Na Zitto Kabwe
TANGU kuanza kwa Bunge Maalumu la
Katiba (BMK), nimekuwa mkimya kuliko nilivyozoeleka katika maisha yangu ya
kisiasa. Watu wengi wamekuwa wakiniuliza maswali kuhusu nini msimamo wangu
katika masuala anuai yanayojadiliwa ndani ya Bunge.
Hata hivyo, kuliko jambo lingine
lolote, ukimya wangu ulitokana na uzito wenyewe wa jambo ambalo BMK unatakiwa
kulifanya. Inapaswa kufanya utafiti mkubwa kabla ya kuzungumza maana haya
tunayoyafanya sasa yatakuja kusomwa katika vitabu vya historia miaka mingi
baada ya sisi sote kuondoka katika ulimwengu huu.
Bila shaka, uamuzi mkubwa zaidi
ambao BMK linatarajiwa kuufanya ni kuhusu aina ipi ya ushirika au mahusiano
ambao nchi yetu sasa itaamua kuufuata kupitia Katiba Mpya tunayotaka kuipitia.
Ni kuhusu idadi ya serikali
tutakazokuwa nazo na uhusiano utakaokuwepo. Serikali mbili au tatu. Tume ya
Jaji Joseph Warioba ilipendekeza muundo wa serikali tatu lakini inaonekana Rais
Jakaya Kikwete na serikali yake ya CCM wanapendelea kuendelea na mfumo wa sasa
wa serikali mbili.
Jambo moja ambalo nimejifunza wakati
nikifanya utafiti na kufuatilia mijadala mbalimbali inayoendelea kuhusu suala
hili ni kwamba Watanzania wengi wanapenda Muungano wetu uendelee.
Niseme mapema kwamba Watanzania
hatupaswi kuiga isipokuwa kujifunza kwa nchi nyingine. Hivyo muundo gani unafaa
ni uamuzi wetu wenyewe. Hata hivyo uamuzi huo ni lazima ujibu vigezo fulani
fulani.
Vigezo vikubwa ni viwili; Je, Muundo
tunaoutaka utajibu kero (malalamiko) za Muungano wa sasa? Je, Muundo tunaoutaka
utajibu hofu za Muungano kuvunjika. Muundo utakaojibu hofu hizo ndio utakaotufaa.
Suala la serikali ngapi zinatakiwa ni suala linalokuja baadaye baada ya kujibu
hoja hizo za msingi.
Kwa sasa, bado kuna utata iwapo
Tanzania ni Shirikisho (Federation) au ni Muungano (Union). Katika vikao vya
Kamati za BMK vinavyoendelea sasa, jambo hili limezua mjadala mkubwa ambapo
baadhi ya wajumbe wanapendekeza kuwa neno Shirikisho litoke kwenye Sura ya
Kwanza ya Rasimu ya Katiba na wengine wakipendekeza libakie au hata kuweka wazi
kabisa kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar.
Ni vema, kama mtu mwenye mapenzi
mema na Taifa lake, nikatumia fursa hii kuzieleza dhana hizi za muundo ili
zieleweke vizuri na watumiaji waweze kuzitumia kwa usahihi. Kwa ufupi tutazame
maana ya kila dhana na mifano mbalimbali duniani. Tutatazama dhana tatu kuu -
Muungano (Union), Shirikisho (Federation) na Jumuiya (Confederation/Community).
MUUNGANO
Katika mfumo huu, Nchi kuungana
kuunda Taifa moja, Dola moja ndani ya Nchi moja. Serikali za Washirika huachia
sehemu kubwa ya madaraka yao kwa Serikali ya Muungano. Mara nyingi muundo huu
hupelekea kuwapo kwa Serikali moja yenye nguvu (ya Muungano) na kama Washirika
wanabakia na serikali zao, basi hubakia na mambo machache sana. Faida ya Muundo
huu iko kwenye uimara wake na si rahisi kuvunjika.
Hasara za muundo huu ni athari ya
moja ya nchi, hasa kama ni ndogo, kumezwa na Mshirika mkubwa. Hapa Afrika, Nchi
ya Afrika ya Kusini inafuata muundo huu wa Muugano ambapo Serikali ya Muungano
ina nguvu na mamlaka mengi kuliko zile za Majimbo yanayounda Jamhuri ya Afrika
ya Kusini. Huko Asia mfano mzuri ni India ambapo japo muundo wake unatoa nguvu
kubwa kwa Majimbo kujitawala, Serikali ya Muungano (Union Government) ina nguvu
kubwa zinazoondoa sifa ya kuitwa Shirikisho.
Si lazima 'Union' kuwa na Serikali
moja (Unitary State) isipokuwa mazingira ya nchi husika ndio yanaweza kuamua.
Mfano mzuri hapa ni ule wa Afrika ya Kusini ambayo ni 'unitary state' yenye
Serikali 10, tisa za Majimbo na Moja ya Muungano.
SHIRIKISHO
Katika muundo huu, serikali za
washirika hukasimu sehemu ndogo ya madaraka yake kwa Serikali ya Muungano.
Mambo ya kidola (sovereign functions) hufanywa na Serikali ya Shirikisho na
Serikali za Washirika kubakia na mambo yake yenyewe.
Faida kubwa ya muundo huu ni kuondoa
hofu ya mkubwa kummeza mdogo na ule uhuru wa kujiamulia mambo mengi. Hasara ya
muundo huu ni kujengwa kwa utaifa au hisia za utaifa za Washirika ambazo
hatimaye hupelekea Shirikisho kuvunjika. Hapa Afrika mfano mzuri wa Shirikisho
ni nchi ya Ethiopia ambapo Majimbo yake yanao uwezo hata wa kujitoa katika
Shirikisho kikatiba.
Eritrea ilitumia fursa hii na
kujitoa kuwa sehemu ya Ethiopia mara baada ya mapinduzi yaliyomtoa Mengistu
Haile Mariam. Ujerumani pia ni Shirikisho.
JUMUIYA
Katika muundo huu kila Mshirika
anakuwa na uhuru wa mambo yake yote isipokuwa tu kunakuwa na mambo ya uratibu
wa pamoja. Aina hii ya Muundo ndio unapaswa kwa kinachoitwa Muungano wa
Mkataba.
Faida kubwa ya muundo huu ni kwamba
hakuna kubanana na pale kunapotokea hofu Mshirika hujitoa. Mfano mzuri ni
Uswisi na Jumuiya ya Ulaya. Hata Jumuiya ya Afrika Mashariki pia inaitwa ni
Muungano wa Mkataba.
MUUNDO GANI TANZANIA?
Tanzania kuwa Shirikisho au Muungano
ni mjadala ambao utaendelea kuwapo licha ya kuamua kuchagua muundo mmoja wapo.
Wakati wa kuandika Katiba ya India mwaka 1947 ubishani huu ulikuwa mkubwa sana
pia.
Katiba ya India imegawanya mamlaka
katika sehemu tatu - Mambo ya Muungano, Mambo ya Washirika na Mambo ya Pamoja
(concurrent). Wajumbe wa Bunge la Katiba la India wanaotaka Shirikisho
walipinga muundo huo na kukataa 'Washirika kuwa ombaomba kwa Serikali ya
Muungano'.
Hata hivyo ubishi huo ulimalizwa na
Mwanasheria mahiri wa India, BM Ambedkar, kwa kusema 'tunataka Serikali imara
ya Muungano na yenye nguvu iwezekanvyo' na alifunga mjadala kwa kusema
'Muungano wa Washirika unatakiwa zaidi kuliko Shirikisho la Washirika'.
Tanzania inaweza kuwa na Muundo wa
Muungano wenye Serikali tatu ama Muundo wa Shirikisho wenye Serikali mbili, ama
kinyume chake. Idadi ya Serikali haina uhusiano wowote na ama tunaitwa
Shirikisho au Muungano. Mifano miwili hapo juu ituongoze, India ni Muungano
unaitwa Shirikisho na Afrika Kusini ni Shirikisho linaloitwa Muungano.
Muungano wa Serikali 3 na sio
Shirikisho la Serikali 3 ndio mapendekezo yangu. Muungano (Union) wa Washirika
ni bora, imara na endelevu zaidi kwa mazingira ya Afrika kuliko Shirikisho
(Federation) la Washirika.
Mapendekezo yangu mahususi
yaliyowasilishwa kwenye kamati namba 12 ya BMK ni kama ilivyo hapa chini.
SURA YA KWANZA
SEHEMU YA KWANZA
1(1) Irekebishwe na kuandikwa upya
na isomeke
Tanzania ni Nchi Moja na ni Jamhuri
ya Muungano yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa Nchi za
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya
Makubaliano ya Muungano ya Mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.
1(2) neno Shirikisho lifutwe na
kuongeza maneno ....Nchi ya.... baada
ya neno 'ni' na kabla ya neno 'kidemokrasia'
Ongeza ibara ya mpya ya 3
itakayosomeka
3(1) Shughuli zote za Mamlaka ya
Nchi katika Jamhuri ya Muungano
zitatekelezwa na kudhibitiwa na
vyombo vitatu vyenye mamlaka ya
Utendaji, vyombo vitatu vyenye
mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na
pia vyombo vitatu vyenye madaraka ya
kutunga sheria na kusimamia
utekelezaji wa shughuli za umma
3(2) Vyombo vyenye Mamlaka ya
Utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na
Serikali ya Tanganyika; vyombo vyenye Mamlaka ya kutekeleza utoaji haki
vitakuwa ni mahakama ya Juu ya Jamhuri ya Muungano, Mahakama ya Tanganyika na
Mahakama ya Zanzibar na vyombo vyenye Mamlaka ya ya kutunga sheria na kusimamia
utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge la Jamhuri ya Muungano, Baraza
la Wawakilishi la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
3(3) Kwa ajili ya utekelezaji bora
wa shughuli za umma katika Jamhuri
ya Muungano, na kwa ajili ya
mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika
ibara hii, kutakuwa na mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza
ya Kwanza ya Katibahii, kutakuwa na mambo ya uratibu wa pamoja na kutakuwa na
mambo yasiyo ya Muungano ambayo ni mambo mengine yote yasiyo mambo ya Muungano
na yasiyo ya uratibu wa pamoja.
3(4) Kila chombo kilichotajwa katika
ibara hii kitaundwa na kutekeleza
majukumu yake na Katiba za Serikali
za Washirika na kwa kufuata
masharti ya katiba hii.
3(5) Kwa ajili ya utekelezaji bora
wa shughuli za Serikali ya Jamhuri
ya Muungano au Serikali ya
Tanganyika au Serikali ya Zanzibar Bunge
laweza kuigawa Jamhuri ya Muungano
katika Mikoa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge; Isipokuwa kwamba Bunge
litapata kwanza Azimio la Baraza la Wawakilishi la Tanganyika kwa mikoa ya
Tanganyika au Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa mikoa ya Zanzibar.
SABABU ZA MAREKEBISHO
YANAYOPENDEKEZWA
Rasimu ya Katiba imetangaza tu kuwa
'Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) ni Nchi' na kuacha 'ambiguity' ya kwamba
Tanzania ni nchi ngapi.
Katiba ya sasa imetamka bayana kuwa
'Tanzania ni Nchi Moja'.
Rasimu pia imetamka kwamba JMT
inatokana na 'muungano wa nchi mbili'. Hivyo basi ni vema kuweka wazi kabisa
kuwa Nchi hizi mbili zimeunda nchi moja. Hii itaepusha migongano ya siku za
usoni kuhusu tafsiri ya Katiba na Mamlaka za Nchi. Ifahamike wazi kuwa idadi ya
Serikali haina uhusiano na uundaji wa nchi moja.
Rasimu imetangaza kuwa Tanzania ni
Shirikisho ingawa bado imetamka 'Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (United
Republic of Tanzania).
Dhana za 'Union' na 'Federation' ni
dhana mbili tofauti katika miungano.
Idadi ya Serikali haina mahusiano ya
moja kwa moja na aina ya Muungano kama ni 'Union' au ni 'Shirikisho'. Kwa
mazingira ya Nchi za Kiafrika ni salama zaidi kuwa na 'Union' kuliko Shirikisho.
Rasimu imeweka sura ya Kwanza bila
kutaja vyombo vya Jamhuri ya
Muungano. Ni vema ili kuondoa
'ambiguity' vyombo vya Jamhuri ya
Muungano kutajwa kinagaubaga katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika sura ya 'uundwaji wa nchi'. Mapendekezo ya
ibara mpya za sehemu ya kwanza ya sura ya kwanza yanazingatia tahadhari hiyo.
Katika kutaja vyombo mapendekezo haya yanaonyesha dhahiri kuwa ugawaji wa Nchi katika
Mikoa inakuwa ni mamlaka ya Bunge.
Serikali za Washirika zaweza kuwa na
mamlaka ya Serikali za Mitaa. Mikoa inapaswa kuwa mamlaka ya Bunge la Muungano
kwa sababu yaweza pia kutumika katika kupata Wabunge wa Muungano lakini pia
itasaidia kuondoa tabia ya kugawa mikoa hovyohovyo.
Kimsingi ilipaswa Mikoa yote ya Nchi
itajwe ndani ya Katiba kuongezeka au kupunguka kwake kutokane na maamuzi
maalumu ya Bunge hata ikibidi iwe kwa theluthi mbili.
SURA YA SITA
Ibara ya 60(1) maneno shirikisho
yafutwe na kubaki uwepo wa Serikali 3.
60 (3) isomeke
Muundo, madaraka na mambo mengine ya
kiutendaji yahusuyo Serikali ya Tanganyika, na Serikali ya Zanzibar yataanishwa
katika Katiba za Washirika na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
Ibara ya 63 iitwe 63(1)
Iongezwe 63(2)
Kwa ajili ya uratibu bora wa
shughuli za Mamlaka za Nchi na kwa ajili
ya kuhakikisha ufanisi na weledi
katika uendeshaji bora wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
mgawanyo wa madaraka, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya
uratibu juu ya mambo ya uratibu kama yalivyoorodheshwa katka nyongeza ya pili
ya Katiba hii.
64(1) maneno nchi washirika yaondoke
na kubakia neno Washirika au
Washirika wa Muungano.
64(5) isomeke
Serikali za Washirika zitakuwa na
hadhi na haki sawa ndani ya Jamhuri
ya Muungano na zitatekeleza majukumu
yao kwa mambo yote yasiyo ya Muungano katika mamlaka za Serikali za Washirika
kwa mujibu wa
masharti yatakayowekwa na Katiba za
Serikali za Washirika kwa
kuzingatia masharti ya Katiba hii.
65 maeneo yote yenye maneno Nchi
Washirika yafutwe na kuandikwa
Washirika wa Muungano
67 ifutwe yote
69 maneno Nchi yafutwe ....katiba za
Washirika.......
69 (2) maneno Viongozi wakuu yafutwe
na kuandikwa ' Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Wakuu wa
Serikali za Washirika watakuwa ni Viongozi Wakuu wa Nchi'
69(3) isomeke
Viongozi wanaohusika na masharti ya
ibara hii ni
(a) Rais wa Jamhuri ya Muungano
(b) Mkuu wa Serikali ya Tanganyika
ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
(c) Mkuu wa Serikali ya Zanzibar
ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Ongeza ibara ya 70
(1) Mkuu wa Nchi ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambaye ataitwa Rais atapatikana kwa kuchaguliwa kwa kura
na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano kwa Mujibu wa masharti ya Katiba hii.
Rais atakuwa pia Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Wakuu wa Serikali za Washirika
watapatikana kutoka kwenye Mabaraza ya Wawakilishi ya Washirika kutoka Chama
cha siasa chenye wawakilishi wengi kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na
Katiba za Washirika na kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
SABABU ZA MAPENDEKEZO
Lengo ni kuhakikisha kuwa Jamhuri ya
Muungano inabakia ni nchi moja yenye serikali 3 zenye mamlaka na madaraka yake
yaliyofafanuliwa na katiba.
Kwa kuwa tunaamua kuwa na Nchi moja
basi Serikali zinazoundwa
zitakuwa ni Serikali Washirika na
sio nchi Washirika tena kama rasimu
inavyoita.
Kuweka wazi kuwa ni kiongozi mmoja
tu wa Serikali ndio
atachaguiwa na wananchi wote wa
Jamhuri ya Muungano naye ni Rais - Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi
ya Ulinzi na usalama.
Majina ya Wakuu wa Serikali za
Washrika yatatolewa na kwa mujibu wa Katiba zao na hivyo hakuna sababu kwa
Katiba ya Muungano kuunda majina isipokuwa tu Wakuu wa Serikali za Washirika
watakuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia kuwa iwapo
Rais wa Muungano anatoka upande mmoja wa Muungano, makamu wa kwanza atatoka
upande wa pili wa Muungano. Makamu wa Rais wanaweza kukaimu Urais kwa masharti
maalumu yatakayowekwa na Katiba.
Mapato na mgawanyo wa Mapato ya
Muungano katika Serikali Tatu
Dola inapasa kuwa na rasilimali za
kutosha na ziada inaweza kugawa kwa Washirika na Mikoa katika wajibu wa
kuhakikisha maendeleo yanawiana. Dola pia inaweza kuwa na miradi ya Muungano.
Kuna haja ya kuangalia kwa umakini mkubwa suala hili la mapato ya Serikali ya
muungano kama kweli kuna nia ya dhati ya kuendelea kuwa na Muungano.
Mapendekezo yangu ni kama ifuatavyo;
Mapato ya Muungano
1. Ushuru wa Forodha
2. Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali
ambapo 25% itabaki kwenye mkoa wenye rasilimali na 75% itatumika na Serikali ya
Muungano kugawa kwenye mikoa kwa mujibu wa ‘formulae’ itakayokubaliwa kwa
kuzingatia idadi ya watu, kiwango cha umasikini na ukubwa wa kijiografia.
3. Ushuru wa Bidhaa na huduma ambapo
60% itagawiwa kwa nchi Washirika kwa ajili ya miradi maalumu ya muungano.
4. Mapato kutoka kwenye kampuni za
kibiashara za Serikali ya Muungano na gawio la Benki Kuu ya Tanzania.
MAPATO YA SERIKALI ZA WASHIRIKA
1. Kodi ya Mapato ya watu binafsi na
Makampuni
2. Kodi ya Ongezeko la Thamani au
kodi kama hiyo
3. Tozo mbalimbali zitakazotungwa
kwa mujibu wa sheria
4. Mapato yasiyo ya kikodi kutoka
idara na Wizara za Serikali.
MAPATO YA MIKOA
1. 25% ya Mrahaba kutokana na
uvunaji wa Rasilimali/maliasili inayopatikana katika mkoa husika
2. 10% ya makusanyo ya kodi ya
mapato ya watu binafsi na makampuni kutoka katika mkoa husika
3. Mgawo kutoka Serikali ya Muungano
4. Mgawo kutoka Serikali ya
Washirika
5. Tozo mbalimbali zitakazoanzishwa
kwa mujibu wa sheria ndogo ndogo zitakazopitishwa na Mabaraza ya Mikoa.
Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini na pia Mjumbe wa BMK
CHANZO: RaiaTanzania
0 comments:
Post a Comment