
- Aeleze nilitoa lini, wapi, kwa nani
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema
amechoshwa na tuhuma za kipuuzi za kumhusisha na rushwa na sasa amewataka wote
wenye ushahidi wa tuhuma hizo dhidi yake wazitoe.
Akizungumza na mamia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), mjini hapa jana alipokuwa akirejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama
hicho ili awanie urais kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, Lowassa alisema
kwa muda mrefu kuna watu ambao wamekuwa wakimtuhumu kwa rushwa tuhuma ambazo
alisema siyo za kweli.
“Ninatoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma
hizo za kipuuzi autoe. Aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme
nimechukua rushwa lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani,” alisema.
Aliongeza kuwa yeye ni muadilifu, na anaposema kuwa
atasimamia vita dhidi ya rushwa atafanya hivyo kwa vitendo bila kumuonea mtu
wala kumuonea haya yeyote.
“Ndugu wanachama wenzangu, na wananchi kwa ujumla, ni
lazima sasa tufike mahali tuseme imetosha. Majungu yametosha, upotoshwaji
umetosha, rushwa imetosha, na kwa pamoja tunaweza kukomesha haya. Tutayakomesha
kwa kusimamia ukweli, uadilifu, uaminifu na kutenda kwa haki,” alisema Lowassa
katika hotuba iliyovuta hisia kwa waliokuwa wanamsikiliza.
Alisema tuhuma hizo zimeendelea hata wakati wa kutafuta
wadhamini kwa baadhi ya watu kuzieneza.
“Tumefanya kazi ya kutafuta na kuomba udhamini kwa
uadilifu na umakini mkubwa. Na hapa nitumie nafasi hii pia kuwashukuru makatibu
na viongozi wote wa Chama katika mikoa na wilaya kwa maandalizi mazuri katika
kuifanikisha zoezi hili,” alisisitiza.
Alisema kuwa walifanya kazi yao vizuri kinyume kabisa
cha vijimaneno vilivyoenezwa kwamba kulikuwa na matumizi ya fedha katika
kuwatafuta wadhamni.
“Hivi kweli, unahongaje watu zaidi ya laki nane?”
alihoji.
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, alisema tuhuma
hizo zimekuwa zikitolewa na watu ambao wamekosa hoja na zinatolewa bila
ushahidi wowote.
Aliwataka wote ambao wamekuwa wakimtuhumu kwa miaka
kadhaa sasa na kumhusisha na suala zima la rushwa, waache mara moja kwani
hakuna hata chembe ya ukweli wa maneno hayo.
Alisema akifanikiwa kushika wadhifa wa urais, ataendesha
nchi kwa kufuata katiba na sheria.
Kuhusu safari ya kusaka wadhamini, Lowassa aliwashukuru
wana-CCM waliomdhamini na kwamba walijitokeza kwa wingi jambo ambalo limempa
picha ya kuungwa mkono na kukubalika.
Alisema wanachama waliojitokeza kumdhamini walifanya
hivyo kwa utashi wao na bila kishawishi chochote cha fedha au fadhila nyingine
yoyote.
Alisema kuwa udhamini alioupata ni kielelezo cha vitendo
kwamba wapo naye katika Safari ya Matumaini.
“Nina matumaini na imani kubwa kwamba mtaendelea kuniunga
mkono ndani ya Chamna chetu ili kwa pamoja na mshikamano ndani ya Chama niweze
kuteuliwa kugombea kiti cha urais,” alisema.
Lowassa alisema: “Kwa mafanikio haya ya hatua ya awali
nina imani kwamba ni ishara njema kueleke hatua zilizobakia na uweza wake
Mwenyezi Mungu Mungu, na kwa ushirikiano wenu kwa pamoja tutalivuka daraja ili
hatimaye niwatumikie kwa utumishi uliotukuka nikiwa Rais wa Awamu ya Tano.”
Aliongeza kuwa: “Nina shauku kubwa ya kuunganisha nguvu
na uwezo ya kila Mtanzania katika kupambana na umasikini wa nchi hii. Umasikini
wa watu wetu siyo amri ya Mwenyenzi Mungu. Nina imani kabisa kwa pamoja
tunaweza kutumia rasilimali tulizo nazo kwa bidii, maarifa na ufanisi zaidi ili
kutokomeza umasikini huu.”
Mbali na Lowassa jana makada wengine watano wa CCM
walirejesha fomu ambao ni Luaga Mpina, Dk.Hamis Kingwangala, Mwigulu Nchemba,
Dk. Hassy Kitine na Eldoforce Bilohe, hivyo kufanya waliorusisha fomu kufikia
33 kati ya 42 anasaka wadhamini ili wapate ridhaa ya Chama hicho kuwania urais
kwenye uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge Oktoba 25, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment