Vikosi vya usalama nchini Uturuki vimefanikiwa kumtia
nguvuni abiria alijaribu kuiteka ndege iliyolazimishwa kutua mjini Istanbul
usiku wa leo.
Afisa mmoja kutoka wizara ya uchukuzi nchini humo
amekaririwa akisema kuwa wakati wa zoezi hilo hakuna maafa yaliyotokea na
kwamba abiria wote wameondolewa katika ndege.
Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 110 kutoka Ukraine
ililazimishwa na ndege za jeshi la Uturuki kutua katika uwanja wa ndege wa
Sabiha Gokcen mjini Istanbul baada ya kuwepo kwa jaribio la utekaji ambapo
mtekaji huyo alitangaza kuwepo kwa bomu ndani ya ndege na kutaka ielekezwe mjini Sochi nchini Urusi
ambapo michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi inaendelea.
Itakumbukwa kuwa Januari 20 mwaka huu, kundi moja la wanamgambo
Kaskazini mwa Urusi lilitishia kufanya mashambulizi dhidi ya michezo hiyo ya Olimpiki.
Katika mkanda wa video uliorushwa mtandaoni, kundi hilo
lilimuonya Rais wa Urusi Vladimir Putin asikaribishe michezo hiyo, likisema kuwa
wale watakokwenda Sochi wangepokelewa kwa “matukio ya kushtukiza.”
Wanamgambo hao waliojitokeza katika video hiyo, walidai
pia kuhusika na mashambulizi pacha ya mabomu katika kituo kimoja cha treni na
katika basi moja la abiria katika mji wa kusini wa Volgograd mwezi Desemba,
ambapo watu zaidi ya 30 walipoteza maisha.
Hata hivyo, Rais Putin aliahidi kuhakikisha amani na
usalama wakati wa michezo hiyo inayofanyika katika mji huo ulio kandokando mwa
pwani ya Bahari Nyeusi.
“Kama waandaaji wa wa mashindano haya, tunawajibika
kutoa dhamana ya usalama wa wanamichezo na wageni wa michezo hii ya Olimpiki na
tutafanya kila liwezekanalo kufikia lengo hili,” alisema Putin alipotembelea
mji huo wa Sochi mwezi jana.
Putin alifanya ziara mjini Sochi siku moja baada ya
kufanya mkutano na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao mjini Moscow ambapo aliwaambia
kuwa mashindano hayo yangefanyika bila ubaguzi wowote dhidi ya wanamichezo na
wageni.
Michezo ya Olimpiki Majira ya Baridi imeanza rasmi Februari
7 mpaka 23, na kwa mara ya kwanza katika historia ya michezo hiyo, wageni
wataweza kusafiri kwenye mji mwenyeji bila visa.
Hata hivyo, vitisho dhidi ya mashindano hayo
vimeongezeka licha ya hakikisho hilo lililotolewa na Rais Putin.

0 comments:
Post a Comment