Zitto Kabwe
Mwalimu Azaveli Lwaitama ni mwalimu na mlezi wangu nje
ya darasa. Alipokuwa Katibu wa Umoja wa Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam mimi nilikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Idara ya Uchumi. Nilikuwa
nashinda kwenye Ofisi ya UDASA tukijadiliana kuhusu Umajumui wa Afrika
(Pan-Africanism), Ujamaa na harakati za kulinda haki za watu. Ilikuwa ni nadra
kwa mwanafunzi wa uchumi kuwa karibu na mwalimu wa lugha na mnadharia mkubwa.
Wanafunzi wa uchumi tulikuwa tunajidai na kujivuna. Tulikuwa tunajiona bora sana
maana darasa letu halikuwa linazidi watu 40 na kwa kweli wote hawamalizi.
Darasa langu tulimaliza wanafunzi 25 tu kati ya 40 tulioanza. Mwalimu Lwaitama
ni mpenzi mkubwa wa Muungano kama nilivyo mimi. Tumeapa kuulinda kwa namna
yeyote ile. Yeye alikuwa mhafidhina (conservative) sana akitaka Muungano wa
muundo huu aliouacha Mwalimu Nyerere. Mimi nataka kuulinda kwa kuufanyia
marekebisho makubwa sana ya kimuundo. Hatukuwa tunakubaliana.
Wiki iliyopita Mwalimu Lwaitama kaandika kuhusu muundo
wa Muungano katika makala zake za kila wiki katika gazeti la kimombo la The
Citizen. Amebadili msimamo. Ameona sasa muundo wa Muungano ulivyo sio endelevu.
Ametoa mapendekezo niliyoyatoa siku za nyuma katika mazungumzo yetu ingawa yeye
bado anayasema kwa shingo upande. Lwaitama sasa anataka Serikali mbili
zilizonyumbuliwa. Anapendekeza Waziri Mkuu wa Muungano mwenye nguvu za za
kitendaji. Nampongeza kwa kuboresha mawazo yake.
Hata hivyo bado Mwalimu wangu na Watanzania wengi
wamejikita katika mjadala wa Serikali ngapi. Idadi ya Serikali inaonekana kama
ndio dawa ya kero za Muungano. Ni kweli Wazanzibari wanataka uhuru zaidi na
wengine hawataki kabisa Muungano. Unawalalia. Unawanyima uhuru wa kuamua baadhi
ya mambo yao na japo halisemwi unawanyima wanasiasa wa Zanzibar mamlaka ya
masuala mengine ambayo yangewafanya wajilimbikizie madaraka.
Huku bara napo kuna watu, tena wanaongezeka kwa kasi
kweli kweli, wakitaka Tanganyika yao. Tena wengi vijana. Demografia zetu
zinaonyesha kwamba Watanganyika waliozaliwa Tanganyika ni takribani asilimia 12
tu ya Watanzania. Asilimia 70 ya Watanzania wamezaliwa wakati Muungano
umeshasherehekea miaka 15 ya kuzaliwa kwake. Lakini wanataka Tanganyika yao.
Wamechoshwa na kelele za Wazanzibari. Hawawataki Wazanzibari kujaa kwenye Bunge
la Muungano wakati wapo kiduchu sana. Wanasiasa nao, japo hawasemi waziwazi
wanataka wawe na mamlaka zaidi bila kulazimika kushauriana na wanasiasa wa
Zanzibar. Linapokuja suala la wagombea Urais ndio kabisa wanakereka kutafuta
mgombea mwenza kutoka Zanzibar. Wachambuzi wa historia za kisiasa siku wakiamua
kufanya tafiti watachoka na roho zao watakapoona aina za wagombea wenza ambao
wagombea Urais huteua, hasa kutoka sisi vyama vya upinzani.
Kimsingi idadi ya wapinga Muungano inazidi kuongezeka
siku hata siku. Ukiwauliza kwa nini hawataki Muungano wanasema aah, basi tu.
Kama ni Mzanzibari atasema Tanganyika wanatutawala. Kama ni Mtanganyika atasema
Wazanzibari wamezidi kelele, tunataka Tanganyika yetu. Sisi ‘Unionists’
(Wanamuungano) nao hatuna majibu ya kuridhisha sana na ya kukonga nyoyo.
Isipokuwa tu, Muungano huu ni wa aina yake Afrika na Duniani. Ni alama pekee ya
kuonyesha Mwafrika kupinga mipaka ya kikoloni. Sasa hili haliwaingii kichwani
‘secessionists’ (Wanautengano) na hatuna la kuwasaidia. Lakini ni lazima
tuurekebishe Muungano huu. Ulivyo sasa utavunjika tu. Kuulinda Muungano ni
kuufanyia marekebisho makubwa. Mwalimu Lwaitama kaliona hilo. Pendekezo lake
liboreshwe sasa. Sio rahisi sana.
