
Na Kabuga Kanyegeri
RAIS aliyeondolewa madarakani nchini Misri, Muhammad
Mursi, amesema katika barua maalumu aliyoiandika, kuwa alitekwa nwa Walinzi wa
Jamhuri kabla ya jeshi kutangaza rasmi kuwa limemuuzulu mwezi Julai.
Katika barua hiyo iliyosomwa katika televisheni jana na
wakili wake, Muhammad Damati, Mursi anasema: “Wananchi wema wa Misri wanapaswa
kujua kuwa nilitekwa kwa nguvu na bila ridhaa yangu kuanzia Julai 2 mpaka Julai
5 katika jengo la Walinzi wa Jamhuri mpaka pale mimi na msaidizi wangu
tulipohamishwa tena kwa nguvu kwenda kwenye kambi ya jeshi la maji kwa muda wa
miezi minne kamili.”
Aidha, katika barua hiyo, Mursi alitangaza kuwa yeye
ndiye rais halali wa Misri na kuelezea kitendo cha kuondolewa kwake madarakani
kuwa ni mapinduzi ya kijeshi na ni kosa la jinai.
"Misri haitatulia mpaka yote yaliyotokea kwa sababu
ya mapinduzi haya yatakapoondoka na wale waliohusika na umwagaji damu kila
mahali katika taifa washitakiwe,” alinukuliwa akisema.
"Ninawapongeza wananchi wa Misri waliosimama dhidi
ya mapinduzi haya, ambayo yatashindwa kwa nguvu ya umma wa Misri katika
kupigania haki na uhuru wao,” aliongeza kusema.
Mapema usiku wa Julai 3, mkuu wa jeshi la Misri Jenerali
Abdul Fattah al-Sisi alitangaza kuwa Mursi ameondolewa madarakani, akamtangaza
mkuu wa Mahakama Kuu ya Katiba, Adly Mahmoud Mansour, kuwa rais mpya wa mpito
na kusimamisha matumizi ya katiba.
Maafisa wa jeshi walisema kuwa Mursi, aliyeingia
madarakani Juni 2012, alikuwa ameshikiliwa na jeshi sehemu maalumu.
Misri imekuwa katika ghasia na vurugu tangu Julai 3.
Serikali ya Mansour imeanzisha operesheni maalumu dhidi ya wafuasi wa Mursi na
kuwakamata zaidi ya wanachama 2,000 wa Vuguvugu la Udugu wa Kiislamu, akiwemo
kiongozi mkuu, Muhammad Badie, aliyekamatwa Agosti 20.
Watu wapatao 1,000 waliuawa ndani ya wiki moja katika
makabiliano baina ya wafuasi wa Mursi na vikosi vya usalama baada ya polisi
kuzibomoa kambi zao katika operesheni kabambe dhidi ya wafuasi hao Agosti 14.
Mauaji hayo yaliamsha lawama za kimataifa na kuzifanya
taasisi mbalimbali kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu ghasia na
mauaji hayo.
0 comments:
Post a Comment