![]() |
| Mwanamke wa Kipalestina na wanaye wakiwasha mishumaa baada ya ukame wa umeme kulikumba eneo la Gaza Novemba 10, 2013. |
Na Kabuga Kanyegeri
ENEO la Ukanda wa Gaza linakabiliwa na hali mbaya ya
kibinadamu ambapo Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo la pwani wameendelea
kukosa umeme kutokana na mzingiro wa miaka 6 ulioweka na utawala wa Israeli
katika eneo hilo.
Mzingiro huo unawafanya wakazi hao kutokuwa na uwezo wa
kuingiza bidhaa na huduma mbalimbali.
Hali ya kibinadamu imezidi kuwa mbaya kutokana na kinu
pekee cha kufua umeme kusitisha shughuli zake tangu Novemba 1 kutokana na
ukosefu wa mafuta.
Katika miezi ya hivi karibuni, upungufu wa mafuta na
umeme umekithiri na kushtadi baada ya jeshi la Misri kuziba na kuzifunga njia
za chini kwa chini zilizokuwa zikisaidia kupeleka bidhaa na huduma katika eneo
hilo. Njia hizo zilikuwa zikisaidia kuokoa maisha ya wakazi wa Gaza wapatao
milioni 1.7.
Wakati huo huo, maafisa katika eneo la Gaza wanasema
kuwa baadhi ya wakazi hao wameanza kutumia maji machafu kutokana na mashine ya
usafishaji wa maji kuacha kufanya kazi kutokana na ukame wa nishati.
Kinu hicho cha kusafisha maji kilikuwa kikiwahudumia
wakazi 120,000. Maafisa hao wanasema kuwa mashine nyingine zitaacha kufanya
kazi hivi karibuni kutokana na ukosefu wa nishati. Manispaa ya mji wa Gaza
imetangaza hali ya dharura, na wataalamu wameonya kutokea kwa janga la
kimazingira.
Ukanda wa Gaza umekuwa katika mzingiro tangu mwaka 2007,
hali ambayo imewafanya Wapalestina hao kutegemea bidhaa na huduma kuwafikia
kupitia njia za chini kwa chini ambazo zimefungwa na watala wa sasa wa Misri.
Mtandao wa mashirika na taasisi za Kipalestina (PNGO),
ambao unawakilisha zaidi ya taasisi 130 za kiraia, umetoa wito kwa jumuiya ya
kimataifa kukomesha mzingiro huo unaondelea kufanywa na utawala wa Israeli.
Mashirika kadhaa ya kiraia na ya haki za kibinadamu
yamelikosoa jeshi la Misri kwa kuwanyima wakazi wa Gaza nafasi ya kupata huduma
nyingi za msingi kama vile vifaa vya ujenzi, chakula na nishati.

0 comments:
Post a Comment