TAFRANI ilizuka usiku wa kuamkia jana katika Hospitali
ya Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar es Salaam, ikihusisha wanandoa baada ya
mke aliyekuwa amempeleka mtoto kutibiwa, kumbamba mumewe akimleta anayedaiwa
kuwa kimada pia kupata matibabu hospitalini hapo.
Mwandishi ambaye alikuwa hospitalini hapo saa 5 usiku,
alishuhudia mke huyo anayedaiwa kuwa wa ndoa akimpiga ngumi ‘nyumba ndogo’
kabla ya kumvamia mumewe na pia kumpiga ngumi akitaka amweleze mwanamke aliye
naye ni nani.
Mwanamke huyo ambaye jina lake halikupatikana, alikuwa
na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka mitatu ambaye alidai alizidiwa
usiku bila mumewe kuwepo.
Akisimulia watu waliokusanyika kushuhudia tukio hilo,
mwanamke huyo aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Mwananyamala, alidai baada ya
mwanawe kuzidiwa, alimpigia mumewe ambaye hakupokea simu, akitaka kumfahamisha
ugonjwa arudi nyumbani wasaidiane kumpeleka hospitali.
“Nilipoona simu
imezimwa kabisa, nikaamua kuchukua pikipiki haraka nikampeleka mtoto zahanati
na wakaniambia nimlete hapa (Mwananyamala),” alisema.
Aliendelea kusimulia, “nimefika nimefungua jalada,
nimekaa kusubiri kumwona daktari, nashangaa namwona mwanaume anaingia huku
amemkumbatia mwanamke aliyekuwa hawezi kutembea akigugumia kama mgonjwa
mahututi,” alieleza mama huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 28.
Baada ya kumwona mumewe akiwa na mwanamke huyo
amemwegemea kifuani, nao wakisubiri utaratibu wa kumwona daktari, mke huyo
halali alinyanyuka taratibu na kuomba ashikiwe mtoto.
Huku akimkaba mumewe, mwanamke huyo alisikika akisema,
“Nataka uniambie huyu ni nani, yaani mimi nateseka na mtoto nyumbani, anaumwa,
nakutafuta usiku huu sikupati, ukanizimia na simu, kumbe uko kwa malaya wako,
niambie ni nani huyu la sivyo utanitambua.”
Watu waliokuwepo waliingilia kati na kumshika huyo
mwanamke wa ndoa wakimtaka apunguze hasira.
Wakati akimng’ang’ania mumewe huku akitaka ufafanuzi,
mwanamke aliyedaiwa kuwa kimada, ambaye awali alifika hospitalini hapo akiwa ameshikiliwa
kwa kutojiweza kutokana na ugonjwa, alitumia nafasi hiyo kutimua mbio na
kuondoka katika eneo la hospitali asijulikane alikoelekea.
Baadhi ya madaktari na wauguzi waliokuwa zamu na watu
waliokuwepo hospitalini hapo, waliwaongoza wanandoa hao kutoka nje kwa kile
kilichosadikiwa ni kwenda kuzungumza na kumaliza tofauti zao.
Gazeti hili lilishuhudia wanandoa hao wakiondoka kwa
gari alilokuja nalo mume na haikujulikana walikokuwa wakienda. Haijulikani kama
walirejea hospitalini hapo kwa matibabu ya mtoto au walikwenda hospitali
nyingine.
0 comments:
Post a Comment