Na Issa Shivji
UTANGULIZI
Nimefurahi kwa sababu huu ni mkusanyiko wa wanazuoni na
wasomi wenzangu ambao tumekusanyika kujadili jambo muhimu sana juu ya hatma ya
nchi yetu.
Sisemi hivyo kwa sababu huu ni mkusanyiko wa vijana;
kwangu mimi ujana na uzee hautegemei umri bali unategemea fikra na mawazo. Kama
wewe una fikra za kimaendeleo na ukombozi, basi wewe ni kijana bila kujali umri
wako. Na kama umechagua kujiunga na matabaka ya wanyonyaji na wakandamizaji na
kusambaza mtazamo wao basi, kwangu, wewe umezeeka hata kama una umri wa miaka
25!
Kwangu mimi nafasi hii niliyopewa ni kujadili mambo
mazito na kuelimishana. Kwa hivyo, mhadhara wangu utakuwa wa kuchochea mawazo
na fikra mbadala.
Maana ya mawazo mbadala kwangu ni mawazo ambayo huwezi
kuyakuta kwenye magazeti, kusikia yakisemwa na wasemaji wa kisiasa au kuyakuta
kwenye uchambuzi wa wasomi wa mambo ya utawala.
Nchi yetu (na hata bara letu la Afrika, ingawa leo
nitazungumzia zaidi nchi yetu) inapitia kwenye kipindi kigumu, kiasi kwamba
tuna wasiwasi kwamba nchi hii ya Tanzania itabaki kuwa nchi au itasambaratika.
Na mchakato wa Katiba Mpya unadhihirisha hali hiyo na ugumu wa kipindi hiki.
Mjadala unaoendelea juu ya Katiba Mpya umejikita, karibu
asilimia mia moja, kwenye suala la muungano, hususan muundo wake. Na hili suala
haliepukiki kwa sababu mambo yote mengine katika Rasimu yanategemea sana muundo
wa muungano.
Haraka haraka nitoe mifano miwili tu: Ukitaka kujadili
malengo makuu ya taifa (Sura ya Pili ya Rasimu), awali ya yote hunabudi ujibu
swali: Taifa lipi? Taifa la Tanganyika au la Zanzibar au la Tanzania? Na hili
Taifa la Tanzania liko wapi, na lina nafasi gani, katika rasimu?
Mfano wa pili: Ukitaka kujadili maadili na miiko ya
uongozi (Sura ya Tatu), inakubidi ujiulize: Viongozi wepi? Viongozi wa serikali
ya muungano, au serikali ya Tanganyika au serikali ya Zanzibar. Ukisoma Rasimu
kwa makini, utakuta viongozi wanaomaanishwa ni viongozi wa serikali ya
muungano. Kama ni hivyo, maadili haya – mazuri tu – yanawagusa vipi wananchi wa
Tanganyika na wananchi wa Zanzibar, wakati viongozi hao wa Muungano hawana
mamlaka juu ya rasilimali zao, ardhi yao, huduma zao, ustawi wao na, kwa jumla,
hali yao halisi. Mambo haya yote siyo mambo ya muungano na serikali ya muungano
haina mamlaka nayo.
Katika mjadala unaoendelea kumekuwa na malumbano na
mabishano kati ya wasemaji, wafuasi na wapigadebe wa ama serikali tatu au
serikali mbili. Wachambuzi, kama wapo, ni wachache sana – na hata hao wachache
hawasemi au hawasikiki. Rai yangu kwenu ni kwamba sisi kama wanazuoni
tusijidandie kundi lolote kati ya makundi hayo matatu.
Jukumu na wajibu wetu ni tofauti kabisa. Wajibu wetu ni
kuchambua hali halisi bila jazba; na kutokana na uchambuzi wetu kuonesha uzuri
na ubaya wa mambo. Sisi wanazuoni nafasi yetu ni kuwa kioo cha jamii, kuonesha
jamii uzuri na ubaya wake na kwa vipi na kwa njia gani uzuri unaweza
kuimarishwa na ubaya kupunguzwa.
Na huu ndiyo mwongozo wangu katika kufanya uchambuzi wa
mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar. Hoja nyingine juu ya muundo wa
muungano, kwa kweli, sitazigusia sana kwa sababu niliwahi kutoa mhadhara juu ya
Rasimu ya Kwanza, na Rasimu ya pili haijabadilika sana na vilevile mawazo yangu
hayajabadilika sana.
