Hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali kwa upande
wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA kinachonisukuma kusema kuwa tunachoona hivi
sasa ni historia. Bila kupoteza muda mrefu kujaribu kuzungumzia matukio naona
kuwa watanzania tungefaidika zaidi kuelewa vyema zaidi nini hasa tunachokiona.
Lazima tukubali kuwa lengo moja kuu (kama si lengo kuu
pekee) ya chama chochote cha kisiasa ni kuingia madarakani. Vyama hivi vinaweza
kutushawishi kuwa wanataka madaraka haya kwa sababu wanataka kutusaidia na ni
haki na wajibu wetu kutathmini na kuamua ni chama kipi kitatusaidia kama jamii
kufikia malengo tutakayokubaliana nayo. Lakini kwa kifupi wanataka madaraka.
Tukishakubali hali hii, basi tunaweza kuangalia tukio lolote la kisiasa kama
ushindani wa kutwaa madaraka. Na ni muhimu tutambue hili bila kujaribu kudai
kuwa eti mwanasiasa au chama fulani kinatupenda na kutujali zaidi na kadhalika.
Hilo ni suala la mtazamo na kwa sasa tuliweke pembeni.
Ninachotaka tujaribu kuangalia ni kuwa ushindani huu wa
kutwaa madaraka pia yapo ndani ya chama chochote cha kisiasa. Na ni kitu kizuri
sana. Naamini ndani ya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR tutaendelea kuona malumbano kwa
sababu ya uchaguzi mkuu 2015. Ni uchaguzi wa kihistoria kwa sababu rais aliyopo
madarakani hatagombea tena (hakuna incumbent) hivyo hata mgombea wa CCM atakuwa
‘mgeni’ kwa wapiga kura. Hivyo vyama vya upinzani vina nafasi kubwa sana
wakicheza karata zao vizuri. Lakini pia ndani ya CCM, hakuna mteule mpaka sasa
– kwa hiyo yoyote anaweza kuibuka kuwa mgombea. Tukishaweza kuangalia hali ya
kisiasa kwa jicho hili tutaona kuwa ndani ya vyama kuna makambi ambayo yanaona
kuwa wao wakiendesha chama sasa wanaweza kukihakikishia ushindi chama chao.
Hivyo uongozi wa chama nao unawaniwa. Na ninarudia hakuna ubaya wowote tena ni
kitu kizuri. Kwani asiyekubali kushindana si mshindani – na ukweli ni kuwa
mgombea ambaye atateuliwa tu na chama chake bila kupitia ushindani mkubwa ndani
ya chama chake, mara nyingi hawi mgombea mwenye ushwawishi mkubwa.
Ninakiri kuwa mi ni muumini wa ushindani katika nyanja
zote kwani ninaamini ushindani hatimaye huleta matokeo mazuri kwani maoni
mbalimbali yakigonganishwa basi tunaweza kupata kitu bora. Kwa bahati mbaya,
ushindani katika historia ya nchi yetu haikuwa neno zuri au dhana iliyokubalika
– katika sekta ya uchumi na hata siasa. Tunaweza kukaa na kuongea na kuleta
nukuu za Baba wa Taifa kuwa alipenda ushindani lakini ukweli halisia ni kuwa
kulikuwa hakuna uhuru wa kusimama na kum-challenge yeye kama kiongozi, au chama
(mfumo wa chama kimoja), ushindani wa kibiashara nk. Na ili kuweza kukamilisha
maoni yangu nitaomba tukiweke hiki kiporo, na mvumilie mawazo yangu kwa sasa.
Sasa basi ni katika historia hii ndo tunaona vyama vya
upinzani hapa nchini vilizaliwa na kwa kweli historia itakuja kutambua mchango
mkubwa wa wale wachache waliokuwa na uthubutu wa ku-challenge system wa wakati
huo. Lakini sasa kipindi kile cha awali cha kuunda umekamilika, kwani hivi leo
kuanzisha chama cha siasa, NGO au kampuni si kitu cha ajabu. Kinachofuata sasa
ni UIMARISHAJI wa vyama hivi.
