![]()  | 
| kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali, Amadou Sanogo –katikati- akiwasili katika uwanja wa ndege wa Bamako | 
Miili 21 imepatikana katika kaburi la pamoja katika mji
wa Diago karibu na mji mkuu wa Mali, Bamako, kufuatia kukamatwa kwa kiongozi wa
mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana.
Miili hiyo inayoaminika kuwa ya askari watiifu kwa rais
aliyeondolewa madarakani, Amadou Toumani Touré, imepatikana usiku wa kuamkia
leo.
Afisa mmoja wa usalama nchini humo amethibitisha taarifa
hizo na kusema kuwa vitambulisho vilivyopatikana katika kaburi hilo vinaonesha
kuwa ni kikosi maalumu cha askari wa jeshi la nchi hiyo.
 Tukio hilo
limetokea wiki moja baada ya kiongozi wa mapinduzi ya mwaka 2012 dhidi ya rais Touré,
Amadou Haya Sanogo, pamoja na watu wengine kumi na tano, wengi wakiwa askari na
wapambe wake, kukamatwa hivi karibuni.
Rais wa zamani wa nchi hiyo, Amadou Toumani Touré,
aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Machi 22,
2012, na kuitumbukiza nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika mzozo uliolifanya
kundi la waasi wa Kituareg lenye mafungamano na al-Qaeda kulidhibiti eneo lote
la upande wa kasikazini mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa serikali ya Mali, Sanogo ameshitakiwa kwa
makosa ya kuteka na kuua.
Kufuatia kuongezeka kwa uasi nchi humo, mwezi Januari Ufaransa
iliamua kuingilia kati kijeshi katika koloni lake hilo la zamani ikionesha
wasiwasi dhidi ya kuongezeka kwa ushawishi na nguvu za wapiganaji kaskazini mwa
nchi hiyo na kuongezeka kwa uasi wa Kituareg wanaotaka kujitenga kwa eneo hilo
kiasi cha kutishia kuanguka kwa serikali. 
Mwezi Februari, shirika la Amnesty International lilielezea
kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo, ikiwa ni pamoja na kuuawa
kwa watoto.

0 comments:
Post a Comment