Na pia, kwa sababu, hivi karibuni imetokea hoja mpya
ambayo inarudiwarudiwa sana na wasemaji na wafuasi (pamoja na magazeti) wa
serikali tatu. Kwa hivyo, nimeona ni vema nijikite kwenye hoja hiyo ya
mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.
HOJA YA KUWA NA NCHI MBILI
Hoja ya mabadiliko ya 10 kuzaa nchi ya Zanzibar na kwa
hivyo kuwepo kwa nchi mbili zenye serikali mbili hivi sasa imewekwa vizuri na
kwa ufasaha katika Taarifa ya Mwisho ya Tume iliyotoka magazetini tarehe 26
Machi, 2014 (ang. Mwananchi ya tarehe hiyo, uk. 37). Kwa hivyo, nitatumia hoja
kuu za Taarifa hii kufanya uchambuzi wangu. Hoja zenyewe ni hizi zifuatazo:
1. Zanzibar imetangaza kuwa Nchi
Katika mabadailiko ya 10 Zanzibar "imetamka kwamba
ni Nchi tofauti na ilivyokuwa imetamka kwamba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano
kabla ya Mabadiliko hayo." Hii ni kinyume na Katiba ya Muungano.
2. Upunguzaji wa Mamlaka ya Bunge la Muungano
Katiba ya Zanzibar imeweka mipaka ya mamlaka ya Bunge la
Muungano katika Ibara ya 132 "ambayo inaelekeza kwamba Sheria iliyopitishwa
na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kuanza kutumika Zanzibar
ipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi na kupata ridhaa ya kutumika
Zanzibar". Hii pia ni kinyume na Katiba ya Muungano.
3. Upunguzaji wa Mamlaka ya Rais
Katiba ya Muungano imempa Rais wa jamhuri kuigawa
Jamhuri katika maeneo ya kiutawala katika Mikoa na Wilaya. Mabadiliko ya 10
sasa yameweka mamlaka hayo ya kuligawa eneo la Zanzibar katika Mikoa na Wilaya
mikononi mwa Rais wa Zanzibar. Kwa hivyo, marekebisho haya yamevunja Katiba ya
Muungano.
4. Upunguzaji wa Mamlaka ya Mahakama ya Rufaa
"Katiba ya Muungano ya 1977 imetoa mamlaka ya
kusikiliza rufaa nchi nzima. Lakini Zanzibar imezuia mahakama hiyo kusikiliza
rufaa kutoka Mahakama za kadhi, kutafsiri Katiba ya Zanzibar na rufaa kuhusu
mashauri ya haki za binadamu." Hii pia ni uvunjaji wa Katiba ya Muungano.
Baada ya hoja hizo, Tume katika Taarifa yake
inahitimisha kama ifuatavyo:
"Waasisi walituachia Bunge lenye madaraka nchi
nzima. Sasa ni lazima lipate idhini ya Baraza la Wawakilishi.
Waasisi waliacha Rais akiwa na madaraka kamili. Madaraka
hayo yamepunguzwa bila kufuata utaratibu wa Katiba.
Waasisi walituachia Mahakama ya Rufani yenye madaraka
kamili. Madaraka haya yamepunguzwa.
Waasisi waliunganisha nchi mbili ikawa nchi moja. Sasa
tunazo nchi mbili. … … … ".
"Tume iliona ni vigumu kwa Zanzibar kurudi kwa
hiyari kwenye hali ya awali, yaani kurudisha mambo yote yaliyotolewa kwenye
orodha ya Muungano, kurudisha madaraka ya rais na kufuta kipengere cha nchi
mbili kwenye Katiba yake. Tume iliona kwamba pamoja na mambo haya kufanywa
kinyume na Katiba ya Muungano hali ibaki hivyo hivyo. Lakini kwa kufanya hivyo
basi malalamiko ya Tanzania Bara nayo yasipuuzwe. Hivyo Tume nayo ikapendekeza
Serikali ya Tanganyika iundwe."
Ndivyo, kwa hoja hizo, Tume inavyohalalisha pendekezo
lake la Serikali tatu. Na bila shaka Tume iliona kwamba hoja hizo ni nzito sana
kiasi kwamba ndio hoja pekee iliyozungumziwa na kutolewa ufafanuzi katika
Taarifa yao ya mwisho.
Nitakachofanya sasa ni kuangalia hoja moja baada ya
nyingine. Tuwe pamoja.
1. Zanzibar imetangaza kuwa Nchi
Kabla ya kuingia kwenye ibara yenyewe ya Mabadiliko ya
10, kwanza tuelewe dhana ya nchi, dola na serikali na jinsi ilivyotumika katika
katiba zetu.
Nchi maana yake ni eneo la ardhi yenye mipaka ambayo
inatambulika; na eneo hilo lina utambulisho wake.
Dola maana yake ni chombo au mamlaka ya utawala ambayo
inatawala eneo maalum lenye mipaka yake. Yaani mipaka ya utawala wa dola ni
mipaka ya jurisdiction au mamlaka yake. Vyombo vitatu, yaani chombo cha
utendaji (ambacho huitwa serikali), chombo cha utungaji sheria (tunakiita
Bunge) na chombo cha kutoa haki (ambacho tunakiita Mahakama) ndivyo kwa pamoja
vinaunda dola. Mara nyingi sana katika lugha nyepesi tunachanganya dhana ya
dola na serikali. Serikali ni chombo kimoja tu katika vyombo vitatu
vinavyokamilisha dola. Ni muhimu sana kutofautisha serikali na dola.
Kwa mfano, huko Zanzibar kabla ya kuundwa kwa serikali
ya umoja wa kitaifa, CCM ndicho kilikuwa chama tawala. Kwa hivyo, tunasema
ilikuwa serikali ya CCM, lakini dola ni ya Zanzibar. Kama, kwa mfano, CUF
wangeshika madaraka, serikali ingekuwa serikali ya CUF, lakini dola ingebaki
kuwa dola ya Zanzibar.
Sasa mara nyingi katika msamiati wa kawaida maneno
serikali na dola yanachangaywa. Ili kujua tafsiri yake sahihi hatunabudi
tuangalie maneno haya katika muktadha (context) wake.
Sasa tuangalie mabadiliko ya 10 yanasemaje: Nukuu ya
ibara ya 1:
Zanzibar ni Nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote
la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari
yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya watu
wa zanzibar.
Neno linalotatiza hapa ni "nchi". Lakini
tujiulize, neno hili 'nchi' inamaanisha dhana ipi? Hoja yangu ni kwamba neno
'nchi' katika muktadha wa Katiba inamaanisha dhana ya DOLA na ndivyo limetumika
katika Katiba ya Zanzibar pamoja na Katiba ya Muungano. Nitathibitisha:
1. Ang. 9(1) ya Katiba ya Zanzibar: "Zanzibar ni
nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii". Maneno hayo hayo yametumika
katika Katiba ya Muungano: Ang. Ibara ya 8(1): "Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii …".
Tafsiri yake rasmi ya kiingereza ni, nitanukuu tafsiri ya 1998: "The
United Repiublic of Tanzania is a state which adheres to the principles of
democracy and social justice ….". Katika hili hakuna shaka kwamba neno
NCHI limetumika kumaanisha dhana ya dola, ambayo ni sahihi kabisa.
Hata Katiba ya Mungano inatambua dola ya Zanzibar
(pamoja na dola ya muungano). Ninukuu ibara ya 4:
4 (1) Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya
Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwi na vyombo viwili vyenye mamlaka ya
utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo
viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za
umma.
Na ibara ndogo (2) inaainisha vyombo hivyo: nukuu:
4 (2). Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni
serikali ya Jamhuri ya muungano na serikali ya Mapinduzi ya zanzibar; vyombo
vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni Mahakama ya serikali ya
Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na vyombo
vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma
vitakuwa ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.
Sasa ukijumlisha vyombo viwili viwili unapata dola ya
Muungano na dola ya Zanzibar.
Kwa hivyo, kama Katiba ya Zanzibar imetambua na
kufafanua kwamba Zanzibar ni dola, kosa liko wapi? Kwanini, jambo hilo linakuzwa
mpaka kudai kwamba Zanzibar imetangaza kuwa nchi?
