![]() |
| Mojawapo ya mabasi yanayotembea nchi kavu na majini. |
- Kwa
Afrika, Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kuwa na aina hii ya mradi wa
mabasi ya majini.
- Mabasi
hayo yana uwezo wa kutembea nchi kavu na majini, hii ina maana kuwa
yatasaidia kwa mfano kusafiri kutoka Posta kwenda maeneo mengine yoyote ya
jiji ambayo yanafikiwa na bahari.
- Mamlaka
ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) inasema mradi huo unaweza
kusaidia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji nchini.
Serikali, mashirika binafsi na wadau wa usafiri ndani na
nje ya nchi wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na msongamano wa
magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Msongamano huo ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na
uduni wa miundombinu ikiwemo barabara, umekuwa ni kero kwa wananchi na Serikali
kwa jumla.
Serikali imewekeza katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi
(BRT) na usafiri wa treni ndani ya Jiji la Dar es Salaam kama njia mojawapo ya
kumaliza tatizo la msongamano wa magari na foleni.
MSINGI WA TATIZO
Chanzo kikubwa cha foleni jijini Dar es Salaam si wingi
wa abiria bali ni wingi wa magari binafsi na njia finyu zisizokidhi mahitaji ya
watu walioko katika jiji hilo.
Njia muhimu ya kupunguza foleni na msongamano wa magari
ni kupunguza wingi wa magari barabarani na kuweza kuzipanua barabara ili kuwe
na uwezekano wa kupita kwa urahisi.
Kutokana na foleni na uduni wa huduma za usafiri wa umma
watu wa kundi la kati, wamekuwa wakikimbilia kununua magari binafsi kwa ajili
ya kwenda nayo kwenye shughuli zao kwa urahisi.
Aidha, katika kuendeleza harakati za kupambana na tatizo
la usafiri, Kampuni ya Transevents Marketing ya Tanzania kwa kushirikana na
Kampuni ya Dutch Amphibious Transport Vehicles (DATV) ya Uholanzi inaendelea na
mchakato wa kuleta usafiri wa mabasi ya abiria yenye uwezo wa kusafiri nchi
kavu na majini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Transevents, Peter Nzunda anasema
teknolojia hiyo ya mabasi ya nchi kavu na majini (amphibious) ina lengo la
kupunguza tatizo la foleni kwenye barabara za Dar es Salaam hususan katikati ya
jiji kwa kuwa mabasi hayo huweza kupita nchi kavu na majini.
Hii ina maana kuwa hata katika maeneo yenye barabara
zisizo nzuri au zenye tope, magari hayo huweza kupita hivyo kutosababisha
foleni kama ambavyo hutokea sasa katika baadhi ya maeneo hasa mvua zinaponyesha
na kuharibu barabara.
Anasema mbali na lengo hilo, mabasi hayo yatatumika kama
vivutio vya utalii kwa kufanya utalii wa baharini ambao kwa Tanzania haujashika
kasi, licha ya sehemu kubwa ya nchi kuzungukwa na maji.
“Mpango huo wa mabasi ya nchi kavu na majini unalenga
kutoa ushawishi kwa watu wa kundi la kati ambao wanatumia magari binafsi
waegeshe magari yao na kutumia usafiri huu ambao utakuwa wa hadhi yao na
unaokidhi haja kwa ubora wake,” anasema Nzunda na kuongeza:
“Lengo ni kujenga maegesho ya magari maeneo mbalimbali
kandokando ya bahari, watu wataegesha magari yao na kupanda mabasi yatakayopita
majini kwenda Posta na baadaye kurejea kwa utaratibu huohuo na kuyachukua
magari yao tena kwenye maegesho walipoacha magari yao”.
SHUGHULI ZA UTALII
Nzunda anasema mbali na teknolojia hiyo kutumika kama
usafiri wa umma Jiji la Dar es Salaam, mabasi hayo yatatumika kupeleka watalii
kwenye hifadhi za taifa zinazozungukwa na maji kama vile Bagamoyo, Mbudia,
Mafia na visiwa vingine ili kujionea mambo mengi zaidi ya kiutalii.
“Tunataka pia watu wanaokwenda kwenye fukwe wasiishie
kulala na kucheza mchangani, bali wawe wanapanda mabasi haya na kutembelea
sehemu mbalimbali zenye vivutio
baharini; hiyo itakuwa ni fursa ya watu kuzunguka baharini wakiwa ndani ya
mabasi hayo yatakayokuwa katika miundo tofauti,” alisema Nzunda.
MAHITAJI YA MRADI
Nje ya Kampuni ya Dutch Amphibious Transport Vehicles
(DATV) kutaka kuingiza teknolojia hiyo nchini, Serikali ya Uholanzi pia ipo
tayari kuchangia kwa asilimia 50 ya
gharama za mradi wote ambao gharama zake zitajulikana mara baada ya kufanyika
tathmini wa mradi.
Aidha, Serikali ya Tanzania, wawekezaji katika sekta ya
usafirishaji wa abiria nchi kavu na majini na wadau wengine watatakiwa
kuchangia asilimia 50 zilizobaki katika kufanikisha kuanza kwa mradi huo ambao
mchakato wa kupata kibali umeshaanza.
Meneja Mwendeshaji wa Transevents Marketing, Mahamud
Omari anaiomba Serikali kusaidia uharakishaji wa utoaji wa leseni ya uingizwaji
wa teknolojia hiyo mpya ya mabasi.
“Mchakato wa kupata kibali umeshaanza na matarajio yetu
ni kufanikisha hatua hiyo baada ya miezi sita kuanzia sasa,” anasema Omari.
Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Edna Rebecca anasema
mradi huo wa ‘Mabasi ya Majini na Nchi Kavu’ utatengeneza ajira nyingi kwa
vijana wengi na kuongeza fursa za kibiashara kwenye hoteli.
Pia mabasi hayo yataongeza pato la taifa kupitia utalii
na maendeleo ya teknolojia hiyo kwa jumla, kwa ajili ya kizazi hiki na kijacho,
ukizingatia takwimu za Shirika la Makazi Duniani, zinaonyesha miaka 50 ijayo,
Jiji la Dar es Salaam litakuwa na wakazi wapatao milioni 18.
Mabasi hayo yatatumika kwa shughuli za harusi hasa kwa
wanandoa ambao watapenda kufunga ndoa ndani ya maji.Pia yatatumika kwa safari
za kitalii za wafanyakazi wa kampuni mbalimbali, wanafunzi, wanakwaya,
wanavikundi na klabu za mipira.
“Usafiri huu utakuwa ni wa bei ya kati ambayo itaendana
na huduma bora na utalenga kuziba changamoto zote ambazo zinapatikana sasa
kwenye usafiri mwingine wa umma,” anasema Rebecca na kuongeza:
“Kuna watu wanapanda magari kwa kulipia Sh1,000 badala
ya Sh400 kutoka Posta kwenda Mwenge ili kukwepa adha ya kubanana kwenye
daladala zinazokaa muda mrefu kwenye foleni, kwahiyo unaweza kuona ni kwa namna
gani watu wanahitaji huduma bora za usafiri wa umma.”
Katika mazingira ya kawaida familia nyingi jijini Dar es
Salaam zinatumia magari matatu kwa wakati mmoja yaani baba, mama na mtoto,
jambo linaloongeza masongamano barabarani.
Rebecca anasema usafiri huo utawafanya watu hao kuyaacha
magari yao nyumbani au kwenye maegesho ya magari yatakayojengwa na hivyo
kupunguza kabisa idadi ya magari barabarani.
Mabasi hayo pia yatapunguza gharama za maisha
zinazotokana na matumizi ya mafuta kwani kama mtu anaweza kutumia lita 20- 50
kwa siku.
SERIKALI INASEMAJE
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra), David Mziray anasema teknolojia hiyo ya usafiri wa mabasi ya
nchi kavu na majini imekuwa na msaada mkubwa kwa nchi nyingi Ulaya, kuja kwake
Tanzania itakuwa ni habari njema hususan wakati huu ambapo jiji linakua kwa
kasi.
“Kazi yetu ni
kupokea maombi na kuangalia kama yanakwenda sambamba na sheria na kanuni zetu
na kama unavyojua hii ni aina mpya ya usafiri kwa hiyo lazima kutakuwa na mambo
ya msingi ya kuyajadili na kuyapatia ufumbuzi kabla ya kuanza,” Anasema Mziray
Baadhi ya wananchi wanasema mradi huo unaweza kusaidia
sana kuondoa kero ya usafiri Dar es Salaam.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:
Post a Comment