Vyama hivi vinahitaji kuimarishwa kwa sababu ni lazima
vitoe taswira mpya na tofauti na chama kilichopo madarakani tangia uhuru – ya
kuwa demokrasia ya kweli ni mfumo yaani taasisi na si ya kikundi fulani. Na
hapo ndipo ninapoona tatizo. Vyama vya upinzani vimejaa kutokuaminiana. Hii
inatokana na kuwa wakati wa kuundwa kwao – juhudi za wazi na za siri
zilifanyika kuwahujumu na hadi leo hii juhudi hizi zipo kwani narudia kwenye
kile nilichokizungumzia hapo juu kuwa vyama vya siasa vinataka madaraka. Yule
aliyopo madarakani hatakubali kuondoka kwa hiari, hivyo ndiyo maana demokrasia
inahitajika kuhakikisha kuwa kwa njia ya wazi, anayekuwa madarakani anakubalika
na walio wengi, na hatimaye awapishe wengine. Sasa hapo ndipo tunapokuja na
kuleta dhana hii hii ndani ya chama chochote cha siasa. Ushindani huu ni muhimu,
ili kujenga imani. Na ningependa nitoe mfano wa nchi ya Marekani ambayo kwa
karne nyingi kumekuwa na ushindani wa kisiasa tena mkali sana.
Mwaka 1968 chama cha Democratic ilikuwa na mkutano wake
mkuu jijini Chicago yaani National convention. Wajumbe na wanachama walikuwa
wametofautiana mawazo kutokana na kuwa mgombea mmoja Hubert Humphrey (makamu
rais) alionekana kubebwa na kupendelewa na viongozi wa chama na rais wa wakati
huo Johnson (ambaye alitangaza kutogombea tena). Wanachama na wafuasi wa mgombea Eugene McCarthy walikataa matokeo
na maandamano makubwa yalifanyika katika eneo lililozunguka mkutano mkuu. Ni
vyema kujua pia kwamba McCarthy alikuwa mgombea pekee ambaye mapema kabisa
alikuwa tayari kum-challenge rais Johnson ambaye mwanzoni alikuwa tayari
kugombea. Katika kura za awali katika mkoa (state) ya New Hampshire, McCarthy
alipata 42% na Johnson 49%. Hii ilimshtua rais Johnson ambaye hatimaye alijitoa
na kumpendekeza makamu wake. Uthubutu wa
McCarthy ya kum-challenge rais aliyopo madarakani na kupata sapoti kubwa pia
iliwahamsisha wagombea wengine kuingia ulingoni kama Robert Kennedy ambaye
aliuwawa wakati mchakato wa uchaguzi wa ndani ukiendelea. Hivyo basi kwenye
mkutano mkuu, ushindani huu uligeuka kuwa ugomvi na mapigano kati ya wafuasi wa
McCarthy na kile kilichoonekana ni uongozi wa kimabavu wa chama. Polisi
waliitwa kutuliza ghasia na badala yake ghasia ilizidi, na wanachama wengi
walipigwa na kuumizwa napolisi. Humphrey alitangazwa mshindi ingawa ushindi
wake ulikuwa wa mashaka kwa wanachama wengi. Na Humphrey alienda kugombea urais
na hatimaye kushindwa vibaya katika uchaguzi mkuu.
Je chama cha Democratic ilifanya nini? Ilimtimua Eugene
McCarthy? Iliwatimua wafuasi wake? Hapana. Mara baada ya uchaguzi mkuu, uongozi
wa Democratic party ulikaa na kuunda kamati iliyoongozwa na Senator George
McGovern na baadaye Donald M Fraser. Na mabadiliko makubwa yalifanyika NDANI ya
chama – ikiwa ni pamoja na kuwa na UWAZI mkubwa zaidi hususan katika chaguzi
mbalimbali. Matokeo yake ni kuwa katika mikoa au states mbalimbali walianzisha
mfumo wa primaries – yaani ngazi ya chini kabisa wanachama waliweza kupiga kura
ya mgombea wanayemtaka. Si tu wagombea wa serikali za mitaa, bunge yaani Senate
na House of Representatives, lakini hata za rais – presidential primaries.
Kupitia njia hii ya wazi, chama cha Democratic ilijikuta kuwa hata kufikia
1984, mmarekani mweusi wa kwanza alitaka kuwa rais wa Marekani – Jesse Jackson
– na alithubutu na kujaribu kutwaa ugombea rais wa chama ingawa hakufanikiwa.
Hatimaye 2008, mmarekani mweusi Barack Obama alifanikiwa kuutwaa ugombea rais
wa chama chake kama mwanasiasa mgeni asiye na uzoefu mkubwa – akimbwaga Hillary
Clinton ambaye alikuwa ameshachukuliwa na viongozi wa chama kuwa ndo mgombea
mteule. Kupitia mfumo huu wa uwazi, Obama na Hillary walichuana vikali sana
kiasi kwamba wataalam wa masuala ya siasa wanasema Obama alipata mikikimikiki
mingi zaidi katika uchaguzi wa ndani ya chama kuliko wakati wa uchaguzi mkuu.
Mfano mzuri ni kashfa ya mchungaji wake Rev Wright ambayo iliibuliwa na kambi
ya Hillary Clinton. Kambi ya Hillary pia iliandaa matangazo ya TV na radio ya
kumbeza Obama kuwa akiamshwa usiku wa manane kuwa kuna janga limetokea
atashindwa kutoa suluhu kwa sababu si mzoefu. Matangazo kama haya yalikuwa
mengi kwa kambi zote mbili, ila Hillary Clinton alianza na pesa nyingi na
sapoti ya viongozi wa chama. Lakini kama tunavyojua Obama alitumia mbinu ya
kutafuta sapoti ya wanachama wapya – hususan vijana na wafanyakazi. Swali je
Obama na timu yake wangekuwa Tanzania wangeruhusiwa kugombea?
Mfano huu wa Marekani utatusaidia vipi kuelewa hali ya
sasa hivi? Chama chochote nchini si tu CHADEMA ni lazima iwe tayari kufanya
yafuatayo ili iendelee kuimarika:
Uwazi mkubwa katika uongozi wake – katika matumizi ya
fedha na kadhalika
Ushindani wa wazi katika kuwania uongozi na kuhakikisha kuwa uongozi uliopo madarakani
inaweza kuwa challenged kwa uwazi
Mfumo au utaratibu wa wazi wa kugombea nafasi za uongozi
– primaries kwa ngazi zote
Lakini mi si mtaalam wa masuala ya siasa na ninaamini
katika vyama vyote wataalam wapo wengi na wasomi wanaoweza kuja na reform ya
chama chao ili kurudisha imani miongoni mwao.
Hivyo basi tunachokiona leo hii ndani ya CHADEMA ni
changamoto kubwa lakini pia ni nafasi ya kipekee kwa chama hiki kikubwa cha
upinzani kuandika historia. Kwani suluhu si kutimuana, “kuvuana nguo”, kuitana
majina – hii itafanyika wakati wa mchakato rasmi – ila kwa sasa ni muda wa
kujitafakari. Ni nafasi ya kipekee kwa chama hiki kukaa na kutafakari na
kupokea ukosoaji wote wa pande zote na kisha kuzifanyia kazi. Huu si wakati wa
kurudi kwenye dhana ya zamani ya kusema eti ushindani ni kitu kibaya. Wananchi wengi nilioongea nao na kuwasiliana
nao wanaonyesha hofu na wamekata tamaa wakisema chama hiki kikubwa cha upinzani
kikipasuka hakuta kuwa na ushindani wa vyama. Mi binafsi nasema mpaka sasa
tamko la Zitto na la Kitila kuwa hawaondoki ndani ya chama na watabaki ni
habari njema. Kwani mikwaruzano, na malumbano haya ndani ya chama kinaweza
kuimarisha chama kama pande ZOTE zitaweza kutambua kuwa lengo lao kuu hatimaye
ni kushika madaraka ya nchi. Na sisi wananchi tutambue kuwa katika ushindani
huu hakuna malaika wala shetani, ni mgongano wa mawazo.
Hivyo basi katika ushindani huu ndani au nje ya chama –
tujue kuwa ile principle ‘All is fair in love and war” – yaani kila kitu ruksa
katika vita na mapenzi – hata hapa hutumika. Ninamaanisha kuwa ili kutwaa
madaraka, pande zote zitapanga mikakati, zitajadili njia za kumdhoofisha
mpinzani wake, zitatumia njia hata za kutuma ‘majasusi’ wa kisiasa kupata
taarifa kuhusu pande wa pili, zitatoa taarifa za uongo za kuchafuana, zitatumia
uzushi. Hii pia ni sawa kabisa na si kitu cha ajabu. Tusijidanganye, huu ni ushindani
tena mkali. Upande utakaokataa kuwa haifanyi au haitumii mbinu hii utakuwa
hausemi ukweli au utapotea bila kujielewa. Siasa ya vyama vingi ni ya ushindani
na ushindani si lelemama. Kama kuna mtu anadhani Obama aliingia Ikulu ya
Marekani kwa huruma, na kambi yake haikutumia mbinu na hila basi anajidanganya.
Kama mtu anafikiri kuwa Magreth Thatcher aliongoza Uingereza kama waziri mkuu
kwa sababu waingereza walimwonea huruma, wajue wamepotoka. Kama mtu anafikiri
Tony Blair au David Cameron waliingia madarakani kutokana na ujana wao tu,
wanahitaji kusoma zaidi historia. Viongozi wote hawa wameshika madaraka
kutokana na kuwa walijiandaa mapema tena kwa SIRI, walikuwa na timu kali
iliyowapangia mikakati yao ya ndani ya siri. Kuna wataalam wa mikakati yaani
political strategists ambao wanafanya hii kazi kitaalam na huajiriwa na kambi
za wagombea ili kuwaandikia mikakati. Hii si kitu cha ajabu na muda umefika
hata sisi Tanzania tuwe tayari kuona ukweli kuwa pande zote husika katika siasa
zetu, ndani na nje ya vyama vya siasa hutumia mbinu na hila. Kusema eti kambi
fulani haiitumii mbinu na hila ni uongo, wako katika ushindani mkali wa
kudhoofishana machoni mwa wanachama wao. Hivyo utasikia kambi moja inamwita
mgombea mtarajiwa wa kambi nyingine “msaliti”, kambi nyingine inamwita mgombea
mtarajiwa wa pande wa pili “mbadirifu”.
Lakini lazima wakiri hatimaye kuwa wanachogombania ni madaraka. Angalau
katika mkutano wao na waandishi wa habari, Zitto na Kitila wamekuwa wa kweli na
kukiri hilo. Pande wa pili pia ifanye hivyo ili sasa ushindani wa wazi uanze.
Lakini pia ikumbukwe kuwa katika harakati hizi chama kitakachokinzana na
CHADEMA yaani CCM inatumia fursa hii kuwadhoofisha – na itaendeleza ushindani
huu wa kutwaa uongozi wa ndani ya chama na kuukuza. Na hii pia ni sehemu ya
ushindani wa kisiasa. Hatutakiwi kukataa au kujidanganya katika hili.
Sasa kitu ambacho
sikubali kabisa ni pale watu wanapojaribu kusema eti “hii ni Tanzania, hatuendi
hivyo”. Mi naomba nijibu hiyo hoja – demokrasia na mfumo wa vyama vingi
havikutungwa Tanzania. Kama tumekubali kutumia huo mfumo tufuate kama
ilivyolengwa. Vinginevyo turudi kwenye uchifu. Tanzania tunaweza kujenga jamii
ya kidemokrasia na itajengwa na SISI
wananchi na si wanasiasa. Kwa sababu wanasiasa wako bize kutwaa madaraka -
mwanasiasa yoyote yule – tusidanganyike! Hivyo basi sisi wananchi tukiwa kama
wanachama wa vyama, kama wapiga kura, tuhakikishe tunakuwa mashabiki wa
demokrasia na uwazi kwanza na si mashabiki wa vyama na wanasiasa.

0 comments:
Post a Comment