Angola imeripotiwa kuipiga marufu dini ya Kiislamu na
kuanza kubomoa misikiti, na hivyo kuwa nchi ya kwanza ulimwenguni kuchukua
hatua hiyo.
Siku ya Ijumaa, magazeti kadhaa katika nchi hiyo ya
kusini mwa Afrika yalidaiwa kumnukuu Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo, Rosa
Cruz e Silva, akisema kuwa “mchakato wa kuuhalalisha na kuuruhusu Uislamu haukuidhinishwa
na Wizara ya Sheria na Haki za Binadamu... hivyo misikiti itafungwa mpaka
taarifa zaidi itakapotolewa."
Silva alidaiwa kusema kuwa marufuku hiyo ni muhimu kwa kuwa
Uislamu “unapingana na desturi za utamaduni wa Angola."
Baada ya hapo serikali ilianza programu ya ubomoaji wa
misikiti na maeneo mengine ya Waislamu kama sehemu ya marufuku hiyo.
Uamuzi huo ni hatua mpya kabisa ya mlolongo wa jitihada
za kupiga marufuku kile ambacho maafisa wa Angola wanakiita kuwa ni “madhehebu
haramu ya dini.”
Hata hivyo, Mzizima 24 inaendelea kufuatilia kwa karibu ripoti
za marufuku hiyo dhidi ya Uislamu, kwa maana hazijathibitishwa na vyanzo huru ,
kwa kuwa katiba ya Angola inatoa uhuru wa kuwa na dini kwa raia wote wa nchi
hiyo.
Jana Jumatatu, afisa mmoja kwenye Ubalozi wa Angola
mjini Washington D.C. alikanusha taarifa za nchi yake kuupiga marufuku Uislamu,
akisema kuwa “Jamhuri ya Angola… ni nchi isiyoingilia masuala ya dini.”
“Tuna dini nyingi kule. Kuna uhuru wa dini. Kuna Wakatoliki,
Waprostanti, Wa-Baptist, Waislamu na
hata Walokole,” alisema afisa huyo.
Mwezi Oktoba, Waislamu wanaoishi manispaa ya Viana Zango
mjini Luanda, walipigwa na butwaa baada ya kukuta mnara wa msikiti wao ukiwa
umevunjwa vipande vipande. Mamlaka za serikali hazikutoa maelezo yenye
kujitosheleza kuhusu hatua hiyo.
Idadi ya raia wa nchi hiyo yenye wakazi milioni 19, ni
Wakristo. Kuna Waislamu wanaokadiriwa kuwa 80,000 mpaka 90,000, na idadi yao
inaongezeka.
0 comments:
Post a Comment