![]() |
| Waasi wa M23 baada ya kujisalimisha kwa serikali ya Uganda |
Na Kabuga Kanyegeri
Waratibu wa mazungumzo ya amani yanayofanyika mjini
Kampala baina ya maafisa wa serikali ya Kongo na waasi wa M23 wamesema kuwa
mazungumzo yataendelea, licha ya pande hizo mbili kushindwa kufikia muafaka
hapo jana.
"Pande zote mbili bado zipo hapa Uganda… Mazungumzo
hayajafungwa rasmi,” msemaji wa serikali Uganda, Ofwono Opondo, aliwaambia
waandishi wa habari.
Mazungumzo yalivunjika baada ya serikali ya Kongo kutaka
kuwepo kwa mabadiliko katika hati ya mkataba, licha ya kamba Waziri wa Mambo ya
Nje wa Kongo, Raymond Tshibanda, alikuwa amesisitiza kuwa serikali inataka
amani.
Uganda, ambayo ni mwenyeji wa mazungumzo hayo, ilisema
kuwa inatarajia mazungumzo hayo yataendelea.
Mnamo Novemba 5, Kongo ilitangaza kuwa imewashinda
kabisa waasi wa M23 baada ya kuziteka ngome za mwisho za kundi hilo kaskazini mwa
Goma na kuhitimisha vita iliyodumu kwa muda wa miezi 20.
Saa chache baadaye, kiongozi wa M23, Bertrand Bisimwa,
alitangaza kuwa kundi lake limeachana na mapigano na kwamba litaweka silaha
chini na kufanya mazungumzo ya amani.
Waasi wa M23, walikuwa wakiyashikilia maeneo kadhaa
mashariki mwa nchi hiyo na kuendesha mapambano dhidi ya serikali kuu.
Mapema mwaka huu, Umoja wa Mataifa uliidhinisha
kupelekwa kwa kikosi maalumu kinachoundwa na wanajeshi wa Kiafrika kikiwa na
mamlaka ya kupambana na waasi hao.
Licha ya kusambaratika kwa kundi la M23, ndani ya Kongo
bado kuna makundi mengi ya waasi na mengi yapo katika eneo la mashariki lenye
utajiri mkubwa wa madini.

0 comments:
Post a Comment