UAMUZI wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kumvua madaraka, Zitto Kabwe unadaiwa kuanza kukitesa
chama hicho na kwamba sasa uongozi wa juu umeamua kusaka suluhu ya jambo hilo.
Taarifa ambazo zimezinaswa kutoka Kinondoni, jijini Dar
es Salaam yalipo Makao Makuu ya Ofisi za Chadema, zinaeleza kuwa, tayari baadhi
ya viongozi wamekubali kuketi meza moja ya mazungumzo na Zitto baada ya kupewa
ushauri na watu mbalimbali wakiwamo wasomi wakubwa wanaoheshimika ndani ya
chama hicho.
Hatua hiyo imekuja wakati ambao tayari uamuzi wa kuwavua
madaraka, Zitto pamoja na Mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk.
Kitila Mkumbo, umesababisha mtafaruku na mgawanyiko ndani ya chama.
Uamuzi wa kuwavua uongozi makada hao ambao ulitangazwa
na Tundu Lissu mbele ya Freeman Mbowe, ulipokelewa kwa mtazamo tofauti na makada
wa chama hicho, ambapo baadhi waliamini kuwa ni sahihi huku wengine wakiyapinga
kwa madai kuwa yanaua demokrasia hasa kwa chama ambacho kimejipambanua
kupigania demokrasia nchini.
Miongoni mwa makada wanaodaiwa kupingana na hatua hiyo
ya kamati kuu ni wasomi, ambapo mmoja wao amemtaka Mbowe kutumia nafasi yake ya
uenyekiti kuzungumza na Zitto ili kukinusuru chama.
Msomi huyo aliyebobea katika masuala ya sheria nchini,
ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, pamoja na kutokubaliana na
baadhi ya vitendo vya Zitto, anadaiwa kuweka wazi kwamba utaratibu uliotumika
kumuadhibu si sahihi na hivyo ni vema jitihada za haraka zikafanyika ili
kulimaliza suala hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo kutoka kwenye chanzo cha
kuaminika kilicho karibu na Mbowe, mara baada ya kutangazwa kwa maamuzi ya
kuwavua uongozi Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, msomi huyo
alizungumza kwa kina na Mwenyekiti wake na inaelezwa kuwa baadhi ya maneno
mazito aliyotumia kumfikishia ujumbe yalisababisha Mbowe amwage machozi.
“Mwenyekiti alilia baada ya kuelezwa maneno mazito na
mmoja wa wanasheria wa chama, alimtaka aachane na mivutano hii na badala yake
akae mezani na Zitto ili wayamalize,” alisema mtoa habari wetu.
Imeelezwa kuwa baada ya ushauri huo, Mbowe alimuomba mwanasheria
huyo kumtafuta, Zitto ili wakae mezani.
Imebainika kwamba ni suala gumu kwa Mbowe kukaa meza
moja na Zitto bila ya kuwepo kwa mtu wa kuwasuluhisha kutokana na wawili hao
kuwa na migogoro iliyodumu kwa muda mrefu.
Katika kuhakikisha Mbowe na Zitto wanakutana na
wanamaliza tofauti zao zilizoanza kuchomoza mwaka 2009, tayari kuna mipango ya
kuunda Kamati ya usuluhishi ambayo inatajwa huenda ikaongozwa na Profesa
Mwesigwa Baregu na Mabere Marando.
Jukumu la wateule hao ni kuhakikisha wanawakutanisha
mahasimu hao ili kurejesha umoja na amani ndani ya chama.
Aidha zipo taarifa kwamba katika kuhakikisha amani ya
moja kwa moja inarejea ndani ya chama, Zitto amepangiwa kupewa nafasi ya
kuwania umakamu Mwenyekiti Bara, huku Mbowe akiachiwa nafasi yake.
Mbali na kuachiwa nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti, pia
zipo taarifa kwamba Zitto ataachiwa jukumu la kuwania nafasi ya urais kwenye
uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wakati ambapo mwaka 2015, Dk. Willbrod Slaa
atawania nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa,
Profesa Baregu na Marando wamepewa jukumu hilo la kusuluhisha, kutokana na
ushawishi walionao kwa pande zote mbili.
