Habari kwamba Iran na madola makubwa 6 wamefikia muafaka
wiki iliyopita ni suala ambalo linaonekana kuwa ni mapatano ya kihistoria, sio
tu kwa uhusiano wa Marekani na Iran, bali pia kwa eneo zima la Mashariki ya
Kati. Ingawa muafaka wa mwisho haujasainiwa na bado kuna mambo ya kiufundi
ambayo nchi hizi zinatakiwa kuyajadili, taathira ya mapatano hayo kwenye
mustakbali wa Mashariki ya Kati imeanza kujadiliwa na kuzungumzwa. Mapatano hayo
yanaweza kubadilisha, kwa kiasi kikubwa, baadhi ya mizania muhimu sana katika
ukanda huo, na yanaweza kuleta ulinganifu kwenye mahusiano baina ya Marekani na
nchi hizi na pia kusababisha utata na mkanganyiko wa kiuhusiano miongoni mwa
mataifa ya Mashariki ya Kati.
Kwa kiasi kikubwa mapatano haya yataathiri pakubwa
uhusiano wa Marekani na Israel. Tangu mwanzoni mwa mashauriano ya kufikia
muafaka imara, Israel imekuwa mkosoaji mkali na mpinzani mkubwa dhidi ya mapatano
baina ya Marekani na Iran ambayo yataipa Iran uwezo na miundombinu ya kuwa na
nishati ya nyuklia. Netanyahu alijaribu kuishawishi moja kwa moja jamii ya
Marekani kabla ya uchaguzi wa Urais mwaka ili kuliibua suala la miundombinu ya
nyuklia ya Iran. Baadaye, kwa mara nyingine, Netanyahu alipinga mapatano yoyote
baina ya Marekani na Iran, na akaendelea kuonya kuwa mapatano na muafaka kama
huo utahatarisha uhai wa Israel. Mapatano ya awali yalipofikiwa mwezi Nevemba
2013, serikali ya Israel iliyapinga. Netanyahu aliyaita mapatano hayo kuwa ni “kosa
la kihistoria.” Wakati mazungumzo yakiendelea baina ya mataifa hayo 6, Netanyahu
alipoteza matumaini ya kuwa na tashwishi ya moja kwa moja na kuanza kufanya
juhudi za kuweka tashwishi kwenye uamuzi wa utawala wa Obama kupitia bunge la Congress
ya Marekani. Hotuba yake kwenye bunge hilo la Congress, ambayo iliibua mpasuko
mkubwa kati ya Ikulu ya White House na serikali ya Israel, lilikuwa jaribio la
mwisho la kutaka kusimamishwa mazungumzo hayo kabla ya muafaka wa mwisho
kufikiwa. Hata hivyo, utawala wa Obama ulighadhibishwa na hatua ya kiongozi wa
kigeni kuingilia masuala ya sera ya nje ya Marekani. Wakati Netanyahu akiwa
Washington hakukutana na kiongozi yeyote wa utawala wa Obama. Katika kujibu
hotuba ile, Obama alisema kuwa Netanyahu hakuzungumza kitu kipya, hii ikiwa ni
moja ya nyakati mbaya kabisa za mvutano mkubwa baina ya Israel na Marekani. Kuhusu
hatua ya Netanyahu, Obama alisema: “Kumbuka tulipotengeneza mapatano ya muda,
Waziri Mkuu Netanyahu alitoa hotuba kama hiyo akizungumzia namna mapatano hayo
yatakavyokuwa hatari. Lakini, mwaka mmoja baadaye, hata maafisa wa upelelezi wa
Israel, na baadhi ya viongozi wa serikali ya Israel, walikiri kuwa hakika mapatano
yale yaliizuia Iran isiendelee na programu yake ya nyuklia… na mbadala anaoutoa
waziri mkuu sio suluhisho, jambo ambalo litaifanya Iran ianze mara moja
kuendeleza programu yake ya nyuklia, kuharakisha programu yake, bila sisi kujua
wanachokifanya na bila kuhusishwa. Na hoja yake ya msingi ni kwamba kama
tutaongeza vikwazo mara dufu, Iran haitataka kufanya hivyo”.
