![]() |
| Watoto nchini Afghanistan wakienda shule |
Umoja wa Mataifa umesema kuwa idadi ya watoto waliouawa
na kujeruhiwa katika vita nchini Afghanistan mwaka 2013 imeongezeka kwa
asilimia 34.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA) umesema
katika ripoti yake ya kila mwaka iliyotolewa leo kuwa raia 2,959 waliuawa
nchini humo mwaka jana, wakiwemo watoto 561 na wanawake 235.
UNAMA imeongeza kusema kuwa zaidi ya watu 5,600,
wakiwemo watoto 1,195 na wanawake 511 walijeruhiwa mwaka 2013.
“Ni uhalisia ulio wazi kuwa wanawake wengi na watoto
wameuawa na kujeruhiwa katika maisha yao ya kila siku – wanapokuwa nyumbani,
wanapokuwa njiani kwenda shule, wanapofanya kazi mashambani au wanaposafiri
kwenda kwenye shughuli ya kijamii,” amesema mkurugenzi wa haki za binadamu
katika shirika hilo, Georgette Gagnon.
Ripoti hiyo imeongeza kusema kuwa hali jumla ya maafa ya
raia imepaa kwa asilimia 14 mwaka 2013 ikilinganishwa na raia 2,768 waliouawa
na wengine 4,821 waliojeruhiwa mwaka 2012.
UNAMA imekitupia kikundi cha Taleban lawama ya kuhusika
na asilimia 75 ya vifo vya raia. Lakini kundi hilo limekana ripoti hiyo na
kutupilia mbali madai ya kuhusika na
vifo hivyo na kusema kuwa wao hawalengi raia katika mashambulizi yao.
Mabomu yanayotegwa kandokando ya barabara ndiyo yanayoua
raia wengi na kusababisha asilimia 34 ya vifo na majeruhi mwaka uliopita,
imesema ripoti hiyo.
Juma la vifo na majeruhi 8,615 kwa mwaka 2013 ndio idadi
kubwa kabisa kuwa kuripotiwa tangu Umoja wa Mataifa ulipoanza utaratibu wa
ukusanyaji wa ripoti hizo mwaka 2009.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2001 majeshi ya kigeni,
yakiongozwa na Marekani, yaliivamia Afghanistan katika kile kilichoelezwa kuwa
ni operesheni dhidi ya ugaidi. Uvamizi huo ulishuhudia kikundi cha Taliban
kikiondoka madarakani, lakini nchi hiyo imeendelea kuwa katika hali tete ya
ukosefu wa usalama.
Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai, katika mahojiano
aliyoyafanya hivi karibuni na gazeti la Sunday Times, alisema kuwa hafurahishwi
na uwepo wa vikosi vya kigeni nchini mwake, akiongeza kuwa, “kwa miaka yote 12
nimekuwa nikitoa ombi kuu la kuwataka Wamarekani wauchukulie uhai wa raia wetu
kama uhai wa watu.”
Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi ya ndege
zisizokuwa na rubani kwa hoja kuwa mashambulizi hayo yanawalenga wanamgambo,
hata hivyo ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa mara nyingi raia wa kawaida
wamekuwa waathirika wa mashambulizi hayo.

0 comments:
Post a Comment