![]() |
| Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwa Bungeni mjini Dodoma Jana. |
Julius S. Mtatiro
Tunafahamu kuwa kuna njama zinapangwa ili wajumbe wa
bunge la katiba ati waongezewe fedha zaidi.
Hoja hii imetolewa leo hii na mmoja wa wajumbe huku
ikionekana kuwa maarufu na inayoungwa mkono na baadhi ya wajumbe, hasa wabunge
wa CCM.
Binafsi na wenzangu wengi tumepanga kutumia kila uwezo
kuzuia nia hiyo OVU, ifikie wakati tuambiane ukweli vinginevyo nchi hii watu
watakufa masikini.
Shilingi laki tatu tunazopewa kwa siku zinatosha kabisa,
ambaye hazimtoshi aongeze za kwake, na ambaye anaona hawezi kuongeza zake
aondoke Dodoma ili kupisha wanaoweza kutunga katiba kwa posho ya shs 300,000
waendelee.
Laki tatu tunazopata zinatosha kila kitu na CHENJI
inabaki, zinatosha kula, kulala, kumpa dereva na kuishi Dodoma.
Lazima sisi tunaotunga katiba tufahamu kuwa maisha ya
wananchi ni muhimu na kwamba wana mahitaji yasiyokwisha hata baada ya bunge
hili.
Baadhi yetu tulioko humu bungeni tutakataa jambo hili
kwa maneno na vitendo. Wakipitisha kwa wingi wao tuta-boycott kuzipokea.
Kenya pale mnakumbuka hoja ya wabunge kujiongezea mapesa
ilipingwa vikali na wananchi waliandamana hadi nje ya ukumbi wa bunge. Hapa
Tanzania hata zikiongezwa milioni kila siku hutaona mwananchi anachukua hatua
kwa vitendo, kuoneshwa kutoridhishwa kwake.
Tuna tatizo kubwa sana, sisi viongozi na wananchi wetu.
Kuna mtu anasema, viongozi ni zao la jamii hiyohiyo.
Tuungane pamoja kusimamia jambo hili, ninyi mlioko nje
na sisi tulioko ndani.

0 comments:
Post a Comment