2. Kama kweli mabadiliko ya 10 yaliitangaza Zanzibar
kama Nchi kwa maana ya "country", basi Zanzibar wangeuandikia Umoja
wa Kimataifa (UN) kwamba kwa mujibu wa Katiba yao Zanzibar ni 'sovereign
republic' yenye 'international personality'. Hii haijafanyika. Katika ngazi ya
kimataifa kuna 'sovereign republic' moja tu na ni Jamhuri ya Muungano. Bila
shaka, kwa mambo ya ndani mamlaka yamegawanyika kati ya dola ya Muungano na
dola ya Zanzibar (divided sovereignty). Na ndivyo inavyotokea katika muungano
na shirikisho.
3. Kama kweli, Zanzibar ni nchi yenye madaraka kamili
tangu 2010, kwa mujibu wa tafsiri ya Taarifa ya Tume, kwanini baadhi ya
Wazanzibari wanadai mamlaka kamili wakati already wanayo tangu 2010?
4. Kama kweli, neno nchi maana yake siyo dola, basi,
tujiulize Rasimu katika pendekezo lake la muundo wa serikali tatu limependekeza
nchi tatu? Yaani Nchi ya Tanganyika, Nchi ya Zanzibar na Nchi ya Tanzania? Na
hii nchi ya Tanzania ni ipi? Ni nchi hewa!
Ni wazi, na inathibitishwa na Rasimu yenyewe,
kilichopendekezwa ni nchi moja yenye dola tatu: dola ya Muungano, dola ya
Tanganyika na dola ya Zanzibar. Sasa ugumu wa kukubali Zanzibar kama dola uko
wapi?
Ni kweli, kama Tume invyosema katika Taarifa yake, kwamba
kabla ya mabadiliko haya, Katiba ya Zanzibar ilisema kwamba "Zanzibar ni
sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania". Kwanini basi Wazanzibari
waliona haja ya kutolea ufafanuzi 2010? Ninavyohisi mimi ni kwamba kwa kweli
Wazanzibari walichoka na wanasiasa, wasomi na hata mahakama [ang. Hukumu ya
Mahakama ya Rufaa iliyoandikwa na Jaji Ramadhani katika kesi ya S. M. Z. v.
Machano Khamis Ali & 17 Others,] kutokutambua Zanzibar kama dola. Kipigo
cha mwisho kilikuwa mwaka 2008 wakati Mhe. Waziri Mkuu aliposema kwamba
Zanzibar siyo Nchi. Kauli hii ya Waziri Mkuu ilileta mabishano na malumbano
makali ambayo hatimaye yalitulizwa na Rais Kikwete katika hotuba yake Bungeni.
Nionavyo mimi, hii ndiyo sababu iliyowafanya Wazanzibari waweke wazi kwamba
Zanzibar ni nchi kwa maana ya dola.
2. Upunguzaji wa Mamlaka ya Bunge la Muungano
Hii inahusu Ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar. Kwanza,
ibara hii haikuongezwa wakati wa mabadiliko ya 10. Imekuwa katika Katiba ya
Zanzibar tangu 1984, wakati muasisi mmojawapo bado alikuwepo. Na rasimu ya
katiba hii iliridhiwa na CCM. Nukuu ya ibara yenyewe ni hii:
132(1) Hakuna Sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la
Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka Sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo
ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya Baraza la
Wawakilishi na Waziri anayehusika.
Ibara hii inaweka masharti matatu ili sheria
iliyopitishwa na Bunge la Muungano itumike Zanzibar.
a) Iwe kwa ajili ya mambo ya Muungano. Hii haina ubishi
kwa sababu ndivyo Ibara ya Katiba ya Muungano (ib. 64) inavyoelekeza.
b) Iwe imepitishwa kulingana na maelekezo ya vifungu vya
Katiba ya Muungano. Hii pia haina ubishi.
c) Ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi.
Kinachozungumzwa hapa na sheria hiyo kuwa tabled katika Baraza la Wawakilishi
kwa taarifa.
Hii haina madhara yoyote. Ni kawaida kabisa kwa nyaraka
mbalimbali (kwa mfano sheria ndogondogo zinazopitishwa na serikali za mitaa au
Taarifa za Mashirika ya Umma) hupelekwa mbele ya Bunge kwa taarifa. Lakini hii
haina maana kwamba Bunge linaidhinisha au linaridhia nyaraka hizo.
Kwa bahati mbaya, Taarifa ya Tume imeongeza sharti
lingine jipya la kupata idhini ya Baraza la Wawakilishi ambalo halimo kabisa
katika ib. ya 132.
Ili kuthibitisha hoja yake kwamba sheria kama hizo
zinahitaji idhini ya Baraza la Wawakilishi, Tume inanukuu mifano miwili. Moja
ni Sheria ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (Commission for Human Rights and
Good Governance Act) na nyingine ni ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (Deep Sea
Fishing Authority Act) ambazo zilirudishwa na zilitakiwa ziridhiwe na Baraza la
Wawakilishi. Lakini hii ilikuwa ni sahihi kabisa kwa sababu sheria zote hizo
mbili hazikuwa juu ya mambo ya Muungano – haki za binadamu au uvuvi siyo mambo
ya Muungano.
Ukweli ni kwamba ni Bunge la Muungano ndilo lilivuka
mipaka ya mamlaka yake kwa kupitisha sheria juu ya mambo yasiyo ya muungano na
kutaka zitumike Zanzibar.
3. Upunguzaji wa Mamlaka ya Rais
Jambo hili linahusu madaraka ya rais kuigawa Jamhuri
katika maeneo ya utawala, yaani Mikoa na Wilaya. Ni kweli kwamba ibara ya 2 ya
Katiba ya Muungano imeweka mamlaka haya mikononi mwa Rais wa Jamhuri lakini
anapogawa Zanzibar katika mikoa na wilaya anatakiwa kushauriana na rais wa
Zanzibar. Ni kweli pia kwamba, mabadiliko ya 10 yameweka mamlaka haya mikonini
mwa Rais wa Zanzibar.
Labda tuchambue jambo hili kwa kina kabla hatujafikia
hitimisho.
1. Mambo ya utawala wa mikoa na wilaya, kwa jumla
serikali za mitaa, sio jambo la Muungano. Kwa hivyo, ni kosa kutoa mamlaka haya
kwa Rais wa Jamhuri. Kwa hivyo, kama kuna kosa, basi ni kosa la Katiba ya
Muungano na sio Katiba ya Zanzibar.
2. Katiba ya Zanzibar ya 1979 (ambayo ilikuwa katiba ya
kwanza ya Zanzibar baada ya mapinduzi) katika ibara yake ya 2(2) inasema,
nainukuu:
Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali,
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar aweza kuigawa Zanzibar
katika Mikoa, Wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu au kukubaliwa na
Chama cha Mapinduzi.
Rasimu ya Katiba ya 1979 iliidhinishwa na Kamati Kuu ya
CCM.
Kwa hivyo, kilichofanyika na mabadiliko ya 10 ni
kurudisha mamlaka haya mikononi mwa Rais wa Zanzibar ambayo ni sahihi. Kwa
hivyo, kama kuna Katiba inayotakiwa kurekebishwa, basi ni Katiba ya Muungano na
sio Katiba ya Zanzibar.
4. Upunguzaji wa Mamlaka ya Mahakama ya Rufaa
Ni kweli kwamba Mahakama ya Rufaa ni jambo la Muungano,
ingawa uamuzi wa kuongezwa kwake katika orodha ya mambo ya Muungano una
utatanishi. Ni kweli pia kwamba Katiba ya Zanzibar imeweka mipaka ya mamlaka
yake, kwa mfano, kesi kutoka Mahakama za Kadhi, kesi kuhusu tafsiri ya Katiba
ya Zanzibar na kesi kuhusu haki za binadamu haziwezi kwenda Mahakama ya Rufaa.
Kwa hivyo, kuna mgongano kati ya Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Muungano. Hata
hivyo, Mahakama zetu, pamoja na Mahakama ya Rufaa yenyewe, wamekwepa kutolea
maamuzi jambo hili, wamewaachia wanansiasa kufanya marekebisho.
Mgongano huo ungeepukika, pale ambapo Mahakama ya Rufaa
ya Afrika Mashiriki ilipovunjika, kama kungekuwa na mashauriano zaidi na
Wazanzibari jinsi ya kuunda Mahakama ya Rufaa ya Muungano na mamlaka yake. Hata
hivyo, kwangu mie jambo hilo sio kubwa na wala halipaswi kukuzwa.
Linarekebishika bila shida. Na mgongano huo haujawahi kuhatarisha uhai wa
Muungano.
Mwisho, ningependa kutoa tahadhari. Hoja za Tume
zinajaribu moja kwa moja kulaumu Wazanzibari kwamba ni wakosaji kwa kuvunja
Katiba. Hio sio sahihi. Ningependa kutoa mfano moja ambao uzito wake unapita
hoja hizo zote. Na mfano huu utadhihirisha kwamba kuna kasoro kubwa mno katika
Katiba ya Muungano.
Ibara ya 64 ya Katiba ya Muungano inasema kwamba Mamlaka
ya Kutunga sheria juu ya mambo ya Muungano yamo mikononi mwa Bunge la Muungano
na mamlaka ya kutunga sheria za Zanzibar juu ya mambo yasiyo ya muungano ni ya
Baraza la Wawakilishi. Hii ni sawa kabisa na inaendana na mfumo wa
"serikali mbili", au kwa usahihi zaidi, dola mbili, zilizowekwa na
Hati ya Muungano mnamo mwaka 1964 na katika Katiba ya Muungano wa 1977.
Lakini ibara ndogo ya 64(4) inasema: [nitanukuu maneno
yanayohusika]
Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote
haitatumika Tanzania Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo –
(a) Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika
Tanzania Bara na vivile Tanzania Zanzibar ….; au
(b) ……
(c) Sheria hiyo iwe inahusu Mambo ya Muungano, … .
Maana ya ibara hii ni kwamba Bunge la Muungano linaweza
kutunga sheria juu ya mambo yoyote yale hata kama sio mambo ya Muungano na
yatatumika Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ilimradi imesema tu kwamba
yatatumika Bara na Zanzibar. Hii, kwa kweli, inamaanisha kwamba Bunge la
Muungano limepokonya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi na kwa hivyo kuvuruga
kabisa muundo wa dola mbili. Ibara hii iliwekwa katika mabadiliko ya Katiba ya
Muungano ya 1984 baada ya machafuko ya hali ya hewa wakati Mheshimiwa Warioba
akiwa Waziri wa Sheria. [Ilitakiwa kuwekwa neno 'na' badala ya 'au'.] Mbaya
zaidi, ibara hii imetumika kupitisha zaidi ya shertia 40 juu ya mambo yasiyo ya
muungano na kutumika Zanzibar mpaka Wazanzibari wakaamka na kupinga sheria zile
mbili ambazo tumekwisha zizungumzia.
Ibara hii moja kwa moja inaathiri muundo uliowekwa na
Hati ya Muungano. Kwa hivyo, tunapolaumu Wazanzibari kuvunja katiba lazima pia
tuangalie upande mwingine wa sarafu. Na tukifanya hivyo ndio tutaweza
kusawazisha mambo haya yote katika Katiba mpya, badala ya kuyatumia kuhalalisha
muundo wa serikali tatu ambao ni wazi kabisa kwamba utavunja muungano.
***
Sasa nije kwenye hitimisho la Tume. Kama nilivyoonesha,
hoja tatu kati ya nne za kudhihirisha hoja kuu ya Tume sio sahihi. Na hoja ya
Mahakama ya Rufaa ni dogo. Kwa vyovyote vile, hoja hii ya mwisho haituruhusu
kabisa kuhitimisha kwa kusema kwamba waasisi waliunganisha nchi mbili ikawa
moja na sasa tunazo nchi mbili zenye serikali mbili. Kutokana na uchambuzi
wangu ambao ninawasilisha kwenu hitimisho langu ni kwamba waasisi walidhamiria
nchi moja yenye dola mbili na mpaka sasa tuna nchi moja yenye dola mbili. Ni
kweli muundo tuliyonao una matatizo lakini haya yanaweza kutatuliwa bila
kuhatarisha uhai wa muungano.
