![]() |
| Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta |
Katiba Mpya ya Kenya imeanzisha mambo mengi mapya.
Imeshusha madaraka kwa wananchi na kuwapa madaraka makubwa magavana ya kuamua
mambo mbalimbali.
Kenya ilizindua Katiba mpya Agosti 27 mwaka 2010 kwenye
sherehe iliyojaa mbwembwe katika bustani ya Uhuru, Nairobi.
Hiyo ilikuwa baada ya Wakenya kupiga kura kwa wingi
wakiunga mkono Katiba Mpya. Badala yake katiba imekuwa chungu kwa Wakenya kwa
magavana kuaanzisha ushuru wa aina mbalimbali ikiwemo ushuru wa kuaga maiti.
Inatafsiriwa kuwa, magavana wametumia mamlaka yao
kunyanyasa wananchi katika kaunti.
Katika Kaunti ya Kiambu, inayoongozwa na Gavana William
Kabogo, kuna ushuru mpya unaotozwa kwa
familia iliyopoteza mpendwa ama wapendwa wao.
Hakuna anayekubaliwa kumzika mfu wao bila kulipa ushuru
huo. Pia, huwezi kuchinja mfugo wako nyumbani bila kulipa ushuru!
Katika Kaunti ya Kakamega, Gavana amebuni ushuru wa kuku
ambapo kila mfugaji atalipa Sh20 kwa kila kuku anayemfuga.
Pia, watu wanapoomboleza, lazima walipe ushuru wa
kuomboleza haswa wanapotazama mwili wa marehemu.
Ukiutazama zaidi ya mara mbili, utalipa ushuru zaidi ya
mara moja!
Watu hawajui la kufanya na wana majuto makuu kwa
kukaribisha Katiba mpya 2010. Walipokuwa wanaipitisha walikuwa na matumaini
kwamba ingebadilisha maisha yao kwa kuleta utawala na huduma za Serikali Kuu
karibu yao.
Wakati huo wa mchakato wa Katiba mpya, Makamu wa Rais
William Ruto alikuwa katika upande uliokuwa ukipinga Katiba hiyo.
KUTETEA KATIBA
Hata hivyo, Muungano wa Jubilee ulipochukua hatamu ya
uongozi, Ruto na Uhuru Kenyatta waliapa kuilinda na kuitetea Katiba hiyo.
Katiba ikawa mwanzo wa Serikali mpya iliyoshusha zaidi
madaraka kwa wananchi hadi ngazi ya Kunti, kwa lugha ya Kenya inaitwa Serikali
ya Ugatuzi, ambapo mipaka ya nchi iliyowekwa
wakati wa ukoloni, iligawanywa upya ili
mipaka mipya ya Kaunti 47 iundwe.
Machi 4 mwaka 2013, uchaguzi mkuu ukafanyika na viongozi
mbalimbali wakiwamo magavana wakachaguliwa, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Kenya
kuwa na viongozi wa aina hii.
Sasa Kenya ina magavana 47, baadhi ya watu wanaona kuwa
viongozi hawa wanakuwa kama miungu watu ambao Wakenya hawana budi kumshukuru
Mola kwa sababu yao.
Hali hiyo inatokana na tuhuma za ufisadi zinazowakabili
baadhi magavana, hali iliyowakasirisha Wakenya walio wengi.
Mmoja wa anayekabiliwa na tuhuma hizi ni Martin Wambora
wa Kaunti ya Embu. Kiongozi huyu alipoteza wadhifa wake wiki iliyopita, baada
ya Bunge la Kaunti kupiga kura ya kumwondoa katika wadhifa wa Ugavana.
Wambora alituhumiwa kujihusisha na ufisadi wa hali ya
juu, ambapo Kaunti ilipoteza mamilioni ya fedha
baada ya zabuni ya kununua mbolea na mbegu za mahindi kwenda mrama.
Mbegu za mahindi hazikumea na mbolea haikuwa nzuri, huo
ulikuwa mwanzo wa masahibu ya Wambora yaliyomfikisha mbele ya Kamati ya Seneti
iliyosikiliza kesi yake na kuamua kumfuta kazi. Naibu wake sasa amechukua
nafasi yake na kufanya Kenya kupata gavana wa kwanza mwanamke.
Kufutwa kazi kwa Wambora kulifungua mlango wa Bunge la
Seneti kuonyesha kati ya seneta na
gavana, ni nani mkubwa.
Wakati Seneti ilikuwa ikitoa uamuzi wake kuhusu
hatma ya Wambora, maseneta wawili walisema hawatashiriki kwenye zoezi hilo kwa
sababu mchakato mzima haukufuata haki.
Seneta mmoja aliyeunga mkono kufutwa kazi kwa Wambora,
aliiambia Seneti kuwa, kuanzia sasa magavana watajua ‘ nani kati yao na sisi
ndiye ana uwezo wa kumtimua na kumwadhibu’.
