Wiki iliyopita, mwandishi wa makala haya aliyewahi kuwa Mkuu wa Freemason Afrika Mashariki, Sir Andy Chande alisimulia namna alivyoanzisha Shule ya Shaaban Robert, pia alieleza kuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alikuwa gavana wa kwanza wa shule hiyo. Sasa endelea…
Akisimulia mchango wangu, Waziri Mkuu Frederick Sumaye (wakati huo), alisema: “Wakati tunasherehekea mchango wa watu ambao kila siku wamekuwa sura ya shule hii, ni vizuri pia kama tutawashuruku wote hata wale ambao wanatoa mchango wao nyuma ya pazia na mmoja wao ni Dk Chande, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa shule.
“Ningependa kumpongeza hasa Dk Chande siyo kwa msaada mkubwa alioutoa tu bali kwa tuzo aliyopokea ambayo siyo rahisi kuipata. Nina kila sababu ya kusema Dk Chande amefanikiwa katika kuonyesha utu, utendaji kazi ngumu na kujitoa.”
Kutokana na mchango wangu wadau wa shule waliamua kuupa jina langu ukumbi wa mikutano ambao ulikuwa umefunguliwa na Rais Benjamin Mkapa. Kabla ya kufanya hivyo waliniomba ruhusa.
Katika hali hiyo hiyo, mwaka 1970, aliyekuwa Meya wa Dar es Salaam, Kitwana Kondo, naye alinifuata akiniomba mtaa mmoja Dar es Salaam uitwe jina langu. Nilikataa nikamwambia kwetu hatufanyi hivyo, labla mtu atakapo fariki dunia.
Nikirudi kwenye mabadiliko makubwa yaliyokuwa yakitokea katika nchi yetu, ingawa mimi nilikuwa nikishiriki kwenye jamii ya watu wenye asili ya Asia, uhusiano wangu na Rais Nyerere ulinifanya nione vitu kwa mtazamo tofauti kabisa.
Ingawa nilikataa ombi la Tanu lililotaka nisimame kama mgombea wa chama hicho kule Tabora mwaka 1960, uhusiano na Mwalimu Nyerere ulinifanya niingie serikalini.
Ilipofunguliwa ofisi, Mwalimu Nyerere alinipa mialiko mingi ya kuonana naye jambo lililoongeza umuhimu kwangu kutoka kiongozi tu wa kawaida wa makumbusho ya taifa hadi kwenye ngazi za juu serikalini.
Nilichaguliwa kuwa mwanachama wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco). Kitu cha muhimu zaidi kwangu ni kwamba niliweza kumsaidia Mwalimu kabla ya Uhuru kama mfanyabiashara zaidi kuliko mwanasiasa.
Nafasi yangu katika Makumbusho ya Taifa kabla na baada ya uhuru haikuwa na umuhimu, lakini ilinipa fursa kutembelea baadhi ya sehemu muhimu za makumbusho kwa wakati ule.
Mwaka 1964, nikiwa mwenyekiti wa Makumbusho ya Taifa nilipata nafasi ya kuzungumza na mvumbuzi maarufu, Dk Louis Leakey kuhusu uwezekano wa kurejesha fuvu la Zinjanthropus aliloligundua yeye na mkewe, Maria huko Olduvai Gorge, Kaskazini mwa Tanzania.
Kitu cha kushangaza jambo hili lilikuwa rahisi kuliko nilivyotarajia. Pamoja na kuwapo kwa mikataba iliyokuwa imesainiwa na Dk Leakey na Waziri wa Elimu, Oscar Kambona, Dk Leakey hakuwa tayari kurudisha fuvu hilo nchini.
Alisema alikuwa ana majukumu mengine ya kimataifa yaliyokuwa yanahusiana na fuvu lile, kwa hivi sasa ilikuwa ni kazi yangu kumshawishi kulirejesha nchini.
Nilikuwa na mikutano mingi sana na Dk Leakey katika majaribio yangu ya kumshawishi hadi tulipofikia mahali ambapo pia palionekana kumsaidia yeye kisayansi.
Makubaliano yetu yalikuwa ni kujenga chumba chenye kiyoyozi kilicho na usalama mkubwa na kumwajiri mfanyakazi mwenye taaluma ya uhifadhi mambo ya kale ili aendeleze utafiti wa kisayansi.
Baada ya kukubaliana mambo hayo ndipo mwafaka ukafikiwa kati yangu na Dk Leakey. Tukaanza kuangalia namna ya kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza makubaliano.
Wakati huo Makumbusho ilikuwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Michezo na Utamaduni, bajeti kubwa ya wizara ilikuwa inakwenda katika mambo ambayo siyo ya kitamaduni.
Nilimpigia simu Waziri Mgonja, aliniambia kuwa fedha zilikuwa kidogo mno Hazina zisingeweza kusaidia ujenzi wa mradi huo.
Kilio changu cha kutaka kusaidia uhifadhi hakikusikilizwa. Baada ya kusikia kutoka kwa waziri nilikwenda kwa Rais Nyerere, alifurahishwa na wazo la Dk Leakey, lakini akaniomba niendelee kutafuta fedha kutoka kwa wafanya biashara zaidi kuliko serikali.
Hatimaye jitihada zangu zilifanikiwa, msaada ulipatikana kutoka kwa Kampuni za Williamson Diamonds, Gailey na Unilever Group. Michango hii siyo tu ilitosha kutimiza masharti ya Dk Leakey, ilitosha kujenga ukumbi.
Wakati wa ufunguzi, Rais Ali Hassani Mwinyi, Dk Leakey na mtoto wa Louis walitoa hotuba nzuri kwa Kiswahili. Wakati huohuo, Bodi ya Makumbusho chini ya msaada kutoka Serikali ya Denmark walimpata mtaalamu wa mambo ya kale aliyekuwa akiitwa Meyer Hesselberg, ambaye wakati huo alikuwa Ghana.
Ili kuharakisha Hesselberg anaanza kazi haraka, nililazimika kutumia njia ya mkato, badala ya kwenye Hazina, nilimwomba Dk Wilbert Chagula, aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam aandike barua ili Hesselberg afundishe chuoni hapo atakapokuwa akifanya kazi Makumbusho.
Chuo na Ubalozi wote walikubaliana na mawazo yangu. Kwa msaada wa kamati ya nyumba iliyokuwa chini ya Katibu Mkuu David Mwakosya.
Baada ya miezi mitatu tangu awasili nchini, Hesselberg aliiandikia barua Hazina akiomba kuingiza gari nchini bila kulipa kodi. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Katibu Mkuu wa Hazina, Jacob Namfua aliniita nikamweleze ni serikali ngapi zilikuwa zikiendesha nchi.
Hatimaye baada ya kueleza nini kilichokuwa nimetokea, Namfua alikubali. Fuvu hilo bado lipo kwenye makumbusho ya taifa hata sasa pamoja na mapambo mengine aliyoyatoa Dk Leakey.
Kumekuwapo na uvumbuzi mwingine kule Gorge na sehemu nyingine, lakini siwezi kusahau siku ya kwanza nilipoona fuvu la Zinjanthropus, ambalo ni la mtu wa kale zaidi kuishi duniani.
Mwaka 1965 niliteuliwa kushiriki kwenye kikao Umoja wa Kiarabu (UAR) kuzungumzia mikataba ya kibiashara. Timu kutoka Tanzania ilikuwa na Jerry Kasambala aliyekuwa Waziri wa Biashara na Ushirika, Uli Mwambungu, Katibu wa wizara na mimi mwenyewe. Katibu wetu alikuwa Nasor El-Buali.
Tulisafiri hadi Cairo kwa ndege ya Umoja wa Falme za Kiarabu tukiwa na Ahmed Shafik Mustafa kutoka Ubalozi wa Jumuiya za Kiarabu.
Naweza kusema hakukuwa na utaratibu siku ile, watu walikunywa bia walivyotaka hadi tulivyofika Cairo. Tulipowasili tulipokewa na Waziri wa Biashara ya Mambo ya Kigeni, Shukr. Alituacha tunywe juisi kwa muda mrefu katika chumba cha watu mashuhuri, hadi nilipomuuliza mtu aliyekuwa anatusaidia nini kilikuwa kinaendelea.
Ndipo tulipoambiwa kuwa Waziri wa Tanzania hakuwa na cheti kinachoonyesha kuwa alikuwa amechoma sindano ya homa ya manjano. Viongozi waliokuwa wanasimamia afya walikuwa wakimzuia kuingia.
Walisema wangeweza kumruhusu kwa kibali kutoka kwa Waziri wa Afya wa Misri, bahati mbaya wakati huo alikuwa akihudhuria harusi. Hatimaye walifikia mwafaka, tukaruhusiwa kuondoka uwanja wa ndege.
Japokuwa tulisafiri safari ndefu, tukasubiri sana pale uwanjani, bado waziri alikubali ofa tuliyokuwa tumepewa na wenyeji wetu ya kwenda kwenye klabu ya usiku ijulikanayo kama Shahara City. Wote tulirudi kwenye vyumba vyetu karibu na asubuhi.
Itaendelea kesho.
CHANZO : MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment