Tangu juzi kumekuwapo na tetesi kuwa vyama vinavyounda
umoja wa katiba ya wananchi UKAWA, huenda umoja huu ukasambaratika kwa kile
kinachoelezwa kutokukubaliana kwa mgawanyo sawa wa majimbo kuelekea uchaguzi
mkuu Oktoba.
Imeripotiwa pia leo vijana wa chama cha wananchi CUF na
NCCR mageuzi, wanatarajia kuandamana ili kushinikiza viongozi wa juu wa vyama
vyao kuachana na UKAWA kwa kile wanachokiita kupunjwa usawa wa uwakilishi
katika majimbo na CHADEMA.
Aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa CUF Tanzania bara, Julius
Mtatiro amekuwa akitoa mtazamo wake mara kwa mara kuhusu kadhia na migogoro hii
ya UKAWA, akisisitiza kutokukubaliana na kuvunjika kwao.
Kwenye ukurasa wake wa Facebook ameandika yafuatayo:
“SHEREHE ZA KUVUNJA UKAWA??? Ndugu zangu, Tangu jana
nimeona MATAMKO ya watu mbalimbali wakijinasibu kwamba ni bora UKAWA ivunjike,
wengine wanasema vyama vyao vinamezwa, wengine wanasema hawakubali hili na lile
n.k. bahati mbaya haya yasemwayo ni mambo ambayo viongozi wa juu wa UKAWA ndiyo
wanapaswa kuyashughulikia, si viongozi wa kawaida wa vyama au wanachama.
Mimi nataka tena kurudia kusema hapa, kwamba UKAWA
ikivunjika kwa sababu yoyote ile, ni KITENDO CHA VYAMA VYA UPINZANI KUWASALITI
WANANCHI. Hakuna lugha nyingine.
Na wale wanaofurahia UKAWA ikitetereka na wanaoombea
ivunjike waendelee kuomba maombi hayo yasiyo na tija kwa taifa. UKAWA
ikishavunjika vyama vya upinzani havitabaki salama hata kidogo.
Athari ambazo chama kimojakimoja kinazipata ndani ya
UKAWA ni chache kuliko chama kimojakimoja kikienda kivyake. UKAWA ilikuwa na
malengo makubwa sana, achilia mbali uchaguzi, kuna ajenda ya katiba.
Tuliondoka kwenye bunge la katiba na kuacha milioni 30
kila mjumbe kwa sababu ya kujenga mshikamano wa upinzani. Kuvunja UKAWA leo ni
kusema pia TUNAIKUBALI KATIBA inayopendekezwa. Tukivunja UKAWA leo tunapigwa
kwenye uchaguzi mkuu huu uu lakini zaidi ya yote wananchi
watatupiga mawe tutakapojipeleka kuwaambia waikatae Katiba inayopendekezwa
kwani tutakuwa hatuaminiki kwa mambo madogo na hatuwezi kuaminika kwa mambo
makubwa.
Mimi naamini katika USHIRIKIANO WA VYAMA VYA
KIMABADILIKO ili kulikomboa taifa, siamini kinyume chake hata kidogo. Kwa
sababu viongozi waliahidi leo ndipo wataamua mustakabali wa kila kitu, kila
mpenda mabadiliko anasubiri kwa hamu kujua viongozi wanaongoza tupite njia ipi.
Mungu awabariki nyote,” ameandika Mtatiro.
Tafadhali tuachie maoni yako hapo chini, na endelea
kukaa karibu na mzizima24.com
CHANZO: TIMES FM
0 comments:
Post a Comment