![]() |
| Rostam Aziz |
Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz (49),
ametajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa sasa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la Marekani
la Forbes na kutoa taarifa yake juzi, Rostam amekamata nafasi hiyo na ya 27
katika Afrika akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni moja (Sh1.6
trilioni).
Mbunge huyo wa zamani wa Igunga, ameingia kwa mara ya
kwanza katika orodha ya matajiri 50 wa Afrika ya jarida hilo, pamoja na
wafanyabiashara wengine wa Tanzania, Reginald Mengi na Mbunge wa Singida Mjini
(CCM), Mohamed Dewji ‘Mo’. Katika orodha hiyo pia yumo Said Bakhresa ambaye
aliwahi kutajwa siku za nyuma.
Rostam, ambaye aliachana na siasa mwaka 2011, amempiku
Bakhresa, ambaye mwaka jana Jarida la Ventures Africa la Nigeria lilimtaja kuwa
ndiye aliyekuwa tajiri namba moja wa Tanzania. Bakhressa katika kipindi hicho
alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 620 milioni (Sh971 bilioni).
Katika orodha hiyo ya Ventures Africa, Bakhresa
alifuatiwa na Rostam, Mengi na mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi anashika nafasi ya pili kwa Tanzania na ya 34
Afrika akiwa na utajiri wa Dola 550 milioni (Sh861 bilioni).
Forbes linaonyesha kuwa Bakhresa amefungana na Mo katika
nafasi ya tatu ya orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika, wote
wakiwa na utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783 bilioni).
Rostam, Mengi na Bakhresa hawakupatikana jana
kuzungumzia suala hilo huku Mo akisema kwamba asingeweza kuzungumzia suala hilo
kwa kuwa jana alikuwa katika mapumziko ya Sikukuu ya Ashura.
Tajiri wa Nigeria, Aliko Dangote, ambaye anajenga
Kiwanda cha Saruji huko Mtwara ndiye anayeshika nafasi ya kwanza katika orodha
ya Afrika, akiwa na utajiri wa Dola20 bilioni (Sh31.7 trilioni), akifuatiwa na
familia ya Johanny Rupert ya Afrika Kusini yenye utajiri wa Dola7 bilioni
(Sh10.7 trilioni) na Nick Oppenheimer, pia wa Afrika Kusini mwenye utajiri wa
Dola 6.6 bilioni (Sh10.3 trilioni).
1)ROSTAM AZIZ
Jarida la Forbes limeripoti kuwa utajiri wa Rostam
unachangiwa zaidi na biashara ya mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi na
uchimbaji wa madini.
Anamiliki asilimia 35 ya hisa katika Kampuni ya Simu za
mkononi ya Vodacom. Ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya simu za mikononi
nchini Tanzania ikiwa na wateja zaidi ya milioni 9.5.
Pia anamiliki Kampuni ya Caspian, ambayo inafanya kazi
za kuchimba madini katika migodi inayomilikiwa na Kampuni za BHP Billiton na
Barrick Gold.
Pia ana hisa katika Kampuni ya Hutchison Wampoa
inayofanya kazi za kupakua mizigo bandarini na anamiliki majumba nchini na
katika nchi za Mashariki ya Kati.
2) MENGI
Ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP.
Utajiri wake unatokana na kumiliki vyombo vya habari,
kiwanda cha vinywaji baridi na madini.
Mengi anamiliki magazeti kumi na moja, vituo vitatu vya
televisheni na takriban vituo 10 vya redio.
Pia ana mgodi wa madini ya dhahabu na viwanda vya
CocaCola.
Kwa mujibu jarida hilo, Mengi alizaliwa katika familia
maskini na baadaye kusomea uhasibu huko Uingereza na kufanya kazi huko.
Alijiunga na Chama cha Wahasibu cha Uingereza kabla ya
kurejea Tanzania mwaka 1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Ukaguzi ya Coopers &
Lybrand Tanzania (sasa Price Water House Coopers) hadi mwaka 1989, alipoacha
kazi na kujikita zaidi katika biashara.
3) BAKHRESA
Said Salim Bakhresa ni mwasisi na Mwenyekiti wa Kampuni
ya Bakhresa Group na ana utajiri wa Dola500 milioni (Sh783 bilioni).
Ni kampuni kubwa inayoajiri zaidi ya watu 2,000
ikijishughulisha zaidi katika kusaga nafaka, kusindika matunda, usafiri wa meli
na biashara ya mafuta. Pia kwa kutengeneza pipi na ice cream.
Bakhresa aliacha shule akiwa na umri wa miaka 14 na
kuanza biashara ya kuuza viazi mbatata. Baada ya hapo alifungua mgahawa na
baadaye kuingia katika biashara ya kusaga nafaka.
4) MO
Mafanikio yake yamechangiwa zaidi baada ya kuendeleza
mali ya wazazi wake. Anafanya biashara ya nyumba, kuuza mazao na viwanda vya
mafuta.
Mo alirejea Tanzania baada ya kumaliza masomo yake
katika Chuo Kikuu cha Georgetown, Marekani na kuendeleza biashara ya maduka
ambayo yalianzishwa na baba yake.
Alinufaika baada ya kununua viwanda vilivyobinafsishwa
na Serikali.
Alivifanya viwanda hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua
Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL) kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio
makubwa Tanzania.
Mo pia anajihusisha na biashara ya usambazaji bidhaa,
viwanda vya nguo na kilimo.
Jarida hilo lilipiga hesabu za utajiri wa
wafanyabiashara hao kwa kuangalia thamani ya bidhaa zinazouzwa na kampuni zao,
mikataba yao na hasa wale walio kwenye sekta ya mafuta na ukubwa wa kampuni
zao.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:
Post a Comment