MCHUNGAJI wa Kanisa la Shakinah Pentecostal la mjini
Dodoma, Nabii Elisha Mliri, ambaye pia ni mume wa marehemu Angela Chibalonza,
aliyekuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili, anatuhumiwa kumpa mimba mwanafunzi wa
kidato cha tatu wa Shule ya City High School (jina linahifadhiwa).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana
(juzi), mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Mary Mkombola (49) alidai kuwa mwanaye
alikuwa akisumbuliwa na mapepo, hivyo akaamua kumpeleka kwa Nabii Elisha
ili aweze kuombewa tatizo hilo lililokuwa likimsumbua.
Mama huyo alisema kuwa mara baada ya kumpeleka binti
yake, alifanyiwa maombi na nabii huyo na kisha kuelezwa kuwa alikuwa
anasumbuliwa na pepo ambalo pia lingemharibia masomo yake.
Kwa mujibu wa mama huyo, baada ya mchungaji kumfanyia
maombi binti yake, alimwambia kuwa
atamsaidia kumsomesha kwa kumlipia ada ya mwaka mzima kutokana na yeye kuwa
mjane.
“Alimdanganya atamlipia ada ya mwaka mmoja sh 400,000
ili aendelee na masomo halafu akaniambia kuwa ataniombea na mimi ili niweze
kupata uwezo wa kuendelea kumsomesha,” alisema mama huyo.
Aliongeza kuwa mara baada ya kukubaliana na mtoto wake,
alipeleka taarifa shuleni ambako aliambiwa apeleke barua ya kuthibitisha kuwa
atakuwa anamlipia ada mwanafunzi huyo.
Mkombola alifafanua, kuwa mara baada ya kupeleka barua
shuleni na kukubaliwa, mtoto huyo aliendelea na masomo yake lakini baadaye
alianza kumhisi ni mjamzito.
Alisema kuwa alimuuliza kama ana ujauzito akawa hataki
kumwambia ndipo akaamua kumchapa na kukimbilia kwa mama yake mkubwa maeneo ya
Mbwanga.
“Alipokimbilia kule ndipo akaenda kuwaeleza mama zake
wakubwa kuwa mama ananipiga wakati mimba nimeipata kule alikonipeleka
nikafanyiwe maombi, ikabidi wanipigie simu na kuniambia kuwa mwanangu ana
ujauzito na amepewa na Nabii Elisha.
“Nilimuuliza akanisimulia mambo yote ambayo amekuwa
akifanyiwa na nabii huyo tangu alipopelekwa kufanyiwa maombi mwezi Machi mwaka
huu,” alisema.
Mama huyo aliongeza kuwa waliamua kwenda polisi kutoa
taarifa na kupatiwa fomu ya matibabu kwa ajili ya vipimo ambapo binti huyo aligundulika kuwa ana ujauzito.
Alisema kuwa walipeleka majibu hayo polisi na kutoa maelezo
ambapo waliambiwa kuwa wasubiri uchunguzi unaendelea na utachukua muda mrefu.
“Tulitoa maelezo polisi mimi na mwanangu na kuambiwa
kuwa tusubiri bado wanafanya uchunguzi lakini muda umepita sasa na mtoto tumbo
linazidi kukua na masomo kasimama bila kujua hatima yake,” alisema.
VIONGOZI WA KANISA
Alibainisha kuwa mara baada ya baadhi ya viongozi wa
kanisa hilo kupata taarifa, walimfuata mama huyo wakimsihi asilipeleke suala
hilo polisi bali wao watalimaliza.
“Walinifuata watumishi wawili ambao ni Nabii Mgamba na
Nabii Monika wakasema nisifanye lolote wao watamtunza au kama ikiwezekana
tuitoe mimba hii, jambo ambalo sikukubaliana nalo,” alisema.
MWANAFUNZI AELEZA
Naye mwanafunzi huyo alisema kuwa Juni 8, mwaka huu,
asubuhi alipigiwa simu na Nabii Elisha akamwambia aende mjini na alipofika
alimpakia kwenye gari lake na kwenda naye kwenye nyumba ya kulala wageni
iliyoko maeneo ya jirani na Chuo cha CBE mjini hapa.
“Nilimuuliza tunakwenda wapi, akaniambia tunakwenda
kanisani lakini cha kushangaza tulilipita kanisa, hivyo nikawa na wasiwasi
lakini kabla hatujafika tulikokuwa tunakwenda tukapita sehemu akaongeza upepo
kwenye tairi,” alisema.
Kwamba baada ya kujaza upepo, waliondoka na kwenda
katika nyumba hiyo ya kulala wageni lakini kabla hawajashuka alimpatia soda
aina ya Fanta akanywa na muda mfupi akapoteza fahamu kidogo na alipozinduka
akajikuta anafanya mapenzi na mchungaji huyo.
“Nilijikuta kifuani mwa nabii tukiwa wote watupu,
nikaanza kulia, akanibembeleza na kuniambia ‘unafikiri kukulipia ada yote hiyo
ilikuwa ni bure’ mbona wapo watu wengi sijawalipia ada, lazima nifanye na wewe
mapenzi mara tano, kwa hiyo bado mara nne nitafanya na wewe hata kwa nguvu na
ukimwambia mtu nitakuua kwa maombi,” alisema.
Binti huyo alidai kuwa tangu siku hiyo hakuweza kuziona
siku zake tena mpaka mama yake alipoanza kumhisi kuwa ana ujauzito na kumpeleka
kupima na kubainika ni kweli.
POLISI
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Suzan Kaganda,
alithibitisha kuwa tayari walikwisha kuyapokea malalamiko ya mwanafunzi huyo na
wanayafanyia kazi.
“Tunayafanyia kazi, kwani tulipata malalamiko hayo
lakini tunasubiri hadi atakapo jifungua tuweze kutumia kipimo cha vinasaba
(DNA) kuthibitisha aliyempa ujauzito,” alisema.
Alipotafutwa Nabii Elisha alisema kuwa hayuko Dodoma kwa
wakati huu na kumtaka mwandishi aende polisi atapata maelezo zaidi.
CHANZO: Tanzania Daima

0 comments:
Post a Comment