Kwa wadadisi wa kisiasa, hatua ya Seneti kumng’oa
mamlakani gavana huyo, ni jaribio la maseneta kutoa ujumbe kwa magavana
wanaotuhumiwa kuwapuuza viongozi hao haswa katika suala la kupeleka madaraka
kwenye kaunti.
Sasa, Wambora ameenda nyumbani kutafuta kingine cha
kufanya na Seneti inapanua upeo wake ili inase magavana zaidi wanaoshukiwa
kufuja pesa za umma na kubuni sera potofu za kunyonya jasho la wananchi wa
kawaida kwa kuwatoza ushuru.
KUSAMBAZA UFISADI
Ufisadi sasa umesambazwa kutoka Serikali Kuu hadi
Serikali za Mashinani na kufanya maisha kuingia kwenye mkondo mbaya zaidi.
Fedha zilizopaswa kutumwa kutoka kwenye
Serikali Kuu kwenda kwenye kaunti, hazitumiwi ipasavyo.
Badala yake, pesa hizo za maendeleo ya kikaunti
zinafujwa na kuelekezwa kwenye miradi bifasi ya magavana na vibaraka wao.
Ajira katika kaunti ni kama sarakasi kwa sababu magavana
hawazingatii sheria na kanuni zinaoongoza uajiri wa wafanyakazi wa umma.
Magavana wanaajiri jamaa zao wasio na ujuzi au elimu na
kuwaacha wataalamu waliosomea nafasi husika.
Uchunguzi uliofanywa
miezi mitatu iliyopita, unaonyesha kuwa
magavana wametenga mamilioni ya fedha kugharimia safari zao za nchi za
nje haswa Uingereza, Amerika na Ufaransa.
Seneta inanuia sasa kukata ‘pembe’ za magavana wote
na kuna orodha ya majina tisa ya wale
wanaotakiwa kufika mbele ya Kamati ya Seneti kujibu maswali kuhusu matumizi ya
fedha za umma.
MAJIBU YATAKIWA
Magavana hao tisa
wanatakiwa pia kujibu maswali kuhusu ushuru tata walioanzisha katika kaunti
zao.
Anayelengwa zaidi ni Gavana wa Kaunti ya Bomet, Isaac
Ruto aliyekuwa amezoea kumzomea na kumkosoa Makamu wa Rais kwa hili na lile.
Majibizano kati ya hao wawili yalikuwa yakitawala vyombo vya habari.
Gavana Rutto anaonekana kama ‘mwenye kichwa kikubwa’ na
anafaa ‘kurekebishwa’ na Seneti ili afuate mkondo unaotakikana.
Lakini Seneti ina haki ya kuwaadhibu magavana
wanavyopenda? Nguvu hizi za Seneti kuwaadhibu magavana zimetoka wapi?
Kwa muda mrefu, mashindano katika ya maseneta na
magavana kuhusu ‘ukubwa’ yamekuwa yakitawala vyombo vya habari.
Magavana walioandikiwa barua kufika mbele ya Seneti
wanasema maseneta wamekosea kisheria kuwataka wafike mbele yao.
Hatua ya kwanza wanayochukua magavana kujaribu kuwazuia
maseneta kuwaadhibu ni kutuma maombi ya kesi kwa kwa mahakama ya kisheria ili
iamue nani kati yao ni ‘ndume’ ya mwengine.
Mwaka mmoja umeisha tangu Uchaguzi Mkuu umefanyike, lakini kilichodhairi shahiri ni kwamba
maendeleo ya kipekee wanayoyazingatia viongozi waliochaguliwa ni kujipiga kifua
kuonyesha nani ni mkubwa zaidi ya mwenzake.
Hayo yakiendelea, barabara zimezorota, sekta ya afya
imesambaratika na wananchi wamepoteza matumaini, ya kuona siku moja wataishi
maisha yanayofaa na kuachana na ufukura wao wa miaka mingi.
Ufisadi umeota mizizi nchini na ni mzigo kwa maisha ya
wananchi, hawaoni tofauti kati ya vitendo vya maseneta na magavana.
Hii ni kwa kuwa
wengi wao wanashiriki ufisadi. Ni kweli kwamba kama maseneta wangekuwa na
nafasi ambayo magavana wanazo, baadhi yao wangefanya kama vile magavana
walivyofanya kwa kufuja mali za umma na kuendeleza ukabila.
Katiba Mpya ilikuwa inaonekana kama baraka kwa Wakenya,
lakini kwa hakika imeleta shida nyingi na kufanya maisha kuwa magumu zaidi.
Wanaoumia ni wananchi wa kawaida, huku viongozi
wakiendelea kujilimbikizia mali bila kutoa jasho.
Wanaendelea kutajirika huku wananchi wakihangaishwa na
maisha. Mwokozi wao ni nani?
KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment