![]() |
| Askari wa Seleka |
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa kwa uchache
watu 300 wameuawa katika ghasia zinazoendelea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
tangu alhamisi.
Shirika hilo la kimataifa la misaada ya kiutu limesema
kuwa limekusanya miili 281 ya watu waliouawa wakati wa siku mbili za ghasia
katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui.
Kiongozi wa Shirika hilo, Antoine Mbao Bogo, ameonya kuwa
idadi ya vifo natarajiwa kuongezeka wakati wafanyakazi wa shirika hilo
watakapoendelea na kazi ya kukusanya miili leo Jumamosi.
Wakati hali ikiwa hivyo, juzi Alhamisi, Ufaransa
ilitangaza kuwa itatuma askari nchini humo.
Rais Francois Hollande alitoa tangazo hilo muda mfupi
baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kutuma
vikosi kwenda kudhibiti hali nchini humo.
Baraza hilo lenye wanachama 15 lilipitisha kwa kauli
moja azimio linalovipa vikosi ya Umoja wa Afrika na vile vya Ufaransa idhini ya
kwenda nchini humo. Kwa mujibu wa azimio hilo, askari wapatao 3,600 wa Umoja wa
Afrika na 1,200 wa Ufaransa wameruhusiwa kwenda kudhibiti ghasia zinazoendelea
kupoteza maisha ya watu.
Hollande aliahidi kuwa askari 600 wa Ufaransa ambao
tayari wapo Jamhuri ya Afrika ya Kati wataongezwa mara dufu ndani ya siku
kadhaa au hata saa kadhaa, akisema kuwa nchi hiyo imeiomba Ufaransa msaada wa
kuingilia kati naye ameamua kuitikia ombi hilo bila kuchelewa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nicolas
Tiangaye, ambaye alikuwa Paris katika
kilele cha Mkutano wa Ufaransa na Mataifa ya Afrika, aliitaka Ufaransa kuchukua
hatua za haraka.
“Kutokana na dharura, ninatamani uingiliaji kati ufanyike
mapema iwezekanavyo, mara tu baada ya azimio,” alisema Tiangaye.
Mnamo Novemba 21, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent
Fabius aliielezea Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa ni nchi iliyo katika ukingo wa
kuangukia katika mauaji ya kimbari, akisema kuwa Ufaransa, majirani wa Jamhuri
ya Afrika ya Kati na jumuiya ya kimataifa wana wasiwasi juu ya machafuko nchini
humo.
Jamhuri ya Afrika ya Kati iliingia katika machafuko
baada ya muungano wa waasi ujulikanao kama Seleka, kuanzisha mashambulizi dhidi
ya rekali mwezi Desemba 2012 na hatimaye mwezi Machi wakafanikiwa kumng’oa
madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Francois Bozizé. Waasi hao wamekuwa
wakishutumiwa kwa mauaji, unyang’anyi na ubakaji nchini humo.
Septemba 13, rais wa nchi hiyo, Michel Djotodia,
aliuvunja muungano wa Seleka uliomuingiza madarakani. Baadhi ya waasi waliingia
katika jeshi rasmi la serikali huku wengine wakiachwa.
Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inawashutumu
waasi wa Seleka kwa ghasia nchini humo, ikisema kuwa waasi hao pamoja na
makundi mengine yenye silaha wafanya vitendo vya ubakaji, unyang’anyo,
udhalilishaji wa wanawake na watoto, kufanya mauaji, kutoa mafunzo ya kijeshi
kwa watoto na kufanya mashambulizi na hujuma mbalimbali.
Mwezi Julai, Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu
lilisema kuwa tokea mwezi Machi kwa
uchache mauaji 400 yanayohusishwa na kikundi cha Seleka yalikuwa yamesajiliwa.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ina utajiri mkubwa wa
rasilimali za madini kama vile dhahabu na almasi. Hata hivyo, nchi hiyo imekuwa
ikikabiliwa na mfululizo wa matukio ya uasi na mapindzui tangu ilipojipatia
uhuru wake mwaka 1960 kutoka kwa Ufaransa.

0 comments:
Post a Comment