
HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, imesusa
kuwapokea wagonjwa wa Mabusha, wanaohitaji kufanyiwa upasuaji kupitia Mradi
Maalumu wa Serikali, hivyo kuwalazimu baadhi ya wagonjwa hao kufuata huduma
hiyo nchini Msumbiji.
Taarifa za uhakika zilizopatikana hospitalini hapo kabla
ya kuthibitishwa na baadhi ya wananchi ama wanaosumbuliwa na ugonjwa huo au
jamaa wa wagonjwa hao kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo wa kusini mwa
Tanzania unaopatikana na Msumbiji, zinasema uongozi wa hospitali hiyo uligoma
kuwapokea wagonjwa wa aina hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kutokana na hali hiyo,
baadhi ya wagonjwa wa aina hiyo mkoani humo, ambao walilengwa kuwa wanufaika wa
mradi maalumu wa kupambana na magonjwa ya mabusha na matende nchini,
walilazimika kukimbilia Msumbiji ili kupata huduma hiyo, ambayo kama Tanzania
nchi hiyo nayo ilikuwa na mradi huo kwa udhamini wa Shirika la Afya Duniani
(WHO).
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula,
Mkoa wa Mtawara, Dk. Mohamed Gwao, alipoulizwa kuhusiana na madai hayo ya
kuwakataa wagonjwa wa aina hiyo kupitia mradi huo maalumu wa Serikali, alikataa
kuingia kwa undani kuzungumzia suala hilo, akisema hana taarifa yoyote
inayohusu wagonjwa wa mabusha kunyimwa matibabu hospitalini kwake hapo.
Hata hivyo, Dk. Gwao amekiri kuwepo kwa mradi wa
kupambana na magonjwa ya mabusha na matende, akisema ulikuwa unasimamiwa moja
kwa moja na Maofisa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Dindwa, kilichoko Kata ya
Kitaya, Wilaya ya Mtwara Vijijini, miongoni mwao wakiwemo waliojitambulisha kwa
majina ya Twahiru Godson na Issa Sadiki, wamethibitisha kuwepo kwa wananchi
wengi wa mkoa huo waliokuwa wakikabiliwa na ugonjwa huo waliokosa huduma hiyo,
ambayo tiba yake inahusisha upasuaji.
Katika jitihada za kudhihiti ugonjwa wa mabusha, maarufu
kwa jina la Ngiri Maji pamoja na matende, ugonjwa ambao unaelezwa kuenea zaidi
katika mikoa ya mwambao wa Bahari ya Hindi, hasa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani,
Tanga, Lindi na Mtwara, Serikali, kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
ilizindua kampeni maalumu, takriban miaka minne iliyopita, kwa ajili ya kutoa
huduma ya matibabu bure kwa wananchi wanaosumbuliwa na magonjwa hayo katika
maeneo hayo.
Takwimu kutoka serikalini zinaonyesha kwamba katika
kipindi cha miaka minane iliyopita, wananchi wanaofikia milioni 10, walipatiwa
kinga ya magonjwa hayo nchi nzima.
Habari kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja
na Taassisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) zinaeleza kwamba mpango
huo wa kutoa kinga ya kuzuia maambukizi pamoja na kutoa huduma kwa waathirika
wa magonjwa ya Ngiri maji na Matende, bado unaendelea unaendelea nchini kote,
ukilenga kuhakikisha kuwa maradhi yote hayo yanateketezwa nchini hadi kufikia
mwaka 2020.
CHANZO: Mtandao wa Fikra Pevu
0 comments:
Post a Comment