KIONGOZI WA UPINZANI BURUNDI ATAKA SERIKALI YA MSETO

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza

Kiongozi mwandamizi wa kambi ya upinzani nchini Burundi amemtolea wito Rais Pierre Nkurunziza kufanya mazungumzo na wapinzani wake na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi wa wiki hii, akisema kuwa hatua hiyo inaweza kuepusha kutokea kwa vita mpya vya wenyewe kwa wenyewe.

Agathon Rwasa, kiongozi wa zamani wa waasi, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kuna udharura wa kuwazuia majenerali waliokuwa nyuma ya mpango wa mapinduzi yaliyofeli mwezi Mei kufuatia mgogoro uliochochewa na hatua ya rais kutaka kugombea mhula wa tatu.

"Baadhi wameshatishia kuingia msituni na kuanzisha mapambano,” alisema.
"Ili kuiokoa Burundi, wazo la kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa linaweza kukubalika”, alisema na kuongeza kuwa sambamba na hilo anataka kufanyika kwa uchaguzi mpya ndani ya mwaka mmoja.

Akijibu wito huo wa upinzani, afisa mmoja wa Ikulu amesema Nkurunziza hatolikataa wazo la kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa iwapo ataibuka mshindi katika uchaguzi huo.

"Serikali ya umoja wa kitaifa si tatizo kwa Pierre Nkurunziza, tuko tayari kufanya hivyo,” Willy Nyamitwe, mshauri wa rais, amesema.

Lakini alipinga wazo la kukatisha mhula mpya wa miaka mitano na kusema kuwa hilo ni jambo “lisilowezekana”.

Taarifa kutoka mjini Bujumbura zimebainisha kuwa viongozi wa upinzani wamekuwa wakizungumzia uwezekano wa serikali ya umoja wa kitaifa hata kabla ya uchaguzi wa jana.

Hata hivyo, duru hizo zinasema kuwa mchakato huo unaweza kuchukua muda kwa sababu ya uhesabuji wa kura unaoendelea.

Ripoti zinasema kuwa waliojitokeza kupiga kura walikuwa zaidi ya silimia 70, na idadi ilikuwa kubwa zaidi katika maeneo ya vijijini ambapo Rais Nkurunziza ameendelea kuwa na nguvu.

KURA ZAENDELEA KUHESABIWA

Uhesabuji wa kura unaendelea na matokeo yanatarajiwa kutolewa kesho Alhamisi katika uchaguzi uliosusiwa na vyama vya upinzani na makundi ya kiraia kwa hofu ya uchaguzi huo kugubikwa na hujuma.

Marekani imesema kuwa uchaguzi huo hauwezi kuaminika kwa kuwa umegubikwa na hujuma za serikali dhidi ya upinzani na makundi ya kiraia, kufungwa vyombo vya habari na kuwatisha wapiga kura.

Karibu asilimia 74 ya wapiga kura milioni 3.8 waliojiandikisha wamepiga kura. Hayo yamesemwa na kamishina wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo, Claver Ndayicariye.
Rais Nkurunziza anatarajiwa kushinda mhula wa tatu.

Wapinzani wamepinga hatua ya rais Nkurunziza kugombea mhula wa tatu kwa madai kuwa ni kinyume na katiba na inakiuka makubaliano ya amani ya mwaka 2006 yaliyohitimisha vita nchini humo.

Hata hivyo, mahakama ya katiba ilitoa hukumu iliyomruhusu Rais huyo kugombea.

Zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha tangu chama tawala kilipotangaza mwezi Aprili kuwa Nkurunziza angegombea mhula wa tatu.

Vyombo huru vya habari vimefungwa na wapinzani kadhaa wameikimbia nchi wakiungana na wakimbizi zaidi ya 150,000 wanaohofu kuwa serikali yao inaweza kutumbukia tena katika ghasia za wenyewe kwa wenyewe.


CHANZO: Mzizima na mashirika ya habari
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment