![]() |
| Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa. |
Wakati mchakato wa kuwatafuta wagombea watakaosimama
kupeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ngazi ya
ubunge ukiendelea katika sehemu mbalimbali nchini, zimejitokeza dosari huku
maeneo mengine mikutano ikivunjika.
MTWARA
Wanachama wa Chadema wilaya ya Mtwara wameshindwa kupata
wagombea ubunge katika jimbo la Mtwara Mjini na wa Viti Maalum kutokana na
kuvurugika kwa mkutano kufuatia mkanganyiko juu ya idadi ya kata zilizofanya
uchaguzi na kuwa na uhalali wa kupiga kura za kuchagua wagombea.
Wagombea waliokuwa wanachuana ni Joel Nanauka, Mohamed
Hassan Hanga, Ibrahim Mandoa na Dastani Mulokozi ambaye hakuwapo mkutanoni na
kuwakilishwa na mke wake.
Hatua hiyo ilitokana na hoja iliyotolewa na mjumbe wa
mkutano huo ambaye ni mwenyekiti wa mawasiliano, takwimu na Biometric Voters
Registration (BVR), Karim Salum Ally, ambaye alihoji utofauti wa idadi ya kata
hizo kwamba taarifa alizokuwanazo yeye ni kata 15 huku zile za katibu wa
Chadema mkoa, Willy Mkapa zilisema ni kata 17.
BARIADI
Katika jimbo la Bariadi, zilitokea dosari baada ya
mkutano wa kumpata mgombea wa nafasi hiyo kuvunjika.
Mkutano huo ulivunjika saa 9:30 alasiri, baada ya
viongozi wa chama hicho wilaya na wasimamizi kubaini kuwapo kwa vitendo vya
rushwa kwa wagombea kubainika kugawa fedha kwa baadhi ya wajumbe ili wawapigie
kura.
Kabla ya kuvunjika kwa mkutano huo saa 6:00 mchana,
baadhi ya wapambe wa wagombea wakiwa wanagawa pesa hadharani kwa wajumbe,
vijana wa ulinzi wa chama hicho (red briged), waliwakamata wanawake wawili na
kijana mmoja wa wapambe hao.
Hata hivyo, baada ya kiongozi wa vijana wa ulinzi wa
Chadema wa kanda ya Serengeti, Esau Bwire, alisema watu hao walibainika
wakigawa Sh. 20,000 kwa kila mjumbe.
Msimamizi wa uchaguzi huo wa kanda ya Serengeti,
Emmanuel Mbise, alithibitisha kuwapo kwa vitendo vya rushwa kwa wagombea kadhaa
na kukichafua chama wakati kikipiga vita vitendo hivyo.
Licha ya kuwapo wagombea 12 wa nafasi ya ubunge katika
jimbo hilo, lakini alishindwa kupatikana mmoja kati yao kutokana na kuvunjika
kwa mkutano huo.
SHINYANGA
Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo la Shinyanga Mjini,
Alex Malima, alimtangaza mwenyekiti wa taifa vijana Chadema (Bavicha), Patrobas
Katambi, kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Aidha, Malima alimtangaza mbunge wa viti maalumu
aliyemaliza muda wake, Rachel Mashishanga, kutetea tena kiti hicho kupitia
Chadema.
Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa Mashariki, Silvester
Kasulumbai, alisema chama hicho kinachopendwa na wananchi kinatakiwa kupata
watu makini watakaoweza kupeperusha
bendera ya chama katika uchaguzi ujao wa Oktoba mwaka huu.
BUSEGA
Dk. David Nicas, mgombea wa nafasi ya ubunge katika
jimbo la Busega kwa tiketi ya Chadema, alifanikiwa kupata kura 116 dhidi ya
washindani wake wa karibu 11 ambao ni Mabelele Buluba kura 67 na Revocatus
Madundo (55).
ILEMELA
Mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo la Ilemela,
Highness Kiwia, aliibuka mshindi kwa kupata kura 134 kati ya kura 294
zilizopigwa kwa wagombea wenzake 18.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment