
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini usiku huu ametangaza
kuwa shujaa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na rais mstaafu wa nchi
hiyo, Mzee Nelson Mandela amefariki dunia.
Katika taarifa yake yenye huzuni katika televisheni ya
taifa ya nchi hiyo, Rais Zuma aliyejawa na majonzi ametangaza kuwa mzee Mandela
“amefariki kwa amani.” Amesema kuwa taifa lake limempoteza mmoja wazalendo wake
wakubwa kabisa.
Mandela, ambaye aliongoza mapambano dhidi ya utawala wa
weupe wachache katika miaka ya 1990 baada ya kukaa karibu miongo mitatu
gerezani, alikuwa miongoni mwa wanasiasa wakubwa kabisa wa karne ya 20.
"Wananchi wamempoteza baba. Ingawa tulijua kwamba
siku hii itafika, hakuna kinachoweza kuiondosha msiba huu mkubwa tulioupata,”
alisema Zuma.
"Mapambano yake ya kupigania uhuru bila kuchoka
yalimpatia heshima kubwa ulimwenguni. Unyenyekevu wake, huruma yake na utu wake
viliwafanya watu wampende. Fikra na sala zetu ziko pamoja na familia ya
Mandela. Hakika tuna deni la kuwashukuru. Fikra zetu ziko pamoja na mkewe,
mkewe wa zamani, watoto wake, wajukuu wake, vitukuu na familia yote,” aliongeza.
Mandela alikuwa akipatiwa matibabu nyumbani kwake
kutokana na maambukizi katika mapafu yake baada ya kukaa hospitali kwa muda wa
miezi mitatu. Alikuwa akisumbuliwa na tatizo la upumuaji, ambalo yamkini
lilitokana na taathira aliyoipata wakati akiwa gerezani.
"Fikra zetu ziko pamoja na mamilioni ya watu
ulimwenguni kote ambao walimchukulia Nelson Mandela kama sehemu ya maisha yao
na ambao waliyaona mapambano yake kama mapambano yao. Hiki ni kipindi cha msiba
mkubwa kabisa,” alisema Rais Zuma katika taarifa yake.
"Ni wazi kuwa kilichomfanya Nelson Mandela kuwa mtu
mkubwa ni kile kilichomfanya kuwa na utu. Ndani mwake tunaziona sifa ambazo
tungependa kuwa nazo,” alisema Zuma.
Mandela alikuwa rais wa Afrika ya Kusini kuanzia mwaka
1994 mpaka 1999, na ndiye rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa katika
uchaguzi wenye demokrasia shirikishi iliyowahusisha watu wote wa nchi hiyo.
Baada ya miaka kadhaa ya harakati za mapambano dhidi ya
utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, Mandela alikamatwa mwaka 1962. Alihukumiwa
adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, ambapo alitumikia miaka 27 tu, ambayo
sehemu kubwa aliitumikia katika gereza katika Kisiwa cha Robben nchini humo.
Baada ya kuachiwa huru kutoka gerezani Februari 11,
1990, Mandela alikiongoza chama cha African National Congress (ANC) katika
mazungumzo yaliyopelekea kufanyika kwa uchaguzi wa kidemkrasia uliowajumuisha
watu wote ambao ulifanyika mwaka 1994. Akiwa kama rais, kipaumbele chake
kikubwa alikiweka katika utangamano na maridhiano. Alistaafu mwaka 1999 baada
ya kutumikia kipindi kimoja tu cha urais.
Nchini Afrika Kusini, Mzee Mandela anajulikana sana kwa
jina la ukoo la Madiba, au tata, yaani baba.
Mandela amepokea zaidi ya tuzo 250 ndani ya miongo
minne, ikiwemo Tuzo ya Amani ya Nobel aliyoipata mwaka 1993.
Mwaka 2004, mzee Mandela alitangaza kuacha kujihusisha
na shughuli za umma lakini akaendelea kuonekana katika matukio machache sana.
Taarifa zaidi zitaendelea kukujia hapa hapa Mzizima 24..
0 comments:
Post a Comment