Hoja ya Tume kwamba kwa kuwa ni vigumu kwa
"Zanzibar kurudi kwa hiyari kwenye hali ya awali" na ndio maana
wamependekeza Serikali ya Tanganyika haina mashiko na inagongana. Kwanza, kama
nilivyoeleza kwamba sio sahihi kusema kwamba Zanzibar imetangaza kuwa nchi huru
kwa maana ya nchi. Pili, hata kama hii ingekuwa kweli, au kuna migongano kati
ya Katiba hizi mbili, basi ilikuwa ni lengo la mchakato wa Katiba Mpya
kusawazisha na kuondoa migongano hii. Isitoshe, pendekezo lenyewe la Tume
halitambuwi Zanzibar kuwa nchi na Tanganyika kuwa nchi, bali linaweka dola tatu
katika nchi moja badala ya dola mbili katika nchi moja kama ilivyo chini ya
Katiba ya 1977. Na hatunabudi, sisi ambao tunadai kuwa wataalam wa sheria za
Katiba kuwaeleza wanachi wote kwamba ikiwa Katiba Mpya (ya aina yoyote ile)
itapita kwa kura ya maoni ya wananchi wa pande zote mbili, basi sheria na
katiba ya sasa ya Zanzibar hazinabudi zirekebishwe au hata kuandikwa upya ili
kuendana na Katiba Mpya ya Muungano. Kwa kuwa itakuwa ni mara ya kwanza kwa
katiba ya Muungano kupitishwa kwa kura ya maoni, hakuna yeyote, pamoja na
wanasiasa wa pande zote mbili, wa kung'ang'ania katiba yao ya sasa. Kisheria na
kikatiba, Hati ya Muungano pamoja na Katiba ya Zanzibar ya 1984 hazitakuwa na
nguvu za kisheria; zitakuwa, kama tunavyosema, superceded. Muungano utakuwa
umewekwa kwenye misingi imara ya kikatiba ambayo chimbuko lake ni wananchi
wenyewe wa pande zote mbili.
HITIMISHO
Katika kuhitimisha mada yangu juu ya hoja hizi
zinazojikita kwenye mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, ningependa kutoa
tahadhari.
1. Bila kukusudia, hoja hii kama ilivyoandikwa katika
Taarifa ya mwisho ya Tume inaweza ikawa na hatari. Hii ni kwa sababu, moja,
inaamsha na kushawishi hisia za Utanganyika, na, pili, kufanya watu wa Tanzania
Bara wawachukie wenzao wa Zanzibar. Kwa hivyo, inahatarisha muungano badala ya
kuuimarisha. Na muungano wowote hauwezi kudumu, au kudumu kwa amani, kama hauna
mizizi katika watu na hisia zao.
Mimi binafsi sina shaka kwamba wazee wa Tume hawakuwa na
nia hii. Naamini kabisa kwamba wazee hawa walikuwa na nia njema tu. Lakini kama
usemi wa kizungu unavyosema: The road to hell is paved with good intentions kwa
maana kwamba 'Njia ya jehanam imetandikwa na nia njema.'
2. Juu ya hilo la Utanganyika, ningependa kuongeza
maneno machache hasa kwa faida ya vijana wetu. Nimeshangaa kidogo kwamba hata
mzee na mwanazuoni mwenzangu ametumia msamiati wa 'Utaifa wa Tanganyika' bila
kudadisi kihistoria 'Utaifa wa Tanganyika'.
Kwa muhtasari tu, kabla ya vita vya kwanza, hatukuwa na
Tanganyika. Tulikuwa na German East Africa ambayo eneo lake lilijumuisha
Burundi, Rwanda na eneo hilo la 'Tanganyika' chini ya himaya ya ubeberu wa
Wajerumani. Baada ya Ujerumani kushindwa katika vita, Rwanda na Burundi
ziligawiwa kwa Ubelgiji na Tanganyika kwa Uingereza. Waingereza ndio wakaunda
neno hili 'Tanganyika' na iliitwa 'Tanganyika Territory', yaani, ni bustani ya
wakoloni, sio taifa.
Mababu zetu waliopigania uhuru walijikita kwenye dhana
ya Utaifa wa Kiafrika, kama alivyoeleza vizuri tu Profesa Mpangala. Vyama vya
wananchi, kutoka TAA (Tanganyika African Association) mpaka TANU (Tanganyika
African National Union), viliweka msisitizo kwenye 'African', Uafrika wao.
Iliwabidi kuweka neno Tanganyika kwa sababu tu ndio lilikuwa eneo la utawala wa
wakoloni.
