Waofisa wa Liberia wanawasihi manesi na madaktari
wasitishe mpango wao wa kufanya mgomo nchi nzima katika kipindi hiki ambacho
mlipuko wa maradhi hatari ya Ebola unaendelea kulitikisa eneo la Afrika
Magharibi.
Chama cha Madaktari nchini humo kinataka nyongeza ya
fedha ya mazingira hatarishi wanayolipwa wale wanaowatibu wagonjwa wa Ebola.
Naibu waziri wa afya nchini Liberia, Tolbert Nyenswah,
amesema kuwa mgomo huo utakuwa na athari mbaya kwa wagonjwa na utaathiri
maendeleo yaliyokwishapatikana katika mapambano dhidi ya maradhi hayo.
Serikali inasema kuwa ukubwa wa mlipuko wa maradhi hayo
unaifanya ishindwe kulipa kiasi cha fedha walichokubaliana awali.
Kwa sasa fedha ya mazingira hatarishi ni chini ya dola 500
kwa mwezi, nje ya mshahara wa kawaida ambao ni kati ya dola 200-300. Madaktari wanataka
fedha hiyo iongezwe mpaka kufikia dola 700 kwa mwezi.

Madaktari hao pia wanataka vifaa vya kujikinga dhidi ya
maambukizi na wapewe bima.
Asilimia tisini na tano ya wenzao wameshapoteza maisha
kutokana na Ebola. Liberia ni miongoni mwa nchi zilizoathirika vibaya sana na
maradhi hayo.
Mpaka sasa zaidi ya watu 4,000 wameshapoteza maisha
katika mlipuko huo.
Kituo kipya cha Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuratibu
mapambano dhidi ya maradhi hayo kimewekwa nchini Ghana.
Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamepelekwa nchini
Ghana. Ghana yenyewe bado haijaripoti visa vyovyote vya maradhi hayo.
Mlipuko huo umeleta athari kubwa kwa nchi zilizoathirika
zaidi ambazo ni Liberia, Sierra Leone na Guinea ambako chakula kimekuwa adimu
kutokana na ugavi kutetereka.
Nchini Liberia, uchaguzi umeakhirishwa kwa sababu
mikusanyiko ya watu kwenye vituo vya kupigia kura inaweza kuhatarisha maisha.
0 comments:
Post a Comment