THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 PRESIDENT 'S OFFICE.
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com THE STATE HOUSE,
press@ikulu.go.tz P.O.BOX 9120,
Fax: 255-22-2113425 DAR-ES-SAALAM
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU BARAZA LA MAASKOFU WA
KIPENTEKOSTE TANZANIA (PENTECOSTAL COUNCIL OF
TANZANIA) KUTOKUWA NA UWALIKILISHI KATIKA BUNGE
MAALUM LA KATIBA
1. Uteuzi wa Wajumbe wa Bunge la Katiba unafanywa kwa
mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura, 83 (The Constitutional Review
Act, Cap 83). Sheria hii inaweka mamlaka ya uteuzi, masharti, taratibu, vigezo
na mambo mengine yote yanayopaswa kuzingatiwa katika uteuzi wa Wajumbe wa Bunge
la Katiba. Kwa mujibu wa Kifungu cha 22 (2A) na (2B) vigezo hivi vinajumuisha
umri, jinsia, uzoefu, sifa na mahali anapotoka mjumbe husika.
2. Sheria hii imeainisha aina tatu za Wajumbe wa Bunge
la Katiba kama ifuatavyo:
(i) Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
(ii) Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar; na
(iii) Wajumbe 201 kwa mujibu wa Kifungu Na. 22(1c) cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inaonyesha makundi mbalimbali 10
yanayohusika.
3. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, wajumbe
201 wanatakiwa kuteuliwa kutoka katika makundi yafuatayo:
(i) Taasisi zisizokuwa za Kiserikali (20)
(ii) Taasisi za Kidini (20)
(iii) Vyama vyote vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu
(42);
(iv) Taasisi za Elimu (20);
(v) Watu wenye Ulemavu (20);
(vi) Vyama vya Wafanyakazi (19);
(vii) Vyama vinavyowakilisha Wafugaji (10);
(viii) Vyama vinavyowakilisha wavuvi (10);
(ix) Vyama vya Wakulima (20); na
(x) Vikundi vya Watu wenye Malengo yanayofanana (20).
4. Mchakato wa uteuzi ulianza kwa kutoa Tangazo la
Mwaliko katika Gazeti la Serikali, Tangazo la Serikali Na. 443 la tarehe 13
Desemba, 2013. Tangazo hilo lilitolewa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ili
kuyaalika makundi yaliyotajwa kisheria kuwasilisha mapendekezo ya majina kwa
ajili ya uteuzi katika Bunge Maalum la Katiba. Aidha, Tangazo hilo lilitangazwa
pia katika magazeti mbalimbali yanayosomwa hapa nchini. Pamoja na mambo
mengine, Tangazo hilo lilitamka ukomo wa muda wa taasisi na makundi kuwasilisha
mapendekezo ya majina ya wajumbe kuwa ni tarehe 02 Januari 2014.
5. Mapendekezo hayo yalitakiwa kuwasilishwa kwa Katibu
Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kwa Katibu Mkuu
Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mapendekezo hayo yalitakiwa
kuwasilishwa kwa njia ya barua ya posta au barua inayoletwa kwa mkono. Sheria
haikutoa njia nyingine ya kuwasilisha mapendekezo. Ninafahamu, wengine
wangeweza kutumia barua pepe au hata ujumbe mfupi wa maneno. Sheria haisemi
hivyo!
6. Kufuatia mwaliko huo, taasisi 554 kutoka Tanzania
Bara na 178 kutoka Zanzibar ziliwasilisha mapendekezo yao. Mapendekezo hayo
yalijumuisha majina 2,762 kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar
mapendekezo hayo yalihusisha watu 874. Hivyo basi, taasisi na makundi
mbalimbali yalipendekeza jumla ya majina 3,636. Aidha, watu 118 walijipendekeza
wenyewe kinyume na matakwa ya kisheria na kufanya idadi ya majina
yaliyopendekezwa kuwa 3,754.
7. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imeweka masharti
katika uteuzi wa wajumbe 201 wa Bunge Maalum la Katiba. Masharti hayo, ni
pamoja na wajumbe wasiopungua theluthi moja wanatakiwa kutoka Zanzibar na
theluthi mbili kutoka Tanzania Bara. Kwa sababu hiyo,
katika wajumbe 201, wajumbe 67 wanatakiwa kutoka Zanzibar na wajumbe 134
wanatakiwa kutoka Tanzania Bara. Aidha, uteuzi huo unatakiwa kuzingatia idadi
ya wajumbe kutoka katika kila kundi kama ilivyoainishwa kisheria. Vilevile,
mgawanyo wa wajumbe wanawake na wanaume unatakiwa uwe nusu kwa nusu. Pamoja na
hayo, wajumbe hao wawakilishe sura ya wananchi wa Tanzania kwa ufuasi wa vyama
vya siasa, dini, umri, na maeneo anayotoka.
8. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar walikamilisha
uteuzi wa wajumbe 201 na majina ya walioteuliwa yalitangazwa tarehe 7
Februari 2014. Majina hayo yalitangazwa kupitia taarifa
kwa vyombo vya habari na pia Gazeti la Serikali kwa Tangazo la Serikali Na. 29
la tarehe 7 Februari 2014.
BARAZA LA MAASKOFU WA KIPENTEKOSTE TANZANIA
9. Tarehe 11 Februari 2014, Baraza la Maaskofu wa
Kipentekoste Tanzania lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu uteuzi wa
Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba. Baraza liliomba vyombo vya habari lifikishe
masikitiko ya Baraza kwa viongozi na waamini wa Kipentekoste wote na jamii ya
wapenda haki hapa nchini, kutokana na kitendo cha Serikali wanayoiheshimu, wanayoipenda
na kuiombea, kwa kulibagua na kulitenga
Baraza lisihusike na Bunge Maalum la Katiba.
10. Katika Taarifa yake kwa vyombo vya habari, Baraza la
Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania limeeleza kuwa kwa …”utaratibu tuliojiwekea
katika utawala wa Baraza letu, hakuna Kanisa moja, mchungaji binafsi,
mwamini, anaweza kujitwalia heshima, kuchukuliwa au
kupewa haki na chombo chochote cha Serikali katika nchi yetu kwa nia ya
kuwakilisha wapentekoste, bila kupata idhini toka kikao halali cha Kamati Kuu
ya
Utendaji ya PCT-Taifa”.
11. Kwa kuzingatia utaratibu huu “Kamati Kuu ya Utendaji
ya PCT-Taifa katika kikao chake cha tarehe 5/12/2013 ilipendekeza kwa
Mheshimiwa Rais majina ya wajumbe wake iliowaona kuwa wanafaa kuchaguliwa
katika Bunge Maalum la Katiba, lakini cha kusikitisha kati ya hao hakuna jina
la mjumbe hata mmoja ambaye alichaguliwa na Mheshimiwa Rais katika Bunge Maalum
la Katiba”.
12. Taarifa hiyo imeeleza pia, “… Serikali imeona
hatufai na hatuna sifa za kuweza kuchaguliwa katika Bunge Maalum la Katiba, na
badala yake ikaamua kuteua majina ya wajumbe toka katika taasisi nyingine za
kidini zenye hadhi kama yetu za Waislamu, Wakatoliki, Waprotestanti na Wajumbe
wengine binafsi kwa Tanzania Bara na Visiwani na kuwaacha Wapentekoste…”
UFAFANUZI WA SERIKALI
13. Kwanza kabisa, napenda kuwahakikishia watanzania na
hasa wale waliolengwa na taarifa ya Baraza, kwamba Serikali haikuupuzia kundi
lolote lililoanishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuwasilisha
mapendekezo ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Serikali inaliheshimu Baraza
na tunalishukuru sana katika juhudi inazozifanya kwa pamoja na Serikali katika
kuwaendeleza wananchi wa Tanzania.
14. Kutokana na umuhimu wa makundi mbalimbali, jumla ya
makundi 850 yaliwasilisha mapendekezo ya majina 3,636. Katika makundi haya 850,
kulikuwa na mapendekezo kutoka taasisi au makundi ya kidini 72 ambayo
yalipendekeza jumla ya majina 429. Kwa upande wa Tanzania Bara, taasisi za
kidini 55 ziliwasilisha mapendekezo yenye jumla ya majina 344. Aidha Serikali
ilipokea mapendekezo 118 kutoka kwa waliojipendekeza wenyewe! Hivyo, siyo kweli
kuwa Serikali ilipuuza mapendekezo kutoka kundi fulani ikiwa ni pamoja na
Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania. Serikali hii ni kwa ajili ya watu
na makundi yote. Aidha, Katiba yetu haibagui watu au makundi ya watu kwa lengo
la kuwanyima au kuwakosesha haki.
15. Kufuatia taarifa ya Baraza la Maaskofu wa
Kipentekoste Tanzania kwa vyombo vya habari kuwa mapendekezo yao yamepuuzwa,
kwa kuanzia Serikali imefuatilia kama kweli Baraza hilo liliwasilisha
mapendekezo. Kwa kuwa mapendekezo yote yaliyowasilishwa yaliwekwa katika kanzi
data ya msingi (primary data base) kwa ajili ya uchambuzi, utafutaji kwa
kutumia kompyuta (computer search or find) ulifanywa ili kubaini kama kulikuwa
na mapendekezo kutoka Baraza kati ya mapendekezo 850 yaliyowasilishwa.
