Wapiga kura nchini Guinea-Bissau wanaelekea kwenye vituo
vya kupiga kura kumchagua rais na wabunge miezi miwili baada ya mapinduzi
yaliyotokea nchini humo.
Wapiga kura hao watamchagua rais mpya miongoni mwa
wanasiasa 13 huku vyama 15 vikiweka wagombea mbalimbali wa viti vya ubunge.
Uchaguzi huo unafuatiliwa na watazamaji 500 wa kimataifa
na kusimamiwa na askari 4,200 wa Guinea-Bissau na wengine kutoka Afrika
Magharibi.
Iwapo hatapatikana mshindi wa urais wa moja kwa moja,
uchaguzi wa marudio utafanyika Mei 18.
Uchaguzi wa leo ni wa kwanza tangu jeshi la nchi hiyo lilipofanya
mapinduzi mwaka 2012, ambapo Jumuiya ya Ulaya iliikatia misaada mbalimbali
iliyokuwa ikiipatia nchi hiyo.
Nchi hiyo ina historia ya mapinduzi mbalimbali tangu
ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ureno mwaka 1974. Hakuna rais ambaye amewahi kumaliza
muhula wote madarakani.
Wakati huo huo, wachambuzi wameitaka serikali mpya
itakayochaguliwa kuliweka jeshi chini ya udhibiti utakaolifanya liheshimu
matakwa ya wananchi na demokrasia.
Wanaitaka serikali kuzingatia suala la maafisa wa
kijeshi kufurahia maisha ya juu na kufanya mabadiliko ya sekta ya ulinzi ambayo
yamekuwa yakilifanya jeshi kufanya mapinduzi mara kwa mara.
Serikali mpya utakuwa na kibarua kigumu kupambana na
umasikini kwa kuwa theluthi mbili ya raia wa nchi hiyo wapatao milioni 1.6 wanaishi
chini ya msitari wa umaskini.
Nchi hiyo inakabiliwa na uchumi dhaifu, usafirishaji wa
madawa ya kulevya aina ya cocaine na ufisadi uliokithiri.
0 comments:
Post a Comment