Siku moja baada ya kukalia kiti cha uongozi wa ligi ya
nchini Uingereza, meneja wa klabu ya Liverpool Brendan Rodgers, ametoa onyo kwa
klabu zinazoufukuzia ubingwa wa nchini humo kwa kusema zitapita katika majaribu
makubwa endapo zitahitaji kuwafikia hapo walipo kwa sasa.
Brendan Rodgers, ambae anapewa nafasi kubwa ya
kuirejeshea heshima klabu ya Liverpool kwa kutwaa ubingwa wa ligi ya nchini
Uingereza msimu huu, amesema maneno hayo ikiwa ni mara yake ya kwanza kukiri
wazi suala la kuhitaji taji baada ya kuyakwepa maswali ya waandishi wa habari
majuma kadhaa yaliyopita.
Rodgers, amesema ni wakati mzuri kwa wachezaji wake
kucheza kwa kujiamini na kujiona wana uwezo wa kufanya lolote kwa sasa,
kutokana na kufikia lengo ambalo walikua wakilihitaji tangu walipo poromoka
kutoka kileleni mwishoni mwa mwaka 2013.
Amesema baada ya ushindi wa mabao manne kwa sifuri dhidi
ya Spurs hapo jana, kazi iliyobaki ni kuhakikisha wanashinda michezo
inayowahusu mpaka mwishoni mwa msimu huu, huku akionyesha kutokuwa na wasi wasi
dhidi ya michezo miwiwli ambayo itamkutanisha na washindani wake katika ubingwa
Man city pamoja na Chelsea.
Katika hatua nyingine Brendan Rodgers amesema anatambua
jukumu lililo mbele yake ni kubwa kutokana na kubahatika kuwa meneja ambae
anafikiriwa huenda akaipa heshima Liverpool kwa mara ya kwanza tangu mwaka
1990, ambapo klabu hiyo ya Anfield ilitwaa ubingwa wa nchi kwa mara ya mwisho.
Rodgers amesema atafanya namna yoyote ile ili kutunza
heshima ya mameneja waliomtangulia ambao walikua na wadhifa kubwa katika medani
ya soka, hivyo hana budi kuendelea kuwasisitiza wachezaji wake juu ya suala
hilo ambalo lina umuhimu mkubwa.
Wakati huo hu aliyekuwa meneja wa klabu ya Liverpool
Gerard Houllier, ameonyesha kuwa na uhakika wa klabu hiyo kutwaa ubingwa wa
nchini Uingereza msimu huu, baada ya kuwa na matokeo mazunri katika siku za
hivi karibuni.
Gerard Houllier, ambae aliingoza Liverpool kuanzia mwaka
1998 hadi mwaka 2004 amesema The Reds wamekua na msimu mzuri msimu huu wakiwa
chini ya meneja Brendan Rodgers na soka wanalocheza linamuaminisha msimu huu ni
wa kwao.
Houllier, amesema matokeo ya siku za hivi karibuni
hususan ya mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs yameendelea kumpa faraja ya kuona
klabu hiyo inajihakikishia ubingwa.
Meneja huyo kutoka nchini Ufaransa ambae kwa sasa
ameamua kukaa pembeni katika nyanja ya ufundashaji wa soka kufuatia matatizo ya
kiafya ametoa sababu ya kuamini Liverpool huenda wakatwaa ubingwa msimu huu kwa
kusema kwamba wachezaji wote wa klabu hiyo kwa sasa wanaonyesha uwajibikiaji
kwa kujituma wakati wote, hali ambayo anaamini ndio nyenzo kubwa kwao ya
kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kipindi kirefu kilichopita.
Baada ya matokeo ya mabao manne kwa sifuri
yaliyopatikana katika mchezo dhidi ya Spurs, Liverpool wanashika usukani wa
ligi ya nchini Uingereza kwa kufikisha point 71, wakifuatiwa na Chelsea wenye
point 69 na nafasi ya tatu inashikwa na Man city waliofikisha point 67.
Hata hivyo Man City bado wana michezo miwili nyuma ya
vinara Liverpool, hali ambayo inachukuliwa kama changamoto ya utawala wa The
Reds kileleni.
0 comments:
Post a Comment