
Waandamanaji wanaoipinga serikali nchini Thailand
wameendelea kumshinikiza Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Yingluck Shinawatra, wakisema
anatakiwa kushitakiwa kwa uhaini.
Waandamanaji hao wanasema kuwa wanataka kufuta kabisa
nyayo za kaka wa kiongozi huyo, Thaksin Shinawatra, ambaye aliwahi kuwa Waziri
Mkuu wa nchi hiyo na kuondolewa katika mapinduzi ya mwaka 2006. Wanadai kuwa
bilionea huyo bado anaiendesha nchi kwa mlango wa nyuma.
Haya yanatokea baada ya Bi. Yingluck kuitisha uchaguzi
wa mapema na kutangaza kulivunja bunge katika kujaribu kutuliza hali ya mambo
nchini mwake.
Juzi kiongozi wa waandamanaji, Suthep Thaugsuban, ambaye
alijiuzulu ubunge ili kuongoza maandamano, alimpa Yingluck saa 24 awe
amejiuzulu.
Jana Suthep alisema kuwa polisi walitakiwa kumkamata Yingluck
kwa kuwa muda wa saa 24 ulikuwa umekwisha.
"Ninawataka polisi wamakamate Yingluck kwa uhaini
kwa sababu hajatekeleza maagizo yetu,” aliwaambia maelfu ya waandamanaji
walioweka kambi nje ya jengo la serikali.
"Kama hutatusikiliza, tutazidisha maandamano mpaka
wewe na familia yote ya Shinawatra mshindwe kutembea. Mtawezaje kutembea wakati
watu wakiwatemea mate kila siku?” aliongeza.
Hata hivyo, Yingluck, alipuuza wito wa waandamanaji wa
kumtaka ajiuzulu, akiapa kuendelea kuwa waziri mkuu wa mpito mpaka uchaguzi
mkuu utakaofanyika Februari 2.
Maandamano ya kuipingia serikali yalianza Oktoba 31
baada ya serikali kuwasilisha bunge muswada ambao ungetoa msamaha kwa Thaksin
na kumuwezesha kurejea nchini.
Waandamanaji wanamtuhumu Thaksin kuwa bado anaiendesha
nchi kwa mlango wa nyuma, na wameapa kuibomoa nguvu yake katika siasa za nchi
hiyo.
Bilionea huyo aliyeondolewa madarakani katika mapinduzi
ya mwaka 2006, amekuwa akiishi uhamishoni tangu mwaka 2008. Mahakama nchini
humo ilimpa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela iwapo atarejea Thailand.
0 comments:
Post a Comment