![]() |
| Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye. |
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana ataanza
ziara ya siku 22 kwenye mikoa ya Ruvuma na Mbeya kuanzia tarehe 15/11/2013
mpaka mwanzoni mwa mwezi wa Desemba 2013.
Huu ni mwendelezo wa ziara za kichama katika kuimarisha
chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na
kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi.
Katika ziara zilizopita na vikao kadhaa vya chama Serikali iliagizwa kushughulikia baadhi ya
kero, na tumeshuhudia baadhi ya hoja hizo zikichukuliwa hatua. Baadhi ya hoja
zilizoanza kushughulikiwa na Serikali ni pamoja na:-
1) Hoja ya
kufufua viwanda nchini.
Baada ya ziara kadhaa za Katibu Mkuu, uchambuzi na vikao
kadhaa vya CCM, Chama kiligundua kuwa viwanda vingi vilivyo binafsishwa
havifanyi kazi kama ilivyokusudiwa na vingine kufungwa kabisa na kugeuzwa
magodauni.
Pamoja na athari kubwa kwa uchumi wa nchi yetu, kufungwa
na kutofanya vizuri kwa viwanda hivyo kumechangia sana tatizo la ajira nchini
kuwa kubwa.
Hivyo Chama
kiliagiza Serikali kufanya tathmini ya viwanda vyote vilivyo binafsishwa na
hali yake kwa sasa na vile visivyofanya kazi kama ilivyokusudiwa vichukuliwe na
Serikali na kutafuta njia sahihi ya kuvifufua upya.
Serikali imechukua hatua kadhaa katika hili, ikiwemo
kufanya tathmini na mapendekezo kadhaa yamewasilishwa na timu iliyoundwa na
Serikali kwa ajili ya kufanyia uamuzi na kuchukua hatua.
Tunajua zipo hatua kadhaa zimechukuliwa katika jitihada
za kufufua viwanda vya kubangua korosho kama sehemu ya utatuzi wa tatizo la
soko na zao la korosho.
Pia Serikali ipo
katika hatua kadhaa za kushughulikia viwanda vingine nchini.
Tunaipongeza serikali kwa hatua hii muhimu ya kutekeleza
agizo la chama. Tunaitaka serikali ikamilishe zoezi hili mapema iwezekanavyo
ili nchi ifaidike na ufufuaji huu wa viwanda nchini.
2)
Changamoto kwa wakulima wa pamba
Katika ziara ya Katibu Mkuu mikoa kadhaa ya Kanda ya
Ziwa, alitumia muda mrefu kujifunza na kuzungumza na wakulima wa zao la pamba
wa mikoa hiyo.
Pamoja na tatizo kubwa la soko na bei ya pamba,
pamekuwa na changamoto kubwa ya mfumo
unaosimamia zao la pamba ikiwemo upatikanaji wa pembejeo.
Hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni
pamoja na kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza nyuzi, nguo na
kukamua mafuta ya pamba.
Tulishuhudia ujenzi wa viwanda kadhaa mjini Shinyanga,
vingi vikijengwa na wawekezaji kutoka China.
Lakini wakati wa Bunge la juzi, Serikali imeamua kutoa
ruzuku ya asilimia hamsini kwa mbegu bora za pamba ili kuwawezesha wakulima
kumudu bei ya mbegu hizo na hivyo kuboresha zao la pamba nchini na maisha ya
wakulima kuwa bora zaidi.(bei ya dukani kwa kilo moja ni Sh. 1,200/=; Serikali
italipia Sh.600/=).
Katika hili la mbegu bora na kilimo cha mkataba
tunaitaka Serikali na hasa wakuu wa wilaya na mkoa kuacha mara moja kutumia
nguvu kuwalazimisha wakulima kulima kwa mkataba na kutumia mbegu bora badala
yake wawaelimishe na kuwashawishi badala ya kutumia nguvu.
Tunaipongeza Serikali kwa kuanza kuchukua hatua za
kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya CCM ya namna ya kutatua matatizo
yanayowakabili wakulima wa pamba nchini.
Tunaitaka Serikali kuongeza kasi ya utatuaji wa
changamoto hizo ili wakulima wa pamba wafaidike na uchumi wa nchi kukua kwa
kasi nzuri.
3).
Migogoro kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi juu ya matumizi ya ardhi
Katika ziara mbalimbali za Katibu Mkuu kwenye mikoa kama
ya Morogoro, Njombe, Simiyu, Mara n.k. alishuhudia migogoro mingi sana juu ya
wakulima, wafugaji na hifadhi mbalimbali
nchini.
Hakuna shaka migogoro hiyo imegharimu sana maisha ya
watu na mali zao na hata uchumi wa nchi yetu.
Chama kiliagiza migogoro hiyo kushughulikiwa mapema na
kupata ufumbuzi wa kudumu. Chama kinalipongeza Bunge na hasa Wabunge wa CCM na
Serikali yake kwa uamuzi wa kuunda Kamati teule ya Bunge kuchunguza na kutoa
mapendekezo ya hatua kadhaa za kuchukuliwa katika kufikia suluhisho la kudumu
kwa migogoro hii.
Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kutosha kwa
kamati teule ya Bunge ili kazi hii ya kamati iwe na matokeo mazuri
yatakayosaidia kumaliza tatizo hili nchini.
Wakati Kamati teule ya Bunge ikifanya kazi yake,
tunawaomba wakulima na wafugaji kote nchini kutulia kusubiri matokeo ya kamati
hii teule ya Bunge.
Hivyo basi, ziara
hii ya Katibu Mkuu imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha Chama, kukagua
Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero za wananchi. Tumeona jinsi ziara
zilizotangulia zilivyokuwa na matokeo mazuri, tunaamini ziara hii pia itakua na
matokeo mazuri.
Imetolewa na:-
(Sgd.)
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
12/11/2013

0 comments:
Post a Comment