Inaelezwa kuwa Profesa Baregu amekuwa ni muumini wa
demokrasia ya kweli ndani ya chama na kwamba hakukubaliana na maamuzi ya kumvua
uongozi Zitto na Dk. Kitila na ndiyo sababu iliyomchagiza kutaka kujiuzulu
nafasi yake ya ujumbe wa Mkutano Mkuu.
Profesa Baregu, Said Arfi ambaye amejiuzulu nafasi yake
ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na Dk. Kitila Mkumbo ni miongoni mwa makada
wanaoaminika kusimamia demokrasia ya kweli ndani ya chama.
Msemaji wa Chadema, John Mnyika alipotafutwa kuzungumzia
taarifa hizo, hakukubali wala kukataa badala yake alisema masuala hayo hayajui.
Kwa upande wake, Zitto ambaye kwa sasa yuko nchini
Uingereza kwa kazi za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), aliliambia
Rai Jumatano kwamba taarifa hizo za chama kusaka suluhu naye amezisikia na
endapo atatakiwa kufanya hivyo haoni sababu ya kukataa.
“Nia yangu ni kuona tunavuka salama kwenye upepo huu na
ndio maana nimetangaza kwamba sitoki Chadema, njia pekee ya kuyamaliza haya ni
kuzungumza, sidhani kama nitakuwa na kipingamizi,” alisema Zitto.
Kwa upande mwingine jana chama hicho kimewaandikia barua
yenye mashitaka 11, Zitto, Mwigamba na Dk. Kitila.
Mbali na mashitaka hayo, pia katika barua hizo, wamepewa
muda wa siku 14 kujieleza kimaandishi ni kwanini wasichukuliwe hatua za zaidi,
kabla ya kujitetea tena mbele ya Kamati Kuu ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao
Makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
wa Chadema, Mnyika, alisema sekretarieti iliyokutana juzi, ilikamilisha uamuzi
uliopitishwa na Kamati Kuu ya kuwavua nyadhifa zao ndani ya chama.
Alisema sekretarieti ilijiridhisha kuwa makosa yao
yalitokana na waraka ambao kimsingi ulikiuka kanuni, maadili na taratibu za
chama.
“Mashitaka na makosa 11 waliyofanya, yamejikita katika
uamuzi wa Kamati Kuu na si maneno ambayo waliyazungumza mbele ya waandishi wa
habari katika mkutano wao wa Jumapili.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu
Lissu, alisema Zitto na wenzake wasipojieleza ndani ya siku 14, taratibu ambazo
hakuzitaja zitafuatwa.
Aidha, alimshangaa Zitto kupoteza lengo kwa kuwaambia
waandishi wa habari kuwa amefukuzwa kwa sababu za uongo na kwamba ni za
kizushi.
“Walichokifanya ni kupoteza lengo kwamba wamefukuzwa kwa
masuala ya PAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali), posho za
vikao vya Bunge, kuuza majimbo yetu ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2010 na mambo mengine waliyoyataja.
“Wamefukuzwa kwa kufanya mapinduzi bila kufuata utaratibu,
yaani kwa kifupi walikiuka maadili, hata hivyo, katika mashitaka yao
hayakuzungumzia habari za PAC,” alisema Lissu.
Kuhusu kauli ya Wakili wa Zitto, Albert Msendo, kwamba
Kamati Kuu ilijivika mamlaka yasiyoihusu kuwavua nyadhifa zao, isipokuwa Baraza
Kuu, Lissu alisema Kamati Kuu ilikuwa sahihi kuchukua uamuzi ule.
Kuhusu kauli ya Zitto kwamba ataendelea kuwa mwanachama
mwaminifu ndani ya Chadema, alisema si kweli kwani haiwezekani amtukane
Mwenyekiti (Freeman Mbowe), kisha aseme anaheshimu chama.
Aidha Chadema imesema waraka uliosambazwa kwenye
mitandao mbalimbali ya kijamii na kuchapishwa na baadhi ya magazeti ni feki, na
kwamba waraka halisi wanao na watautoa kwenye mitandao wakati ukifika.
HISTORIA YA MGOGORO WA ZITTO NA MBOWE
Historia ya mgogoro wa Zitto na Mbowe inaanzia mwaka
2009, wakati Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alipoamua kuchukua fomu ya kuwania
nafasi ya uenyekiti kwa staili ya kumshtukiza Mbowe ambaye alikuwa akiwania kwa
awamu ya pili.
Mbowe alichukua nafasi hiyo mwaka 2004 kutoka kwa
marehemu Bob Makani, ambaye alikiongoza chama hicho kwa awamu moja kutoka mwaka
1998 hadi 2004, kama alivyofanya mtangulizi wake, Edwin Mtei ambaye ndiye
mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho aliyekiongoza kutoka mwaka 1993 hadi 1998.
Katika kipindi cha awamu ya kwanza Mbowe alifanikiwa
kuimarisha harakati za chama hicho, ambapo aliweza kuongeza idadi ya wabunge
kutoka sita walioachwa na Makani hadi kufikia 11, watano wakiwa ni wa
kuchaguliwa na sita wa kuteuliwa.
Hatua hiyo ilimpa hamasa mwenyekiti huyo kukiongoza
zaidi chama, ambapo mwaka 2009 wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani, alionesha
dhahiri kukataa kupingwa kwenye uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa
Kiramuu, jijini Dar es Salaam.
Maamuzi ya Zitto kujitosa kuwania nafasi hiyo ya
uenyekiti, yaliibua msuguano mkali kati yake na Mbowe aliyekuwa akiungwa mkono
na muasisi wa chama hicho, Mtei pamoja na baadhi ya makada waliokuwa na dhana
kwamba Mwenyekiti huyo hastahili kupingwa.
Hofu ya Mbowe kupingwa ilizalisha makundi ndani ya
chama, ambapo kundi la mwenyekiti huyo lilimuona Zitto ni mtovu wa nidhamu na
hamuheshimu kiongozi wake na kwamba hakustahili kumpinga mtu ambaye hajamaliza
muhula wake wa pili wa uongozi ndani ya chama.
Wanamtandao wa Mbowe wakaibua hoja kwamba ni vema Zitto
akaondoa jina lake kwenye kuwania nafasi hiyo, ili kukiepusha chama na anguko
wakati huo kikijiandaa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwamba
kama chama kingeingia kwenye uchaguzi na mgawanyiko hali ingekuwa mbaya.
Jitihada za haraka za kukinusuru chama na mpasuko
zikafanyika, ikiwa ni pamoja na kufanya kikao cha usuluhishi kilichoundwa na
wazee kwa nia ya kutafuta muafaka kati ya Zitto na Mbowe, mbunge huyo wa Kigoma
Kaskazini alishawishiwa kuliondoa jina lake kwenye kinyang’anyiro hicho.
Hatua hiyo ilififisha dhana ya uwepo wa demokrasia na
badala yake ukawa mwanzo wa kuzaliwa kwa makundi.
KUKOSEKANA KWA DEMOKRASIA NDANI YA CHADEMA
Hatua ya kupigwa kwa kura ya ndiyo kwenye nafasi ya Mwenyekiti,
ilitowesha demokrasia ndani ya chama hicho, hata hivyo kutokana na wanachama
kuwa na dhamira ya kuiondoa CCM madarakani walifunika kombe na kuanzisha upya
harakati za kukisakama chama tawala.
Kwa kauli moja waliingia mtaani na kukisambaza chama kwa
wananchi na kufanikiwa kuongeza idadi ya wabunge na madiwani, ambapo waliweza
kupata wabunge 23 wa kuchaguliwa na 25 wa kuteuliwa na baadaye kuongeza mbunge
mmoja wa kuchaguliwa na hivyo kuwa na wabunge 49.
MGOGORO MPYA WA ZITTO NA MBOWE WAIBUKA 2010
Baada ya kumalizika wa safari ndefu ya uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2010 ambao kwa kiasi kikubwa ulikiongezea umaarufu chama, baada ya kuleta
upinzani mkali dhidi ya CCM na hata kukipatia idadi kubwa ya wabunge kwa mara
ya kwanza, Mbowe na Zitto walilazimika kufanya shughuli za chama ndani ya Bunge
kwa kuendeleza mapambano dhidi ya CCM na Serikali yake.
