
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, hivi karibuni
alipotangaza kuwa yeye na makamu wake wangechukua nusu tu ya mishahara yao,
halikuwa jambo lenye kustaajabisha kwa mtu anayejulikana kwa maisha ya kufunga
mkanda, na ambaye anakabiliwa na changamoto za kuimarisha uchumi wa nchi yake.
Lakini Rais Buhari sio kiongozi wa kwanza wa Afrika
kutangaza kukata mshahara wake. Kiukweli, hii imekuwa njia na mtindo kwa
viongozi wanaotaka kuinua umashuhuri wao au wanapokuwa wanakabiliwa na nyakati
ngumu za kiuchumi.
Mwaka jana nchini Kenya, Rais Uhuru Kenyatta na makamu
wake William Ruto walitangaza kujitolea kukatwa asilimia 20 ya mshahara wao na
kuwatolea wito viongozi wengine wa serikali kufanya hivyo. Wachache walifanya
kwa shingo upande.
Nchini Tunisia, Rais wa zamani Moncef Marzouki, akiwa
anakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi baada ya mapinduzi, alitangaza kukatwa
theluthi mbili ya mshahara wake kutoka dola 176,868 mpaka dola 58,956.
The Africa Review imekusanya na kuchambua taarifa za mishahara
ya viongozi wa Kiafrika na kuangalia uhusiano baina ya viongozi na raia wao.
Utafiti huo unaonesha kuwa nchi chache ndizo zinazoweka
wazi mishahara ya viongozi wao – jambo linaloonesha ukosefu wa uwazi.
Katika nchi nyingi za Kiafrika, kitu cha kwanza
kinachofanywa na viongozi wanapoingia madarakani ni kuongeza mishahara yao. Kwa
mfano, nchini Misri, mshahara wa rais ulipaa kutoka dola 280 kwa mwezi
zilizowekwa na utawala wa Mursi, mpaka dola 5,900 kwa mwezi pindi Jenerali
Abdel Fattah al-Sisi alipoingia madarakani.
Katika nchi nyingine, huchukua mishahara isiyoendana na
uwiano wa pato la taifa. Nchini Morocco, hazina hutumia dola milioni 1 kwa
ajili ya majumba 12 ya Mfalme Mohammed VI na makazi binafsi 30. Kadhalika hutumia
dola milioni 7.7 kwa ajili ya wasaidizi wa misafara ya kifalme, na mshahara wa
kila mwezi wa dola 40,000 unaolipwa kwa
mfalme.
Mwaka 2014, Mfalme Mswati wa Swaziland aliongeza bajeti
yake binafsi, inayojumuisha mshahara wake na huduma za familia yake, kwa
asilimia 10 mpaka kufikia dola milioni 61, ambayo ni fungu kubwa la bajeti
jumla ya ufalme huo. Kwa kuwa bajeti ya familia ya kifalme haijadiliwi au
kupitishwa na bunge, moja kwa moja imekuwa sheria.
Baadhi ya marais wanaonekana kuwa na mishahara midogo,
lakini wao wenyewe au kupitia familia zao, wana udhibiti mkubwa wa rasilimali
za nchi zao. Kwa mfano, Rais Eduardo dos Santos ana mshahara wa dola 5,000
lakini anaaminika kudhibiti utajiri mkubwa unaotokana na biashara ya mafuta ya Angola,
na familia yake inamiliki baadhi ya makampuni makubwa kabisa nchini humo.
The Africa Review haikuweza kupata taarifa za mshahara
rasmi wa Rais wa muda mrefu wa nchini ya Equatorial Guinea yenye utajiri wa
mafuta bwana Teodoro Obiang’ Nguema
Mbasogo.
Kwa utajiri mkubwa wa mafuta na idadi ya wananchi chini
ya milioni moja, Equatorial Guinea ina kiwango cha juu kabisa cha pato la kila
mtu na ilipaswa kuwa taifa la ulimwengu wa kwanza. Badala yake, utajiri wake
mkubwa unaishia mikononi mwa familia ya Rais.
CHANZO: http://www.thecitizen.co.tz/News/What-African-presidents-are-paid-and-why-it-matters-a-lot/-/1840340/2803820/-/1sc2i7/-/index.html
(TUPE MAONI YAKO)
(TUPE MAONI YAKO)
0 comments:
Post a Comment