16. Kwa kuwa hakukuwa na taarifa za majina ya
waliopendekezwa, jina la taasisi na majina ya maaskofu watano (5) walioshiriki
katika utoaji taarifa kwa vyombo vya habari yalitumika katika kubaini kama wao
pia walikuwa miongoni mwa waliopendekezwa. Utafutaji wa huu haukubaini kuwa
Baraza ilikuwa moja ya taasisi zilizowasilisha maombi. Aidha, hapakuwa na jina
hata moja la viongozi wa Baraza walioitisha vyombo vya habari kutoa taarifa.
17. Pamoja na kwamba haikutarajiwa kuwa viongozi wa
taasisi hii kujipendekeza wenyewe, na hivyo kuwa miongoni mwa watu 118
waliojipendekeza wenyewe, juhudi za Serikali zilijielekeza kutafuta endapo
kulikuwa na mapendekezo kundi hili. Hata hivyo, utafutaji haukubaini majina ya
viongozi hawa kuwepo katika orodha hiyo.
18. Kulikuwa na uwezekano pia, Baraza liliwasilisha
mapendekezo ambayo yalifika kwa Katibu Mkuu Kiongozi nje ya muda uliopangwa
kisheria wa tarehe 2 Januari 2014. Uchambuzi wa mapendekezo 52 ambayo
yaliwasilishwa nje ya muda haukubaini kuwepo kwa mapendekezo kutoka Baraza la
Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.
19. Hivyo, juhudi za Serikali katika kufuatilia uwepo wa
mapendekezo kutoka Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania hazikuweza
kuthibitisha kuwa Baraza lilituma mapendekezo yake kama ilivyokuwa imeagizwa na
Sheria ya mabadiliko ya Katiba!
UWAKILISHI WA MADHEHEBU YANAYOUNDA BARAZA LA
MAASKOFU WA KIPENTEKOSTE TANZANIA
20. Kwa kufahamu umuhimu wa makundi mbalimbali ya kidini
ikiwa ni pamoja na Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania unaoundwa na
Maaskofu Wakuu wa madhehebu ya kipentekoste yapatayo 75, uteuzi wa wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba ulihakikisha kuwa makundi ya kidini yanawakilishwa
ipasavyo.
21. Mgawanyo wa idadi ya wajumbe 20 kutokana na makundi
ya kidini baina ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuzingatia uwiano wa moja ya
tatu ya wajumbe kutoka Zanzibar ulimaanisha kuwa katika kundi hili, wajumbe 7
wangekuwa wanatoka Zanzibar na wajumbe 13 wangekuwa wanatoka Tanzania Bara.
Uteuzi wa wajumbe katika kundi hili umezingatia kigezo hiki.
22. Kufuatia uteuzi uliofanywa tarehe 7 Februari 2014,
uchambuzi wa majina ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba umebaini kuwa kati ya
wajumbe 13 kutoka taasisi za kidini wa Tanzania Bara walioteuliwa, mjumbe mmoja
(1) aitwaye Bibi Respa Miguma Adam ameteuliwa kutoka Evangelistic
Assemblies of God Tanzania (EAGT), Patmos Vision,
Kigamboni Church. Evangelistic Assemblies of God Tanzania ni moja ya madhehebu
ambayo maaskofu wake wakuu wanaunda Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste
Tanzania.
23. Hivyo, tamko la Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste
kuwa wanabaguliwa halina ukweli kwa kuwa uchunguzi tulioufanya haujathibitisha
kuwa Baraza lilileta mapendekezo. Ni vyema Baraza likafanyia kazi kwa nini kama
kulikuwa na mapendekezo, hayakufikishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi
(Dar es Salaam) au Katibu Mkuu Kiongozi (Zanzibar).
Ninaamini kabisa kama mapendekezo hayo yangekuwa yamewasilishwa, Mhe. Rais
angechagua mwakilishi kutokana na mapendekezo hayo.
HITIMISHO
24.Uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
uliofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na
Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar tarehe 7
Februari 2014, kwa namna yoyote ile haukuwa na nia ya kulibagua Baraza la
Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.
25. Kuna kila sababu ya kuamini kuwa mapendekezo ya
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste
Tanzania hayakuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kama sheria ilivyohitaji.
26. Pamoja na kuwa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste
Tanzania hawakuweza kuwasilisha mapendekezo yao kama ilivyotakiwa, tunaamini
kuwa Baraza, kama ilivyo kwa wananchi wote, litawakilishwa vyema na wajumbe
walioteuliwa ambao wanajumuisha mjumbe aliyeteuliwa kutoka
moja ya madhehebu yanayounda Baraza la Maaskofu wa
Kipentekoste Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Februari 2014

0 comments:
Post a Comment