Mazungumzo yaliendelea, na mapatano yakafikiwa wiki
iliyopita kati ya Iran na madola hayo makubwa. Moja kwa moja serikali ya
Israeli ilijibu na kufanya kikao cha dharura kuhusu muafaka huo. Kwa mara
nyingine Netanyahu alitoa hoja kwamba mapatano hayo ni hatari kubwa kwa ukanda
wote wa Mashariki ya Kati. Baada ya muafaka huo, Obama na Netanyahu walifanya
mazungumzo kwa njia ya simu ambapo Netanyahu alirudia kuelezea wasiwasi wake
kuhusu athari ya mapatano hayo kwenye usalama wa Israel. Kwa mujibu wa ripoti, Netanyahu
alisema: "Mapatano haya yatahalalisha programu ya nyuklia ya Iran,
yataimarisha uchumi na kuupa nguvu ushawishi na vitisho vya Iran katika
Mashariki ya Kati na kwengineko… mapatano kama hayo hayataizuia Iran kuwa na
bomu la nyuklia. Kinyume chake, yataifanya iwe nalo.” Siku moja baada ya
muafaka huo, Netanyahu pia alisema kuwa wakati wa kutia saini muafaka huo basi
Iran inatakiwa itambue haki ya uwepo wa Israel. Hata hivyo, kabla ya mazungumzo
ya simu, Obama alisisitiza kuwa iwapo Netanyahu anatafuta njia ya kuizuia Iran
kupata silaha za nyuklia, basi njia hiyo ni huu mkataba. Vilevile Obama alisema
kuwa amelipa maelekezo jopo lake la usalama wa taifa kuanzisha mashauriano na
serikali mpya ya Israel kuhusu uimarishaji wa ushirikiano wa kiusalama baina ya
serikali hizo mbili. Pande zote mbili zinaweza kupata ufumbuzi wa ushirikiano
wa kijeshi, lakini wasiwasi wa Israel kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa Iran
katika nchi kama vile Iraq na Syria hautakwisha kwa kuongeza ushirikiano na
Marekani.
Hivyo basi, baada ya mkataba huu uhusiano wa pande hizi
mbili utakuwa katika sura gani? Radiamali iliyooneshwa na Israel baada ya mapatano
haya inaonesha kuwa makabiliano hayajafikia kikomo. Kutokana na kukosekana hali
ya kuaminiana kati ya Obama na Netanyahu na wabunge wengi wa Republican katika Congress
ya Marekani, Netanyahu anaweza kuendelea kutia ushawishi wa kufanyika
mabadiliko kadhaa kwenye mapatano ya mwisho, ikiwa ni pamoja na kuwepo sharti
kwamba Congress itakuwa na jukumu la kuyachunguza masharti ya mapatano hayo. Jaribio
hili litasababisha mvutano zaidi baina ya White House na serikali ya Israel
katika miezi ijayo, hususan wakati wa kuzungumzia masuala ya kiufundi katika
mkataba huo. Aidha, katika mapatano ya mwisho baina ya Iran na mataifa 6,
kutakuwa na mazungumzo mengi kuhusu uhusiano baina ya Marekani na Israel.
Hata hivyo, hilo halitasababisha anguko la moja kwa moja
la uhusiano wa Marekani na Israel. Ni hakika uhusiano kati ya pande hizo mbili
katika ushirikiano wa kijeshi na kiusalama utaendelea.
Kadhalika, kutokana na wasiwasi wa Israel, ushirikiano
huo wa kijeshi unaweza kuwa imara zaidi. Hata hivyo, sambamba na tatizo la
kuaminiana, usawazishaji na uboreshaji wa wa uhusiano kati ya Marekani na Iran
ni jambo linaloweza kuibua baadhi ya changamoto kwenye uhusiano wa Marekani na
Israel.
Ingawa hatujui kiwango cha ushirikiano kati ya Marekani
na Israel kuhusu masuala ya kiintelejensia, pande hizo mbili zimekuwa na
ushirikiano katika kuishughulikia Iran. Katika matukio yote, Iran au maslahi
yake katika ukanda wa Mashariki ya Kati yamekuwa yakilengwa na ushirikiano wa
pamoja baina ya intelejensia ya Marekani na Israel. Kwa mfano, Operesheni
inayojulikana kama Operesheni ya ‘Olympic Games’, ambayo ni shambulizi la
kiteknolojia dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran miaka kadhaa iliyopita,
lilitokana na ushirikiano wa kiintelejensia baina ya pande hizo mbili. Ingawa ripoti
zinaonesha kuwa pande mashirika ya upelelezi ya pande hizo mbili yalikuwa na
tofauti za kimaoni katika utekelezaji wa operesheni hiyo, ilionesha uwazo wa
kufanya operesheni za pamoja baina ya CIA na Mossad. Kadhalika, hivi karibuni
gazeti la Washington Post, lilifichua kuwa operesheni ya kumuua Imad Mughniyah –
kiongozi wa kijeshi wa kundi la Hizbullah – ilifanyika kwa ushirikiano baina ya
CIA na Mossad.
Iwapo uhusiano wa baina ya Marekani na Iran
utasawazishwa, ushirikiano wa kiintelejensia baina ya Marekani na Israel
unaweza kuathiriwa. Katika mazingira kama haya, hata kiwango cha ushirikiano
huo kinaweza kuathiriwa na kuongezeka kwa usawazishaji wa uhusiano baina ya
Marekani na Iran.
0 comments:
Post a Comment