![]() |
| Waandamanaji wakipaza sauti kupinga utawala wa kijeshi mjini Cairo Novemba 27, 2013 |
Na Kabuga Kanyegeri, Istanbul
Joto la kisiasa nchini Misri limeendelea kuwa juu baada
ya mahakama moja kuwapa adhabu ya kifungo cha miaka 11 jela mabinti 21, huku
maimam 17 wa misikiti wakikamatwa katika mji wa Gharbeya kwa kile kinachodaiwa
kuwa wamefanya uchochezi dhidi ya jeshi.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Shorouk la nchini humo,
mahakama hiyo ndogo katika mji wa Alexandria imewapa adhabu mabinti hao 21 kwa
sababu ya kushiriki katika maandamano ya kuipinga serikali ya mpito iliyowekwa
madarakani na jeshi la nchi hiyo.
Aidha, kwa mujibu wataarifa zilizotolewa na vyombo
vinavyoliunga mkono Vuguvugu la Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood),
wanafunzi kadhaa walikamatwa na polisi ya nchi hiyo baada ya kuingia katika makazi
ya wanafunzi hao katika chuo kikuu cha al-Fayoum.
Polisi waliingia katika majengo cha hicho wakafyatua
gesi ya kutoa machozi na kuwakamata wanafunzi kadhaa waliokuwa wakipanga
kufanya maandamano dhidi ya mapinduzi yaliyofanywa na jeshi.
Katika ripoti nyingine, mwendesha mashitaka nchini humo
ameagiza kuwaweka kizuizi kwa siku nne wanaharakati 24 waliokamatwa wakati wa
maandamano ya kupinga sheria mpya inayowatia hatiani wale wanaoandamana bila
kibali.
Adiha, kibali cha kikamatwa kimetolewa dhidi ya
wanaharakati maarufu wanaotuhumiwa kuwachochea waandamanaji kufanya maandamano.
Mamlaka nchini humo zinamsaka mwanaharakati mashuhuri
Alaa Abdul Fatta na Ahmad Maher, muasisi wa vuguvugu la Aprili 6 lililoongoza
mapinduzi dhidi ya aliyekuwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Husni Mubarak mwaka
2011.
Siku ya jana, vikosi vya usalama vilitumia maji ya
kuwasha kuwatawanya watu waliokuwa wakiandamana nje ya bunge la seneti mjini
Cairo.
Waandamanaji hao walikuwa wakipinga mabadiliko ya muswada
wa katiba yatakayoruhusu raia kushitakiwa katika mahakama za kijeshi.
Mnamo Novemba 24, nchi hiyo ilianzisha sheria yenye
utata ambayo mikusanyiko ya zaidi ya watu 10 itahitaji kibali siku tatu kabla
ya kufanyika.
Operesheni ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo dhidi ya
waandamanaji imekuwa ikikoselewa vikali na Kamishna wa Haki za Binadamu wa
Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, na shirika la kimataifa la haki za binadamu, Amnesty
International.

0 comments:
Post a Comment