Sasa tufanyeje? Serikali moja itaimeza Zanzibar.
Serikali Tatu ni gharama kuendesha na Serikali mbili zimeimeza Tanganyika na
watu wanataka Tanganyika yao na zinainyima uhuru Zanzibar na watu wanataka wawe
huru zaidi. Mfumo wa Serikali ngapi na kadhalika ni moja ya mikakati ya
wanasiasa katika kusaka vyeo. Sisemi sio halali kujadili lakini kiukweli mfumo
gani wa Muungano hautaongeza fungu la dagaa kwa mwananchi wa Kagongo au sinia
la ubwabwa kwa mwananchi wa Mkanyageni. Waingereza wana msemo ‘unataka kula
keki yako na kubaki nayo’, basi tuwe na Serikali zote.
Nimeanza na Mwalimu Azaveli Lwaitama. Naboresha hoja
yake kwa kurudia niliyowahi kuyasema huko nyuma kuhusu muundo wa Muungano. Tuwe
na Dola Moja tu. Ndio, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wala sio Shirikisho
la Tanzania (kwanza litatuondoa kwenye kiti chetu kule Umoja wa Mataifa maana
kwa jina letu sisi tunakaa katikati ya Uingereza na Marekani. Katikakati ya
mabwana wakubwa, labda ndio maana wanatupa misaada sana, unajuaje?). Tuwe na
Rais mmoja tu mwenye mamlaka kamili ya Asasi za Dola – Mambo ya Nje, Ulinzi na
Usalama, Uhamiaji, Sera za Fedha na jukumu la jumla la kusimamia ustawi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Achaguliwe na Watanzania wote wa pande zote
mbili za Muungano kwa kupata zaidi ya nusu ya kura za pande zote za Muungano.
Tuachane na mambo ya Mgombea Mwenza. Tumejaribu tumeona hana maana zaidi ya
kutembea na mikasi tu.
Zanzibar iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote
ambayo sio ya Muungano. Tanganyika iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote
ambayo sio ya Muungano. Hawa watateuliwa na Rais wa Muungano kutoka chama
chenye Wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi Tanganyika na Baraza la
Wawakilishi Zanzibar. Wote watakuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
kwa utaratibu kwamba iwapo Rais anatoka Zanzibar, basi Waziri Mkuu wa Tanganyika
atakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Pili wa Rais.
Kule kule kwenye misingi haswa ya Muungano. Hawa wataongoza Mabaraza yao ya
Mawaziri na watakuwa na nguvu ya kuteua na kufukuza Mawaziri wanavyotaka.
Hawatakuwa Wabunge katika Bunge la Muungano.
Bunge la Muungano litakuwa dogo lenye Wajumbe wasiozidi
101 pamoja na Rais wa Bunge la Muungano. Wabunge wa Muungano watatoka kwenye
mikoa (au Majimbo kama sera ya Majimbo itakubalika). Kwa utaratibu wa sasa kila
mkoa utachagua wabunge 2 mmoja mwanamke mmoja mwanaume kwenda Bunge la
Muungano. Wajumbe wa Ziada watatokana na uwiano wa kura ambazo kila chama
kimepata kwenye kura za Rais wa Muungano. Idadi hii yaweza kupunguzwa na hata
kuwa na Wabunge 51 tu akiwemo Rais wa Bunge la Muungano ambapo kwa mikoa ya
sasa kila mkoa utachagua Mbunge 1 na wengine watokane na uwiano. Rais wa
masuala ya Muungano atakuwa Mkuu wa Shughuli za Serikali katika Bunge la
Muungano na Rais kwa mwaka mara moja atahutubia Baraza la Taifa (Wabunge wa
Bunge la Muungano na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka kila upande wa
Muungano). Wazungu wanaita hotuba hii ‘State of the Union’ (Hali ya Taifa) na
wengine huita ‘Queen’s Speech’ (Hotuba ya Malkia).
Mkuu wa nchi mmoja, Dola moja ya Jamhuri ya Muungano.
Serikali mbili na kila upande una Serikali yake yenye mamlaka kamili ya maisha
ya watu wao ya kila siku. Haya matatu pamoja na Serikali ndogo ya Muungano.
Lakini tutakuwa tumepata kila kitu labda. Wenye kutaka Uhuru mpaka Zanzibar
watapata. Wenye kutaka Tanganyika watapata na wenye kutaka Muungano kama Dola
yenye nguvu watapata.
CHANZO: Ukurasa wake wa facebook

0 comments:
Post a Comment