![]()  | 
| Waziri Mkuu wa Somalia Abdi Farah Shirdon | 
Bunge nchini Somalia limepitisha kura ya kutokuwa na
imani na Waziri Mkuu, Abdi Farah Shirdon, kufuatia miezi kdhaa ya mgogoro baina
ya waziri mkuu na rais wa nchi hiyo.
Jumla ya wabunge 184 kati ya 250 waliohudhuria walipiga
kura ya kumuondoa wakiilaumu serikali yake iliyoingia madarakani mwaka mmoja
uliopita kuwa ni dhaifu.
Waziri Mkuu huyo amekuwa na mgogoro na Rais Hassan
Sheikh Mohamoud kuhusu kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri, jambo
lililosababisha kupigwa kwa kura hiyo ya kutokuwa na imani naye.
Wabunge wanalituhumu baraza la mawaziri kuwa limeshindwa
kuongoza nchi na kwamba serikali iliyong’olewa ilikuwa dhaifu.
Kabla ya kura hiyo, waziri mkuu alisema kuwa mgogoro
baina yake na rais ulikuwa wa kikatiba na ulihitajika kuamuliwa na wabunge.
Hata hivyo, rais alisema kuwa hakutaka Waziri Mkuu huyo
ajiuzulu licha ya mkwamo huo wa kisiasa uliodumu kwa miezi kadhaa.
Wataalamu wanasema kuwa itachukua miezi kadhaa kabla ya
kuteuliwa kwa baraza jipya la mawaziri na kisha kupitishwa na bunge.
Somalia imekuwa bila serikali kuu yenye nguvu tangu
mwaka 1991, baada ya wababe wa vita kumuondosha aliyekuwa rais wa wakati huo, Mohamed
Siad Barre.

0 comments:
Post a Comment