![]() |
| Jenerali Leonardo Barrero. |
Rais wa Colombia, Juan Manuel Santos, amemfuta kazi mkuu
wa majeshi wa nchi hiyo kwa matamshi ya kuishushia hadhi mahakama.
Jana Rais Santos alisema kuwa Jenerali Leonardo Barrero alikuwa
amefutwa kazi kutokana na kauli yake ya utovu wa heshima dhidi ya mahakama na taifa
kwa ujumla katika mazungumzo ya simu yaliyochapishwa mwishoni mwa wiki.
Tuhuma hizo zilichapishwa na jarida la Semana la nchini
humo. Matamshi ya Barrero yalinaswa kwa siri wakati akizungumza na simu kuhusu
upelelezi wa tuhuma za ufisadi uliokuwa ukifanywa na waendesha mashitaka.
Barrero alisikika akiwatukana waendesha mashitaka wakati
akizungumza na kanali mmoja juu ya uwezekano wa kuhusika na mauaji ya kiholela.
Barrero alimwambia kanali Robinson Gonzalez del Rio, ambaye
anakabiliwa na mashitaka ya jinai ya mauaji ya watu wawili mwaka 2007, kwamba waendesha
mashitaka wanaochughuza mauaji hayo ni “kundi la wapuuzi” na kushauri kuwa yeye
na wenzake “watengeneze mpango” wa kuwadhoofisha.
Baadhi ya maofisa wa jeshi wanatuhumiwa kuchukua hongo
ya mpaka asilimia 50 ya mikataba, wengine wanatuhumiwa kuhamisha fedha
zilizopangwa kutumika kwa ajili ya kambi na ugavi wa zana za jeshi.
Kwa mujibu wa ripoti ya jarida hilo la Semana, baadhi ya
pesa zilipelekwa kwenye mifuko ya maafisa wanaotuhumiwa kufanya mauaji ya
kiholela.
Serikali ya nchi hiyo imetangaza kuwa mnadhimu wa jeshi,
Jenerali Juan Pablo Rodriguez, atachukua nafasi ya Barrero.
Tukio hilo limekuja wiki mbili baada ya baadhi ya vyombo
vya habari kufichua kuwa kuna baadhi ya maafisa wamekuwa wakiwafanyia ujasusi
wasuluhishi wa mazungumzo ya amani baina ya serikali na waaasi wa FARC.
Jeshi la Colombia limekuwa likipambana na waasi hao kwa
miongo mitano sasa.

0 comments:
Post a Comment