Ripoti kutoka Nigeria zinasema kuwa watu wanaodaiwa kuwa
wanamgambo wa kundi la Boko Haram wameushambulia mji wa kaskazini mashariki mwa
nchi hiyo unaopakana na nchi ya Cameroon na kuuawa mamia ya watu.
Shambulizi hilo limetokea jana katika mji wa Gamboru
Ngala kabla ya alfajiri ambapo watu hao waliuzunguka mji huo na kuushambulia
kwa risasi.
Seneta kutoka mji huo, Ahmed Zanna, amesema kuwa kwa
uchache watu 300 waliuawa katika shambulizi hilo huku nyumba na magari
vikirpotiwa kuchomwa moto. Katika matukio mengine baadhi ya watu walichinjwa.
Zanna amesema kuwa wanamgambo hao walifanya shambulizi
hilo baada ya kutokuwa na ulinzi kwa sababu askari waliokuwa hapo walikuwa
wamepelekwa upande wa kaskazini kwenye Ziwa Chad katika juhudi za kuwakomboa
mamia ya wasichana waliotekwa na wanamgambo hao Aprili 14.
Wakati huohuo tukio la kutekwa kwa wanafunzi wa kike
katika kijiji cha Chibok kaskazini mashariki mwa nchi hiyo limezusha kilio cha
kutoka kila kona ya dunia na maandamano makubwa nchini Nigeria kuishinikiza serikali
kuwakomboa wasichana hao.
Awali wapiganaji wa Boko Haram waliwateka wasichana 276,
lakini wasichana wapatao 53 walifanikiwa kutoroka. Katika tuiko la mwisho la
utekaji nyara mabinti lililofanywa na Boko Haram Mei 4, wasichana wasiopungua
11 walitekwa katika eneo la Gwoza kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno.
Mapema Jumatano, jeshi la polisi nchini humo lilitoa ofay
a dola 300,000 kwa yeyote anayeweza kutoa taarifa za kuaminika zitakazowezesha
kukombolewa kwa wasichana hao.
Kundi la Boko Haram limedai kuhusika na mashambulizi
kadhaa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo tangu mwaka 2009.
Mikoa kadhaa nchini Nigeria imekumbwa na ghasia mbaya
sana katika miaka ya hivi karibuni. Kwa miaka minne sasa, ghasia katika eneo la
kaskazini mwa nchi hiyo zimeyagharimu maisha ya watu 3,600, yakiwemo mauaji
yanayodaiwa kufanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment