhusiana
na jambo hilo na zaidi, akasisitiza kuwa pawe na subira kwani mambo yote
yatajulikana siku atakapozungumza.
“Hakuna ukweli baba... sijui kwa nini watu wanapenda
kutoa kauli za namna hiyo. Ukweli utajulikana tu ndani ya muda mfupi,” alisema
Dk. Slaa kupitia ujumbe mfupi alioutuma kwa namba ya simu yake ya kiganjani
jana.
Awali, Dk. Slaa alipigiwa simu na Nipashe simu yake ya
mkononi ikawa inaita muda mrefu bila kupokelewa, lakini baadaye alipotumiwa
maswali kupitia ujumbe mfupi wa maneno alijibu haraka na kukanusha taarifa
zilizodai kuwa atashiriki uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu zitakazoanza
Agosti 22.
Swali jingine aliloulizwa ni sababu za yeye kuwa kimya
na haonekani katika shughuli za kisiasa za chama chake na Ukawa unaoundwa pia
na washirika wa Chadema; Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John
Mnyika, alikaririwa akisema kuwa amewasiliana na Dk. Slaa na kwamba (Dk. Slaa)
amekubali kushiriki uzinduzi wa kampeni za Ukawa kwenye jimbo la Kibamba.
Mnyika aliwaambia wanachama wa Chadema wa matawi ya kata
ya Goba muda mfupi kabla ya kufanyika kura za maoni kumchagua mgombea wao wa
udiwani katika eneo hilo.
"Dk. Slaa yupo mapumzikoni na nilizungumza naye kwa
kirefu na aliniambia bado anapumzika, lakini atakuja kushiriki kampeni za chama
Jimbo la Kibamba ambalo mimi nagombea ubunge," alisema Mnyika.
KIKAO KIZITO
Kauli ya Dk. Slaa inakuja huku kukiwa na juhudi kadhaa
za kumshawishi mwanasiasa huyo kujiunga na Ukawa kabla ya kuanza kwa kampeni
mwezi huu.
Mathalan, chanzo kimoja kimeiambia Nipashe kuwa Jumanne
wiki hii, Dk. Slaa alifanya mkutano wa faragha na Mbunge wa Kigoma Kusini,
David Kafulila, kwa takriban saa tano.
Inaelezwa kuwa Kafulila alikuwa akijaribu kumshawishi
Dk. Slaa kubadili msimamo wake ili Ukawa waweze kufanya kampeni wakiwa na
umoja.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Dk. Slaa anadai Mwenyekiti
wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, aliwaburuza wenzake katika hatua za mwisho za
kumkubali Lowassa kuhamia chama hicho na hatimaye kuwa mgombea wa urais.
Dk. Slaa pia anahisi kupuuzwa na wenzake hasa kwa
kuzingatia mchango wake wa kukijenga chama hicho tangu mwaka 2010 alipogombea
urais.
Alipoulizwa na Nipashe kuhusiana na taarifa kuwa
alikutana na Dk. Slaa, Kafulila alikiri kufanya hivyo lakini akakataa
kuzungumza kiundani juu ya kile kilichojiri kwa maelezo kuwa ni masuala ya
faragha.
"Tuliongea kweli, ni mambo mazito lakini siyo ya
kuweka hadharani maana ulikuwa mkutano wa faragha," alisema Kafulila.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na hofu iliyotanda ndani ya
Chadema na wananchi kwa ujumla kutokana na kutoonekana kwa Dk. Slaa katika
matukio mawili makubwa ya kisiasa yanayohusu mustakabali wa chama hicho.
Dk. Slaa hakuonekana siku Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, alipotangaza kujivua uanachama
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga Chadema.
Kadhalika, Dk. Slaa hakuonekana wakati Lowassa alipofika
kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho akitarajiwa kuwakilisha
Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Pia hakuonekana katika mkutano mkuu wa Chadema wa
kumchagua mgombea urais na mgombea mwenza na pia katika maandamano ya
kumsindikiza Lowassa yaliyovutia maelfu ya wananchi Jumatatu wakati akienda
kuchukua fomu za kuwania urais kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment