
WAKATI hatima ya kutiwa saini mkataba wa amani kati ya
Serikali ya DRC na waasi waliosambaratishwa wa M23 ikiwa haijulikana, uhusiano
wa maswahiba wawili wa eneo la Maziwa Makuu, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na
Paul Kagame wa Rwanda umetikisika baada ya Museveni kumtaka mwenzake huyo
azungumze na waasi.
Ni ushauri kama huo aliopewa Kagame Mei mwaka huu na
Rais Jakaya Kikwete ukilenga kuleta na kuimarisha amani Mashariki mwa Congo
ndio ulioyumbisha uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda, kabla ya Kikwete
kuifafanua na kisha kukutana na Kagame jijini Kampala, Uganda Agosti mwaka huu.
Kwa mujibu wa mtandao wa AfroAmerica Network, Museveni,
baada ya kurejea kutoka kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC na zile za
Maziwa Makuu (IGGLR) huko Pretoria, Afrika Kusini wiki iliyopita, alimpigia
simu Kagame na kumwambia: “Huenda sasa ni wakati muafaka wa kuzungumza na
wapinzani wako wenye silaha.”
Chanzo cha habari cha mtandao huo kimemnukuu mmoja kati
ya viongozi wa juu wa Jeshi la Rwanda (RDF), akisema Museveni alimwomba Kagame
kuzungumza na waasi hao haraka kabla muda haujapita mara tu Rais huyo wa Uganda
aliporejea Kampala Alhamisi iliyopita.
Mkutano wa pamoja wa wakuu wa nchi za SADC na ICGLR
uliofanyika kuanzia Jumatatu wiki iliyopita chini ya uenyekiti wa marais
watatu, Joyce Banda (Malawi, SADC), Museveni (Uganda, ICGLR) na wa Afrika
Kusini, Jacob Zuma, ulitoa wito kwa M23 kuweka silaha chini. Siku mbili baadaye
waasi hao wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, walishindwa vita na kutangaza
kuacha uasi.
Kagame hakuhudhuria mkutano huo, badala yake
aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo.
“Ni ushauri tu. Nimerejea kutoka kwenye mkutano na SADC
uliojadili amani eneo la Maziwa Makuu. Bahati mbaya inaonekana kwamba karibu
viongozi wote wanaamini kikwazo kikubwa cha amani ni kuwapo kwa waasi wa Kinyarwanda
mashariki mwa DRC.
“Hakika suala hili linapaswa kuzungumzwa kwa njia moja
au nyingine. Na viongozi hao wanaamini kwamba hili halitatatuliwa bila serikali
ya Rwanda kukaa kwenye meza ya usuluhishi na wapinzani wake wenye silaha. Hata
mimi ninaamini hivyo, huenda wakati umefika kwako kuzungumza nao,” alinukuliwa
Museveni akimwambia Kagame katika mazungumzo ya simu yaliyodumu kwa takriban
dakika 15.
Kagame alijibu: “Sitozungumza na FDLR, washiriki wa
mauaji ya kimbari. Never, … , ever. Sitozungumza kamwe na wahalifu.”
Hata hivyo, inadaiwa Museveni alimkumbusha Kagame kuwa
si waasi wote wa Rwanda walioko DRC ni wanachama wa FDLR au wahalifuna kwamba
wapo anaoweza kuzungumza nao kwa kuanzia.
Baada ya mazungumzo hayo, Kagame aliitisha mkutano wa
dharura na washauri wake wakuu na kuwaeleza walichozungumza na Museveni na
kuongeza:
“Nimekuwa nikiwaambia mara kwa mara kuwa tuko peke yetu.
Hata Yoweri, tuliyemwamini kama rafiki yetu na mwenzetu anatugeuka! Leo
anatuambia hiki, kesho anakwenda kukutana na viongozi wengine na
kutubadilikia.”
Baadaye akawataka washauri hao kuja na mpango mkakati wa
nini cha kufanya wakati huu Rwanda ikizidi kutengwa na nchi za Afrika na hata
za nje ya Afrika.
Mwanzoni mwa mwezi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,
John Kerry na mwenzake wa Uingereza walimwonya Kagame kuachana mara moja na
ushiriki wake kwenye machafuko ya mashariki mwa DRC, ikiwa ni mara ya pili
ndani ya mwaka mmoja kwa wakubwa hao kutoa onyo kama hilo.
Wakati hayo yakiendelea, zipo taarifa kwamba Rais Museveni
amepanga kutuma ujumbe nchini kuja kuzungumzia mustakabali wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaambia Watanzania kwamba
Tanzania haijakiuka chochote katika makubaliano ya msingi, ila wenzetu hao ndio
huenda wana ajenda yao.
Kauli ya Kikwete ilihitimisha hali ya wasiwasi wa
Tanzania kujitoa EAC na iwapo ujumbe wa Uganda utakuja, itakuwa ni mwendelezo
wa kilichofanywa mwishoni mwa wiki na Kenya waliomtuma Waziri wa Mambo ya Nje
kuja Dar es Salaam kuweka mambo sawa.
HALİ NCHİNİ KENYA
Mapema wiki hii, aliyekuwa Mwanasheria wa Serikali ya
Kenya, Amos Wako ambaye pia ni Seneta wa Bisia alitoa wito kwa Rais Uhuru
Kenyatta kuhakikisha kuwa EAC haisambaratiki, akidai kuwa watakaoumia zaidi ni
Wakenya.
Wako aliyekuwa kwenye mkutano wa hadhara pamoja na
Mbunge wa Budalangi, Ababu Namwumba, alisema wakati jumuiya ya awali
ilipovunjika mwaka 1977, Wakenya wengi waliokuwa wakifanyakazi nje ya nchi ndio
walioathirika zaidi.
“Wapo watu mashuhuri kama Raila Odinga na Kalonzo Musyoka
wanaokubalika ndani na nje ya nchi ambao kama Uhuru anataka wanaweza kumsaidia
kuzungumza na Rais Kikwete wa Tanzania. Hatutaki jumuiya hii ivunjike, si
busara hata kidogo,” alisema Wako.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment