
Rais wa Marekani Barack Obama amesema kuwa atatetea
msimamo wake juu ya haki za mashoga kufuatia upinzani wa suala hilo unaoendelea
nchini Kenya.
Akizungumza na shirika la habari la BBC, Rais Obama
amesema kuwa atazungumza bila kificho dhidi ya ufisadi na ukiukwaji wa haki za
binadamu wakati wa ziara yake nchini humo.
“Mimi si shabiki wa ubaguzi na uonevu kwa yeyote kwa
msingi wa rangi, dini au jinsia,” alisema.
Obama amekosolewa vikali nchini Kenya kufuatia hatua
yake ya kuunga mkono haki za mashoga huku viongozi wengi wa Kenya wakimuonya
dhidi ya kuibua suala hilo wakati wa ziara yake.
Viongozi hao, wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto, wamezungumzia
msmamo wa wazi wa nchi hiyo kupinga ndoa za jinsia moja na kwamba watapinga
sheria yoyote itakayolenga kuhalalisha ndoa za mashoga.
Akizungumza katika kanisi la AIC mjini Nairobi Bwana
Ruto alionya kwamba sheria yoyote itakayolenga kuruhusu ushoga nchini humo
itapingwa vikali na kuzuiliwa.
“Ushoga ni kinyume na mpango wa Mwenyezi Mungu na
haupaswi kuvumiliwa. Mungu hakuumba mwanaume na mwanamke ili wanaume wawaoe
wanaume na wanawake wawaoe wanawake wenzao.”
Wakati wa ziara yake nchi Senegal mwaka 2013, Obama alizitolea
wito serikali za Afrika kutoa haki sawa kwa mashoga kwa kuacha kutunga sheria
zinazowabagua.
Mpaka sasa Afrika Kusini ndio nchi pekee ya Kiafrika
iliyohalalisha ushoga.
Obama anatarajiwa kuizuru Kenya kuhudhuria Mkutano wa
Kilele wa Ujasiriamali Duniani (GES) unaotarajiwa kuanza leo Julai 24 mpaka 26
jini Nairobi, na anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu
uhusiano wa nchi hizo mbili.
Obama atakuwa rais wa kwanza wa Marekani aliye
madarakani kuhutubia mkutano wa Umoja wa Afrika atakaposafiri kwenda Ethiopia
siku ya Jumapili.
0 comments:
Post a Comment