Wanawake wameshauriwa kuacha kutumia sabuni za kunawia
sehemu za siri ambazo hudaiwa kurejesha ubikra kwani zina madhara makubwa
ikiwemo kusababisha kansa ya shingo ya kizazi. Mkaguzi wa Dawa na Mfamasia wa
Manispaa ya Dodoma, Daria Mwanuka, alisema hayo mwishoni mwa wiki katika
mahojiano na mwandishi wa habari hizi wakati wa uteketezaji dawa, vipodozi na
vyakula visivyofaa kwa matumizi ya bindamu.
Kazi hiyo ilifanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
Kanda ya Kati. Alisema kumekuwa na sabuni mbalimbali ikiwemo Kaisiki ambapo
wanaoziuza wanadai zimekuwa zikisababisha bikira iliyopotea kurudi, kitu
ambacho si kweli.
“Sabuni hizo zinapunguza tu majimaji sehemu za siri za
mwanamke, jambo ambalo husababisha wakati wa kufanya mapenzi mwanaume kupata
ugumu kwenye muingiliano kwa vile mwili unakuwa umekataliwa kutoa maji na hivyo
kuleta michubuko, kitu ambacho ni hatari hasa wenye maambuzi ya magonjwa,”
alisema.
Alisema michubuko inapotokea ni rahisi mwanamke
kuambukizwa magonjwa ya zinaa, hata virusi vya Ukimwi. Mtaalamu huyo alisema
sabuni hizo zinatengeneza hali fulani ukeni lakini haiwezi kurejesha hali ya
maumbile iliyopotea.
Alisema ni vyema wanawake wakatambua thamani yao na
kuachana na matumizi ya sabuni hizo ambazo hazina manufaa yoyote na badala yake
zimekuwa na madhara makubwa kwao.
Kwa upande wake, Fredrick Luyangi, Mkaguzi wa dawa
kutoka TFDA alisema matumizi ya sabuni hizo huleta athari kubwa mwilini na
wakati mwingine kutengeneza kansa bila mhusika kufahamu.
Alisema sabuni hizo husababisha kansa ya kizazi na
kubainisha sabuni hizo licha ya kupigwa marufuku zimekuwa zikiuzwa kwenye
maduka ya vipodozi.
Alisema mara nyingi kwenye operesheni zinazofanyika
zimekuwa zikiondolewa sokoni lakini hata hivyo zimekuwa zikiingizwa kwa wingi,
hali inayofanya zoezi la kudhibiti kuwa gumu.
Alisema ni muhimu kwa wanawake kuacha matumizi ya sabuni
hizo ambazo zina madhara makubwa sana kwao kwani zikikosa wanunuzi zitaondoka
sokoni.
CHANZO: Habarileo
0 comments:
Post a Comment