![]() |
| Waandamanaji wakikabiliana na polisi katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev leo Februari 20, 2014. |
Kwa uchache watu 25 wamepoteza maisha nchini Ukraine katika
makabiliano mapya baina ya Polisi na waandamanaji wanaoipinga serikali na
kufanya idadi ya vifo kufikia zaidi ya watu 50.
Ghasia hizo ziliibuka baada ya wandamanaji waliojihami
kuvamia vizuizi vilivyowekwa na polisi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kiev.
Waandamanaji wameudhibiti uwanja Maarufu wa Maidan
(Uwanja wa Uhuru) katika mji huo, ambapo maelfu ya waandamanaji wamegoma
kuondoka.
Hivyo ni vifo vipya kabisa kuanza kwa wiki hii, ambapo
ghasia ziliibuka baada ya kwisha kwa muda wa mwisho uliowekwa na mamlaka za
usalama zikiwataka waandamanaji kuondoka.
Ghasia hizo mpya zimekuja licha ya kuwepo kwa
makubaliano baina ya Rais Viktor Yanukovych na viongozi wakuu wa upinzani.
Rais Yanukovych alitangaza mapatano hayo usiku wa
kuamkia leo katika juhudi za kujaribu kuikwamua nchi hiyo.
Wakati huo huo, Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka
Ufaransa, Ujerumani na Poland wamekuwa wakiendesha mazungumzo ya kutanzania
mgogoro huo mjini Kiev.
Maafisa wa Ulaya wanasema kuwa wanafikiria kuchukua
hatua za vikwazo dhidi ya serikali ya Ukraine kutokana na mgogoro huo.
Marekani imeweka vikwazo vya kuwapatia pasi za kusafiria
maafisa waandamizi 20 wa Ukraine ambao wanadaiwa kutenda au kutoa maagizo ya
ukiukwaji wa haki za binadamu katika ghasia hizo.
Kwa upande mwingine, Urusi imeyataka makundi ya upinzani
nchini Ukraine kuacha ghasia na kukaa katika meza ya mazungumzo na serikali ili
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo kwa njia ya amani.
Ukraine ilikumbwa na maandamano dhidi ya serikali baada
ya Rais Yanukovych kukataa kusaini Mkataba wa Ushirikiano na Umoja wa Ulaya Novemba
29, 2013, na badala yake akasaini mkataba wa kibiashara nan chi ya Urusi.

0 comments:
Post a Comment