Tulipopata uhuru mnamo Desemba 1961, hatukuwa taifa kwa
sababu mkuu wa nchi bado alikuwa Malkia. Mwezi wa Novemba 1962 ndio tukawa
Jamhuri ya Tanganyika wakati Mwalimu alipochaguliwa kuwa Rais. Na Mwalimu tangu
mwanzo alisistiza kwamba sisi hatukuwa na taifa bali ni mkusanyiko wa makabila na
ilikuwa jukumu la serikali huru kujenga utaifa (nation-building). Lakini
Mwalimu hakupata muda wa kutosha kujenga utaifa wa Tanganyika kwa sababu mwezi
wa Aprili 1964, yaani baada ya miezi 14 tu, tukaungana na Zanzibar kuwa
Tanzania. Na kwa takriban nusu karne tumekuwa tunajenga Utaifa wa Tanzania.
Sasa hii dhana ya Utaifa wa Tanganyika, au Utanganyika, unatoka wapi? Na
mantiki na historia yake ni ipi?
Ningependa kujua hapa tulipo ni vijana wangapi kati yenu
mlizaliwa kama Watanganyika. Nyosheni mikono. Nyinyi wote mlizaliwa mkiwa
Watanzania, utaifa wenu ni Utanzania, Utambulisho wenu ni Utanzania,
mnajitambua kama Watanzania na mnatambuliwa na wengine kama Watanzania.
Ukweli ni kwamba mking'ang'ania Utanganyika wenu ambao
wala hamjui, mtakuwa mnavunja taifa na ndio maslahi na matakwa ya mabeberu na
wanasiasa wachache wenye uchu wa madaraka. Na Utanganyika wenu hautadumu kwa
sababu mtaanza kudai sasa Jamhuri ya Makonde na Jamhuri ya Sukuma! Mtakuwa
vipande vipande. Hivi sio vitisho; kuna mifano hai mbele yetu. Somalia
imesabaratika, Libya pia, Sudan, Afrika ya Kati, na nchi nyingine nje ya Afrika
– Afghanistan, Pakistan, Syria, Iraq bila kutaja nchi za Ulaya.
3. Kuna suala la Utaifa wa Zanzibar. Ukweli wa
kihistoria ni kwamba Wazanzibari angalau wanaweza kuzungumzia utambulisho wao
kwa sababu Zanzibar ina umri wa zaidi ya karne mbili. Na katika muungano wetu
utambulisho wao ulipewa kipaumbele kuondoa hisia za kumezwa na kupoteza
utambulisho wao kutokana na hali halisi ya watu wachache, nchi ndogo n.k. Na
Zanzibar kupewa special dispensation sio jambo geni hata kidogo. Popote pale
kunakokuwa na muungano wa nchi ambazo hazilingani kutakuwa na special
dispensation.
Mie sina shaka kwamba kama tungefanikiwa kuunda
Shirikisho la Afrika Mashariki mara baada ya uhuru, Zanzibar ingeomba na
ingepewa special dispensation. Ushahidi upo.
4. Mwisho, narudia tu nilichosema katika mhadhara wangu
niliotoa juu ya Rasimu ya Kwanza. Rasimu hii ina matatizo mengi. Kwa kweli
Muungano hauwezi kudumu ikiwa Rasimu hii itapitishwa na Bunge Maalum kama
ilivyo. Shirikisho lolote lile ambalo lina serikali ya shirikisho dhaifu, bila
vyanzo vya uhakika vya mapato, bila udhibiti madhubuti wa rasilimali, bila kuwa
na mamlaka juu ya sera za uchumi, fedha, forodha na masoko ya nje, na bila kuwa
na mamlaka juu ya ukusanyaji wa kodi, hauwezi kujiendesha.
5. Pamoja na hayo, mimi sisemi kwamba muundo wa serikali
au dola mbili tulionao hauna matatizo. Unayo. Lakini tusiangalie muungano kwa
jicho la idadi ya serikali. Tuuangalie kwa mtazamo wa demokrasia. Na tukifanya
hivyo tunaweza kubuni muundo ambao utakidhi mahitaji yetu bila kuhatarisha uhai
wa muungano.
6. Mie mwenyewe nimewahi kupendekeza mfumo mbadala
lakini sina muda wa kutosha kuelezea mfumo huo. Hata hivyo, nikipata nafasi
nyingine mwafaka nitajaribu kufanya hivyo.
7. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment