WAANDAMANAJI
wanaoiunga mkono Urusi katika mji wa mashariki mwa Ukraine, Donetsk,
wametangaza kuundwa kwa taifa huru la Jamhuri ya Watu wa Donetsk.
Tangazo
hilo limetolewa na msemaji wa waandamanaji hao nje ya jengo la serikali, ambalo
kwa sasa linadhibitiwa na maelfu ya waandamanaji hao wanaoiunga mkono Urusi.
"Tunatangaza
kuundwa kwa taifa huru la Jamhuri ya Watu wa Donetsk kwa lengo la kutaka taifa
lenye nguvu, lenye uhalali na uhuru,” alisema msemaji huyo.
Wakati
huo huo, wabunge wa jimbo hilo wameamua kufanyika kwa kura ya maoni itakayoamua
iwapo wajiunge na Shirikisho la Urusi tarehe 11 Mei.
Kwa sasa
waandamanaji wanaripotiwa kuzidhibiti ofisi kadhaa za serikali katika mji huo
wa viwanda.
Kuna ripoti
kuwa waandamanaji hao walijaribu kukivamia kituo cha Televisheni cha Donetsk TV.
Aidha,
wameiomba Urusi kutuma majeshi ya kulinda amani katika jimbo hilo
walilolitangaza kuwa huru.
Risasi
kadhaa zilifyatuliwa hewani lakini hakujaripotiwa vifo au maafa yoyote.
Katika
mji jirani wa Kharkiv, makabiliano yameripotiwa kuzuka baina ya waandamanaji
wanaoiunga mkono Urusi na wale wanaoiunga mkono serikali ya Ukraine yenye makao
yake mjini Kiev. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, watu kadhaa wamejeruhiwa.
Katika
wiki za hivi karibuni maandamano ya kuiunga mkono Urusi yamekuwa yakishuhudiwa
katika miji ya mashariki mwa Ukraine.
Maandamano
hayo yalipata nguvu baada ya jimbo la Crimea kujitangazia huru na kufanya kura ya
maoni Machi 16, ambapo asilimia 97 ya washiriki walipiga kura ya kujiunga na
Shirikisho la Urusi.
Mnamo Machi
21, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alisaini hati maalumu za kuitambua rasmi Crimea
kuwa sehemu ya Urusi licha ya sauti zilizopazwa kutoka kambi ya Magharibi na
serikali mpya ya Ukraine.
Mgogoro
wa Ukraine ulianza mwezi Novemba mwaka jana baada ya aliyekuwa rais wa nchi
hiyo, Viktor Yanukovych, kukataa kusaini Makubaliano ya Ushirikiano na Jumuiya
ya Ulaya na badala yake akasaini makubaliano ya ushirikiano na Urusi.
0 comments:
Post a Comment