Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameungana na viongozi
mbalimbali dunia kuomboleza kifo cha shujaa wa mapambano ya siasa za ubaguzi wa
rangi na rais wa zamani wa Afrika Kusini, mzee Nelson Mandela aliyefariki jana
usiku.
Katika salamu zake za rambirambi kwa rais wa Afrika
Kusini Jacob Zuma na Mke wa Mandela Bi.Graca Machel rais Jakaya Kikwete
amemtumia Salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na kupitia
kwake, kwa mkewe Bi. Graca Machel, rais Kikwete amesema msiba huu kuwa ni msiba
mkubwa kwa Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri
na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na 21.
Amesema Afrika Kusini imempoteza kiongozi shupavu,
jasiri, mwana mapinduzi , mvumilivu na mstahimilivu.
Amesema Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina yake kwa
wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo uliomuwezesha
kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini kuwa taifa moja baada ya kipindi
kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. .
Aidha, Rais Kikwete ametangaza maombolez ya siku 3
kuanzia leo hadi Desemba 8 kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa kwanza mzalendo
wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela.
Sambamba na hilo bendera itapepea nusu mlingoti ka siku
zote tatu za maombolezo.
Usiku wa jana, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alitangaza
kifo cha mzee Mandela akisema kuwa taifa hilo limempoteza mmoja wanataifa
wakubwa kabisa.
"Mapambano yake ya kupigania uhuru bila kuchoka
yalimpatia heshima kubwa ulimwenguni. Unyenyekevu wake, huruma yake na utu wake
viliwafanya watu wampende,” alisema Zuma.
RAIS OBAMA
Rais wa Marekani, Barack Obama alielezea huzuni yake
kuhusu kifo cha Mandela, na kumuelezea kuwa alikuwa “mtu mwenye nguvu, jasiri
na mwenye ushawishi ambaye kila mtu angependa kuishi naye, na kwamba alipata
mafanikio ambayo kila mtu angetamani kuyapata. Leo amerejea nyumbani.”
Obama alionegeza kuwa, “sas sio mtu wetu tena;
ameondoka.”
CLINTON
Rais mstaafu wa Marekani ameungana na viongozi wengine
kuomboleza kifo cha Mandela na kumuelezea kama “shujaa wa utu na uhuru wa
mwanadamu.”
"Leo dunia imempoteza mmoja wa viongozi wake muhimu
kabisa na mmoja wa watu wazuri kabisa,” alisema Clinton.
"Historia itamkumbuka Nelson Mandela kama shujaa wa
utu na uhuru wa binadamu, shujaa wa amani na maridhiano. Tutamkumbuka kama mtu
aliyekuwa na huruma isiyokuwa ya kawaida, aambaye kuukabili uchungu na
changamoto mbalimbali haikuwa tu mbinu yake ya kisiasa bali ilikuwa mfumo wa
maisha yake,” aliongeza.
RAIS WA BRAZIL
Naye Rais wa Brazil, Dilma Rousseff, amemuelezea Mandela
kama mfano kwa wale wanaopigania haki na amani. “Mfano wa kiongozi huyu mkubwa
utakuwa muongozo kwa wale wote wenye kupigania haki ya kijamii na amani
duniani.” Alisema Rais Dilma.
IRAN
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Jawad Zarif aliandika
katika ukurasa wake wa twitter:
“Wairan tunaungana na wananchi wa Afrika Kusini
kuomboleza kifo cha Nelson Mandela ambaye amewahamasisha wanadamu kwa ujasiri
na huruma,” alisema Zarif.
UFARANSA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius,
ametoa salamu zake za rambirambi kwa Mandela, akimuelezea kuwa "mtu
aliyekuwa na karisma.”
"Kwa kifo cha Nelson Mandela, baba wa Afrika
Kusini, nguvu ya uhuru na maridhiano imekufa,” alisema Fabius.
UINGEREZA
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron amesema kuwa “nuru
adhimu imezimika ulimwenguni. Nelson Mandela alikuwa mtu mtu adhimu katika zama
zetu; shujaa katika uhai na sasa shujaa katika mauti—shujaa wa kweli wa dunia.”
AUSTRALIA
Naye Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott, amemsifu Mandela
kama “shujaa wa kweli,” akisema kuwa, "Nelson Mandela miongoni mwa
viongozi wakubwa kabisa wa bara la Afrika, na kwa kweli alikuwa mmoja wa
viongozi wakubwa kabisa wa karne iliyopita.”
"Wakati dunia inaweza isimuone tena Nelson Mandela
mwengine, amekuwa hamasa ya wanaume na wanawake wengi duniani kote aliyewafanya
waishi maisha ya ujasiri na uaminifu,” aliongeza Abbott.
UJERUMANI
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema, "mfano
angavu wa Nelson Mandela na athari yake ya kisiasa ya kutotumia vurugu na
kuzilaani aina zote za ubaguzi wa rangi vitaendelea kuwapa hamasa watu
ulimwenguni kote kwa miaka mingi ijayo.”
MEXICO
Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto amesema kuwa, "binadamu
wamempoteza shujaa asiyechoka kupigania amani, uhuru na usawa.”
ASKOFU DESMOND TUTU
Naye askofu Desmond Tutu ameomboleza kifo cha Mandela, akimuelezea
kama “mfano wa utangamano, mfano wa maridhiano, mfano wa uongozi katika
kuwahudumia watu.”
"Kwa hakika, alikuwa mtu wa aina yake, lakini moyo
wa ukuu aliokuwa nao unaishi pamoja nasi sote,” aliongeza.
UMOJA WA MATAIFA
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema, “ni
kwa sababu tu ya mtu adhimu kama Nelson Mandela imewezekana kwa watu Afrika na
kwengineko kufurahia uhuru na heshima ya utu. Tunapaswa kujifunza hekima, azma
na uwajibikaji wa Mandela ili kuifanya dunia kuwa sehemu bora kwa ajili ya watu
wote.”
Mandela, ambaye aliongoza mapambano dhidi ya utawala wa
weupe wachache katika miaka ya 1990 baada ya kukaa karibu miongo mitatu
gerezani, alikuwa miongoni mwa wanasiasa wakubwa kabisa wa karne ya 20.
Baada ya miaka kadhaa ya harakati za mapambano dhidi ya
utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, Mandela alikamatwa mwaka 1962.
Alihukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, ambapo alitumikia miaka 27
tu, ambayo sehemu kubwa aliitumikia katika gereza katika Kisiwa cha Robben
nchini humo.
Baada ya kuachiwa huru kutoka gerezani Februari 11,
1990, Mandela alikiongoza chama cha African National Congress (ANC) katika
mazungumzo yaliyopelekea kufanyika kwa uchaguzi wa kidemkrasia uliowajumuisha
watu wote ambao ulifanyika mwaka 1994. Akiwa kama rais, kipaumbele chake
kikubwa alikiweka katika utangamano na maridhiano. Alistaafu mwaka 1999 baada
ya kutumikia kipindi kimoja tu cha urais.
Nchini Afrika Kusini, Mzee Mandela anajulikana sana kwa
jina la ukoo la Madiba, au tata, yaani baba.
Mandela amepokea zaidi ya tuzo 250 ndani ya miongo
minne, ikiwemo Tuzo ya Amani ya Nobel aliyoipata mwaka 1993.
Mwaka 2004, mzee Mandela alitangaza kuacha kujihusisha
na shughuli za umma lakini akaendelea kuonekana katika matukio machache sana.
Endelea kufuatilia hapa hapa Mzizima 24..
www.mzizima24.com

0 comments:
Post a Comment