TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Baada ya kupokea barua yake ya mashtaka 11 tarehe 01/12/2013
ambayo anashitakiwa nayo na iliyomtaka ajitetee kwa maandishi.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe (MB) jana tarehe
10/12/2013 amefanya hivyo kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji za Chama
Pia Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe (MB) ametoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Chama
kumueleza nia yake kukata rufaa Baraza Kuu la Chama kupinga hatua
iliyochukuliwa na Kamati Kuu dhidi yake kumvua nyadhifa zake ndani ya Chama.
Kuna sababu mbili za msingi za kukata rufaa;
1. Utaratibu wa kuchukua hatua za nidhamu ulikiukwa.
2. Sababu za kuchukuliwa hatua hizo sio sahihi.
Utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa kabla ya kumchukulia
hatua za kinidhamu kiongozi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji ni
kama ifuatavyo;
Kanuni ya Uendeshaji 6.5.6 inasema;
Kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu bila
kwanza kupewa mashitaka yake kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi
ya kujibu mashitaka kwa maandishi.
Pia tunapenda ijulikane kwamba Kanuni ya Uendeshaji
6.5.2 (a), (b), (c) na (d) kama ilivyorekebiswa Januari 2013 inasema; Kwa
mujibu wa ibara ya 5.4.3 na 5.4.4 ya Katiba mwanachama yeyote hatachukuliwa
hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila
kwanza;
a) Kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa
kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.
b) Kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao
kinachohusika.
c) Mwanachama atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao
mnamo wiki mbili baada ya kusikilizwa.
d) Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila
kuzingatia utaratibu (b), (c) hapo juu kama itaona maslahi ya Chama kwa ujumla
yanaweza kuathiriwa isipokuwa mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa
atalazimika kuitwa kwenye kikao husika.
Naomba nichukue fursa hii kufafanua kuwa uongozi wa
chama ulifanya mkutano na waandishi mnamo tarehe 26/11/2013 na kusema kwamba
marekebisho haya ya Kanuni ya mwaka 2013 ambayo nimewawekea hapo juu, ndiyo
utaratibu waliofuata.
Pia walieleza kuwa sikuwa naifahamu na nilidanganywa
kwani Kanuni ilishabadilishwa.
Mabadiliko haya ambayo ni katika kipengele (d) kuhusu
hatua ya dharura iliyochukuliwa na Kamati Kuu haikugusa kipengele (a) cha
Kanuni. Yaani ni kuwa hata kama Kamati kuu itachukua hatua ya dharura kwa
mujibu wa kipengele (d), bado kipengele (a) ni lazima ifuatwe na inatamka wazi
sharti la kiongozi kupewa mashtaka kwa maandishi na kupewa nafasi ya kujibu kwa
maandishi. Hii ni haki ya msingi kwa kila utawala au uongozi.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe hakupewa mashtaka yake
aliyakuta ndani ya kikao baada ya kupewa taarifa kwa ujumbe wa simu (text
message au sms).
Kwa uzito wa makosa hayo yaliyosababisha kuvuliwa
uongozi na kwa kuangalia athari zake kwake yeye binafsi na chama kwa ujumla,
Kamati Kuu ilitakiwa kujiridhisha kwamba Kanuni za Uendeshaji na Katiba
zinafuatwa.
Hili linaendana na utaratibu uliotumika kwa Samson
Mwigamba kuvuliwa nyadhifa yake ya uenyekiti wa mkoa. Yeye hakuitwa kabisa
kwenye kikao hicho na ni ukiukwaji wa Kanuni ya Uendeshaji 6.5.6(d) niliyoisoma
hapo juu kwamba lazima kiongozi huyo aitwe kwenye kikao.
Sababu zilizotumika ingawaje hajapokea taarifa rasmi ya
maandishi kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji ni kwamba yeye ameshirki kwenye
kuandaa na kusambaza waraka ambao unasemekana ni mkakati wa ushindi wenye lengo
la kupindua uongozi uliopo.
Waraka huo haukumtaja Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kama
muandaaji au msambazaji. Waliouandaa hawajaukana na badala yake wamesema
waziwazi kabisa kwa maneno na maandishi kwamba Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe
HAHUSIKI.
Sio sawa kumuadhibu Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe kwa
hisia au tu kwa sababu ya urafiki wake na watu fulani. Haya ni mapungufu ambayo
kwa bahati nzuri Katiba na Kanuni za Uendeshaji zinatoa nafasi ya kurekebishwa
kwa kutoa nafasi ya kukata rufaa. Na utaratibu ni huu hapa;
Kwa ufupi, Ibara 6.3.6(d) ya Katiba ya Chama;
“Kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka
yake ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake ya
nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho”.
Ibara 6.3.6(e) ya Katiba ya Chama;
“Rufaa yoyote lazima ifanyike katika muda wa siku
thelathini tangu tarehe ya kupokea rasmi kwa maandishi maamuzi ya mamlaka
iliyotoa adhabu”.
Kanuni za Uendeshaji zinatoa UTARATIBU ambao unatakiwa
ufuatwe ili kiongozi aliyeadhibiwa aweze kutumia HAKI yake ya kukata rufani kwa
maneno haya;
Kanuni ya 6.5.8 ya Kanuni za Uendeshaji;
“Kiongozi aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi wa
maamuzi ya mamlaka ya nidhamu ili kumuwezesha kuamua kukata rufani au la”
Kanuni ya 6.5.9 ya Kanuni za Uendeshaji;
“Mwadhibiwa atakayeamua kukata rufani atatakiwa kufanya
hivyo katika muda wa siku thelathini baada ya kuarifiwa uamuzi wa adhabu”
Kanuni ya 6.5.10 ya Kanuni za Uendeshaji;
“Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa
taarifa kamili ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu. Taarifa hiyo
lazima ifike katika muda wa siku kumi na nne baada ya kikao cha mamuzi”
Mpaka hivi sasa hatujapokea taarifa kamili ya mwenendo
wa shauri tokea kikao cha Kamati Kuu cha tarehe 20-21/11/2013 Huo ndio
utaratibu ambao Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe ameamua kufuata kwa kuheshimu
maamuzi ya Kamati Kuu lakini kukatia rufaa maamuzi hayo. Kuheshimu maamuzi sio
kuyakubali uhalali wake.
Kumekuwa na matukio ya kusikitisha ambayo mengine
yamefikia mahali kuwa fujo na vurugu ikiwa ni pamoja na kurushiwa mawe Katibu
Mkuu wa Chama. Vurugu hizo baadhi zimehusishwa na Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe
na baadhi ya watu.
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe hahusiki kwa njia yoyote
na hayo yanayoendelea na anayakemea na kuwashauriwanachama wote kuwa watulivu
na kuendelea kuwaheshimuviongozi wa kitaifa. Hatua zimeshachukuliwa kukata
rufaa na niimani yake kwamba Baraza Kuu la Chama litatenda haki kwakupitia
rufaa yake na kutoa uamuzi.
Nawashukuru wote.
ALBERT MSANDO,
Mwanasheria
11/12/2013

0 comments:
Post a Comment