![]() |
| Waandamanaji mjini Bangkok, Thailand |
Waandamanaji wa upinzani nchini Thailand wamefika makao
makuu ya jeshi la nchi hiyo mjini Bangkok, wakitaka jeshi liyaunge mkono
maandamano yao.
Waandamanaji hao wanaipinga serikali ya Waziri Mkuu wa
nchi hiyo, Yingluck Shinawatra, ambaye ni dada wa waziri mkuu wa zamani na
bilionea wa biashara ya mawasiliano, Thaksin Shinawatra, aliyeondolewa katika
mapinduzi ya mwaka 2006. Wananchi wanalalamika kuwa Thaksin bado anaiendesha
serikali ya dada yake kwa namna isiyokuwa ya moja kwa moja au kwa nyuma ya
mlango, na amekuwa akiishi uhamishoni tangu alipoondolewa madarakani.
Leo waandamanaji hao walilazimisha kwa nguvu kufunguliwa
kwa lango la makao makuu ya jeshi na kumiminika ndani ya viwanja vya ofisi hizo.
“Tunataka kujua kama jeshi litawaunga mkono wananchi au
litamuunga mkono dikteta,” alisema mmoja wa viongozi wa waandamanaji hao, Amorn
Amornrattananont.
Pia waandamanaji hao walikusanyika mbele ya makao makuu
ya chama cha Puea Thai, kinachoongozwa
na Waziri Mkuu, Yingluck.
Kwa siku za hivi karibuni, majengo ya serikali likiwemo
jengo la wizara ya fedha mjini Bangkok yamekuwa yakizingirwa na maelfu ya
waandamanaji wakiishinikiza serikali ijiuzulu.
Jana Waziri Mkuu, Yingluck Shinawatra, aliponea chupu
chupu katika kura ya kutokuwa na imani naye iliyoendeshwa na bunge la nchi hiyo.
Katika taarifa yake iliyorushwa na televisheni ya nchi
hiyo, Yingluck alisema kuwa serikali yake iko tayari kufungua uwanja wa
majadiliano na mazungumzo, akisema kuwa maafisa wa serikali yake wapo tayari
kusikiliza sauti za wananchi, wakiwemo wale waliozizingira na kuzikalia kwa
nguvu ofisi za serikali.
Hata hivyo, kiongozi wa upinzani, Suthep Thaugsuban, alitupilia
mbali wazo la kufanya mazungumzo.
“Yingluck anasema serikali inaweza kuendelea kutawala,
inaweza kuendelea kufanya kazi – ninataka kuwaambia kuwa wataweza kufanya kazi
kwa masiku kadhaa tu, baada ya hapo hatutawaacha kuendelea kufanya kazi,” Thaugsuban
aliwaambia wafuasi wake mjini Bangkok.
Maandamano nchini Thailand yaliibuka baada ya bunge la
seneti la nchi hiyo Novemba 11 kuuukataa
muswada unaoungwa mkono na serikali ambao ungempatia msamaha waziri mkuu wa
zamani, Thaksin Shinawatra, ambaye ni kaka wa Waziri Mkuu wa sasa, na
kumuwezesha kutoka uhamishono.
Thaksin Shinawatra anatuhumiwa kwa ubadhirifu, ufisadi,
ufujaji wa mali ya umma pamoja na kutumia madaraka yake vibaya kiasi cha
kutomheshimu mfalme wa nchi hiyo, ambaye anayetambuliwa na katiba, jambo
lililosababisha kung’olewa madarakani mwaka 2006.

0 comments:
Post a Comment