Ni kutokana na msingi huo na katika hatua ya kuonesha
demokrasia ya kweli ndani ya chama, Chadema kilipopata nafasi ya kuongoza Kambi
ya Upinzani Bungeni, kilitoa mwanya kwa wabunge wote wa chama hicho kuwania
nafasi hiyo.
Zitto na Mbowe ndio wabunge wa Chadema walioonesha nia
ya kuiomba nafasi hiyo, hali hiyo iliibua utata mwingine wa demokrasia ndani ya
chama, ambapo katika kuukwepa ushindani Mwenyekiti wa Chadema akatumia turufu
ya Bunge la Tanzania kufuata sheria za Bunge la Jumuiya ya Madola kwa kusema
kuwa kiongozi wa chama anapokuwepo bungeni anakuwa na nafasi ya wazi ya kuwa
Kiongozi bungeni.
Kwa muktadha huo moja kwa moja, Mbowe akazima ndoto za
Zitto na kuchukua nafasi hiyo bila kupingwa huku akimuachia mpinzani wake huyo
nafasi ya Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Ingawa Zitto alikubaliana na maamuzi hayo, wachambuzi wa
masuala ya siasa wanaamini kwamba ilimzidisha mgawanyiko kati ya wawili hao.
MGOGORO WA SASA
Kama ilivyokuwa mwaka 2009, ambapo mgogoro uliibuka
wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa chama, ndivyo ilivyo sasa ambapo pamoja na
mambo mengine pia inaelezwa kuwa kiini cha mgogoro unaoendelea ni nafasi ya
Uenyekiti.
Inaelezwa kwamba, Mbowe amejipanga kukiuka makubaliano
ya mwaka 2009, kwa kutaka kuwania awamu ya tatu ya uenyekiti, jambo ambalo
linaonekana ni kinyume na makubaliano yao ya awali.
Ukiukwaji huo wa makubaliano ndiyo uliwasukuma makada
wanaomuunga mkono Zitto kuandika waraka uliopewa jina la Mkakati wa Mabadiliko
2013, unaoonesha nia na dhamira zao za kutaka kumuondoa Mbowe madarakani kwa
njia ya demokrasia.
Waraka huo ulioandaliwa na Dk. Kitila na Mwigamba ambao
inadaiwa kwamba Zitto hakuujua, uliainisha sifa na mapungufu ya Mbowe, pamoja
na udhaifu na uimara wa kiongozi wanayemtaka apambane na mwenyekiti wa sasa.
Hata hivyo kabla mikakati hiyo haijatimia, baadhi ya
viongozi wa chama hicho walifanikiwa kunasa mkakati huo uliotumika
kuwawajibisha Zitto (MM), Dk. Kitila (M1) na Mwigamba (M3).
Aidha zipo taarifa kwamba baadhi ya mambo mengine
yanayochochea mgawanyiko ni hatua ya mke wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbuzi
kudaiwa kuhusika katika kuusambaza waraka wa siri uliokuwa ukimtuhumu na
kumtishia maisha mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, ingawa Mnyika amepinga hoja
hiyo kwa kudai kuwa Mushumbuzi hahusiki kwa lolote.
MGAWANYIKO NDANI YA CHAMA
Taarifa za uhakika zimebainisha kwamba, kwa sasa ndani
ya chama hicho kumekuwa na mgawanyiko, ambao ulionekana dhahiri kwenye mkutano
wa Kamati Kuu, uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Imeelezwa kuwa ndani ya mkutano huo kulikuwa na mvutano
mkubwa, ambapo baadhi ya wajumbe wa mkutano huo walioongozwa na Mbunge wa
Mpanda, Said Afri, Profesa Safari, Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffer Michael na
Zitto walitoka nje ya ukumbi wa mkutano huo.
Hali ya mgawanyiko iliendelea hata wakati wa kupiga
kura, ambapo baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wakiongozwa na Mwenyekiti wa
Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), John Heche na Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa
Shinyanga, Shilungushela Nyangaki waligoma kupiga kura.
CHANZO: Gazeti la Rai

0 comments:
Post a Comment