![]() |
| Wapiganaji wa M23 wamekusanyika ndani ya uzio baada ya kujisalimisha kwa serikali ya Uganda katika kijiji cha Rugwerero, takriban kilometa 500 magharibi mwa mji mkuu wa Uganda, Kampala. |
Na Kabuga Kanyegeri
MKATABA wa amani uliokuwa ukitarajiwa kusainiwa baina ya
serikali ya Kongo na waasi wa M23 umeakhirishwa baada ya maafisa wa serikali
kuomba muda zaidi wa kuupitia mkataba hu.
Msemaji wa serikali ya Uganda, Ofwono Opondo, amesema
jana kuwa muafaka utalazimika kusubiri mpaka serikali ya Kongo itakapofikia
uamuzi wake.
Mkataba huo ambao ulitarajiwa kusainiwa jana katika mji
wa Entebbe nchini Uganda, ni hatua muhimu ya kumaliza miongo kadhaa ya vita nchini
humo.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Okello
Oryem, alisema kuwa makubaliano hayakufikiwa baada ya serikali ya Kongo
kusisitiza kuwa itasaini “azimio” la kwamba uasi umekwisha badala ya kufanya “makubaliano”
na waasi walioshindwa vita, suala linaloonesha ugumu katika kuzisuluhisha pande
mbili.
Maafisa wa Kongo hawakutoa maelezo yoyote kuhusu hali
hiyo na haijatangazwa tarehe ya kikao kingine baina ya pande hizo.
Hivi karibuni mamia ya waasi wa M23 walikimbilia Uganda
baada ya kushindwa na vikosi vya jeshi la Kongo, ambalo linasaidiwa na brigedi
maalumu ya Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Mnamo Novemba 5, kundi la M23 lilisema kuwa litaweka
silaha chini na kuingia katika mazungumzo ya amani baada ya ngome zake za milimani
katika vijiji vya Tshanzu na Runyoni kwenye mpaka wa Uganda na Rwanda
kudhibitiwa na vikosi vya serikali ya Kongo.
Makundi kadhaa yenye silaha, ikiwemo M23, wanaendesha
harakati zao za uasi mashariki mwa Kongo na wanapigania kuidhibiti nchi hiyo
kubwa yenye maliasili za madini, kama vile dhahabu, urani, coltan, ambayo
hutumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya elektroniki, ikiwemo simu za
mkononi.
Waasi wa M23 waliuteka mji wa Goma Novemba 20, 2012
baada ya walinda amani kuondoka katika
mji huo wenye wakazi milioni moja. Wapiganaji wa M23 waliondoka katika mji huo
Desemba 1,2013 baada ya makubaliano ya kusimamisha mapigano.
Waasi wa M23 walijiondoa katika jeshi la Kongo mwezi
Aprili 2012 kupinga kile walichodai kuwa ni mwenendo mbaya ndani ya jeshi la
Taifa (FARDC). Walikuwa wamejumuishwa katika jeshi chini ya mkataba wa amani
uliosainiwa mwaka 2009.
Tangu mwezi Mei 2012, takriban watu milioni 3
wameyekimbia makazi yao katika eneo la mashariki mwa Kongo. Takriban watu
milioni 2.5 ni wakimbizi wa ndani, huku zaidi ya watu 460,000 wamekimbilia
katika nchi za Rwanda na Uganda.
Kongo imekuwa ikikabiliwa na matatizo matatizo kwa
miongo kadhaa, kama vile umaskini uliokithiri, miondombinu mibovu, na vita
katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambavyo viliibuka tangu mwaka 1998 na
kugharimu maisha ya zaidi ya watu milioni 5.5.

0 comments:
Post a Comment